Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, September 20, 2011

Mada yangu ya leo: Kumekucha


Wakati majadiliano ya madai ya katiba mpya yanaanza niliwahi kuandika makala kwenye safu yangu ya Letter from Butiama, iliyopo kwenye gazeti la Serikali, Daily News, nikitabiri kuwa yatatokea makundi tusiyoyatarajia katika mchakato huu wa kudai haki ndani ya katiba mpya.

Baadhi ya makundi hayo yameanza kuibuka, gazeti la Majira linaripoti. Toleo lake la Septemba 16, 2011 linanmnukuu mwakilishi wa kundi la mashoga akidai nao watambuliwe ndani ya katiba mpya ili kulinda haki zao kama raia. Alinukuliwa akisema kuwa hubaguliwa wanapoomba kazi na kwa kukosa ajira wanaendelea na tabia ambazo hazikubaliki ndani ya jamii.

Hoja yangu, ambayo niliitoa kwenye makala yangu ya Kiingereza kwenye gazeti la Daily News ni kuwa suala zima la mabadiliko ya kikatiba linajikita kwenye kumpa fursa kila raia kufurahia uraia wake bila bugudha toka kwa mtu, taasisi, au kundi lingine lolote la raia. Katiba pia inaainisha wajibu wa raia katika masuala mbalimbali.

Lakini tatizo ni kuwa kwenye nchi nyingi huwa hakuna makubaliano ya mipaka ya haki hizi, na wakati nchi nyingine zinaainisha haki kwa makundi fulani ya raia wake, nchi nyingine zinaweza kuweka marufuku kwa haki hizo hizo kwa makundi ya aina hiyo.

Mfano niliotoa kwenye makala yangu ni kuwa baadhi ya nchi zimepitisha sheria zinazoruhusu ndoa za jinsia moja wakati suala hilo ni ukiukwaji wa sheria kwenye nchi nyingi duniani. Rais Robert Mugabe, ambaye ni mpinzani mkubwa wa sera hizi akihutubia nchini Zimbabwe alisema kuwa sheria hizi zinataka kuruhusu "bibi yangu (nyanya) mzazi kuona na bibi yako."

Kwetu sisi migongano hiyo sasa imefika. Raia shoga anadai haki za kikatiba. Kwa misingi ya wale wanaotufundisha kuwa kila raia anapaswa kuwa na haki chini ya katiba ya nchi ni dhahiri kuwa raia huyu anapaswa kupewa haki zake ndani ya mabadiliko mapya ya katiba.

Iko hoja itakayotolewa na waumini wa dini kadhaa, kuwa suala la ushoga ni kinyume na mafundisho ya dini. Lakini misingi ya kikatiba na haki kwa raia inakinzana na maadili kama haya ya kidini. Kwa mitazamo hiyo hiyo ya haki kwa kila raia, raia wote – wenye dini na wasiyo nayo – wanapaswa kupata haki ile ile ya msingi chini ya katiba.

Kwa mantiki hiyo, yoyote anayepinga ushoga kwa misingi ya dini anaweza kujibiwa kuwa suala la dini haliwezi kuwa kigezo kwa raia ambaye hana dini na anayedai haki zake chini ya katiba.

Maadili, mila na desturi, na tamaduni vimekuwa vigezo vinavyoongoza jamii zetu tangu enzi za mababu na bado zinaongoza jamii katika sehemu nyingi za Tanzania ambapo vigezo hivi vinatumika. Lakini maingiliano na wageni yameleta na yanazidi kuleta vigezo vipya ambavyo vitaleta mkanganyiko mkubwa ndani ya jamii kwa ujumla, na hususani ndani ya huu mjadala wa katiba mpya.

Ni dhahiri kuwa kuna mengi yatapingwa kuhusu hivi vigezo vipya na kuna uwezekano mkubwa kuwa Watanzania wengi hawatakubali kuingizwa kwa haki za mashoga kwenye katiba. Lakini litakapokataliwa ina maana kuwa tutakuwa tumeamua kuchagua 'yanayotufaa' na 'yasiyotufaa'. Na uamuzi kuwa hili linafaa na hili halifai unakinzana na azma ya kumpa kila raia uhuru wa kuwa kile anachotaka kuwa. Kwa maana nyingine, kuna mipaka ya kitamaduni inayoshinikiiza kuwa siyo kila uhuru utakubalika ndani ya jamii ya Kitanzania.

Siyo kazi rahisi kuongoza Serikali katika nyakati hizi za sasa. Zamani ilikuwa rahisi kusema hili halifai, na hili linafaa. Siku hizi kila mtu ana haki. Siku hizi tunaambiwa hata watoto ambao bado wanajikojolea kitandani wanapaswa kupewa uhuru wa kuamua wanayoyataka wao.

Ni mkanganyiko usio mdogo. Ndio maana nasema, kumekucha.

No comments: