Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, April 16, 2012

Mada yangu ya leo

Nilikuwa katikati ya Jiji la Dar es Salaam tarehe 14 Aprili 2012 niliposikia taarifa kuwa tetemeko kubwa la ardhi lilitokea nchini Indonesia na limesababisha kuzuka kwa wimbi la Tsunami kwenye Bahari ya Hindi na kuwa wimbi hilo lilitarajiwa kufika kwenye fukwe za Afrika Mashariki jioni ya siku hiyo hiyo.

Wakazi wa Dar es Salaam walitahadharishwa kuhama maeneo yaliyo karibu na bahari, na nilishuhudia wengi wao ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa maofisini kwenye majengo yaliyopo katikati ya Jiji wakiondoka kwa wingi kwenye majengo hayo na kuelekea maeneo ambayo yangewaepusha na janga la kukumbwa na Tsunami.

Ilikuwa ni siku ya mvua kubwa, na kama ilivyo kawaida jijini Dar es Salaam inaponyesha mvua kubwa, kulikuwa na msongamano mkubwa sana wa magari katikati ya Jiji na maeneo ya Upanga, maeneo ambayo nilipita nikitembea kwa mguu. Naamini hali ya msongamano ilikuwa hivyo hivyo kwenye maeneo karibu yote ya Jiji ikiwa ni pamoja na kwenye barabara kuu zinazopita kandokando ya Bahari ya Hindi, sehemu ambayo ilikuwa na hatari kubwa zaidi kukumbwa na Tsunami.

Baadaye siku hiyo niliamini kuwa Mwenyezi Mungu ana upendeleo mkubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam baada ya kusikia taarifa kuwa tishio la Tsunami halikuwa kubwa kama ilivyotabiriwa awali na hatari yoyote kwa maisha ya watu na mali ilitoweka.

Ukweli ni kuwa wimbi hilo lingefika Dar es Salaam kwa kishindo kile kile tulichoshuhudia nchini Japan basi kwa hakika tungeshuhudia maafa makubwa sana. Wakazi wengi wa Jiji hilo wangekutwa ndani ya magari yao au ndani ya daladala kutokana na msongamano mkubwa wa magari ambayo yalikuwa yakisogea hatua chache tu baada ya muda mrefu.
posted from Bloggeroid

No comments: