Mapema kwaka 2000 nilipewa jukumu la kumtambulisha mgeni kwa kundi la wenyeji waliofika kumpokea huyo mgeni nyumbani Butiama. Kabla ya mgeni kufika nilichukuwa kalamu na karatasi na kumuuliza aliye karibu nami jina lake na akanitajia jina na ubini wake. Cha ajabu, alikuwa na ubini kama wangu. Baadaye niligundua kuwa ni mmoja wa baba zangu wadogo.
Niliona aibu sana, lakini naamini kuwa ninayo sababu nzuri ya kutomfahamu. Marehemu babu yangu, Mtemi Nyerere Burito, alikuwa na wake 22. Aidha alikuwa na kina mama wa nyumba ndogo wanne ambao kwa kabila la Wazanaki wanajulikana kama
vitungo. Kutokana na uzao wa babu na wake zake, mimi nina ndugu na jamaa wanaokaribia 6,000 kwa hiyo kumfahamu kila mmoja wao siyo jambo rahisi.
Kwa kawaida, uzao uliyonitangulia ulikuwa na watoto wengi, lakini iwapo nitachukuwa wastani wa watoto sita tu kwa kila mme na mke kwa ajili ya kukadiria idadi ya uzao wa Mtemi Nyerere, nikianza na bibi zangu ishirini na wawili, napata idadi ya baba wadogo/shangazi 132, watoto wa baba wadogo/shangazi 792, na wajukuu wa baba wadogo/shangazi 4,752, ikiwa ni jumla ya ndugu 5,676. Na hii ni kutoka upande wa baba mzazi tu.
|
Kaburi la Mtemi Nyerere Burito, kulia, pamoja na kaburi la mke wake wa tano, Christina Mgaya wa Nyang'ombe, kushoto, katika eneo la Mwitongo kwenye kijiji cha Butiama.
Hata iwapo watapunguzwa wale waliofariki, bado inaacha idadi kubwa ya majina na sura ambazo si rahisi kuzikumbuka, pamoja na kuzingatia kuwa kukumbuka ndugu ni suala linaloweza kujenga mahusiano mazuri kwenye familia kubwa. Swali moja ambalo naulizwa mara kwa mara ninapokutana na ndugu ambao siwafahamu vizuri ni: "Unanifahamu mimi?" Ninapokuwa namfahamu mambo huenda vizuri lakini pale ninaposhindwa kumtambua nakuwa mtu nisiefaa kabisa, nachukuliwa kama mtu ambaye hafanyi jitihada ya kutosha kuwafahamu ndugu zake.
|
|
Sehemu ya wanaukoo wa Burito Nyerere wakiwa |
Hivi karibuni nilikutana na binamu zangu wawili ambao mama yao, marehemu shangazi yangu, ni binti wa tatu wa mke wa saba wa Mtemi Nyerere Burito. Pamoja na kuwa anakaribia miaka 50, mmoja wa wale binamu zangu hakuwa ananifahamu, na alikuwa hajawahi kusikia jina langu. Ilikuwa ni faraja kubwa sana kwangu kwa sababu ilikuwa ni ushahidi tosha kwangu kuwa tatizo la kutoweza kuwatambua ndugu zaidi ya 5,000 halikuwa linawakumba tu wale waliokaa sana jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment