Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, February 4, 2013

Amani Millanga ahoji ukodishwaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji (sehemu ya tatu kati ya sehemu tatu)


Katika sehemu ya tatu na ya mwisho ya makala yake hii ambayo nimeitoa katika sehemu tatu, Amani Millanga anahoji ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji na, kwa maoni yake, utaratibu huu unaturejesha kwenye ukoloni.

**********************************************************
Mali ya Taifa (sehemu ya tatu)

Na Amani Millanga

Tanzania ya leo imejaa watoto wengi wa mitaani. Katika kusherehekea miaka 100 ya uhuru mwaka 2061 kizazi hiki cha maskini hohehahe wasio na ardhi kitakuwa kimeongezeka sana kwani hakuna jitihada za makusudi za kupambana na ongezeko la watoto wa mitaani. Hawa watakuwa ni watumwa katika Tanzania iliyojaa walowezi. Lakini historia ya wanadamu inaonyesha kwamba binadamu hudai haki zao. Kizazi hiki kitadai ardhi. Itapatikana wapi ardhi ya kuwapa? Katika hiyo benki ya ardhi?  

Nchi yetu inapaswa kujifunza kutoka kwenye makosa makubwa yaliyofanyika katika uwekezaji katika uchimbaji madini ambao kimsingi ni UWIZISHAJI. Mali ya taifa inaporwa kwa kutumia sheria za nchi. Tunaachiwa mazingira yaliyoharibiwa na kemikali na mashimo. Nasikia mashimo hayo yatageuzwa kuwa mabwawa ya kufugia samaki. Kichekesho kwelikweli. 

Jambo la kusikitisha ni kwamba fikra bado ni zilezile ,“wanaokodisha ardhi watatoa ajira, watakuza uchumi na kuwasadia wakulima wadogo.” Kwa kutumia hesabu za pato la taifa (GNP) wanatuonyesha kwamba uchumi utakua lakini ukuaji huo utakuwa mikononi mwa walowezi na wala hautawafikia Watanzania wengi vijijini na mijini.

Tufahamu kwamba wanaokodishiwa ardhi wamekuja kuchuma (kunyonya) na kupeleka mali kwao na wala si kuinua uchumi wa Mtanzania au kumlisha Mtanzania. Na huu ni wizi wa ajira na mapato ya Mtanzania. Kwa jembe la mkono Tanzania inajitosheleza kwa chakula na inalisha nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan ya Kusini, Somalia, Malawi na hata Zambia. Kama tunaweza kuwalisha jirani basi tunaweza kuwalisha Waarabu, Wakorea, Waingereza, n.k. 

Hivi kuna uharamu gani kwa Mtanzania kuzalisha embe na nanasi zikauzwa Uingereza, mchele ukauzwa Saudi Arabia na Qatar, nyanya zikauzwa Korea na machungwa yakauzwa popote pale duniani? Ni wapi tunashindwa? Je tumeshajiuliza ni kwa nini tunashindwa? Je tumeshatafuta dawa mujarabu ya kutuwezesha kuzalisha kwa ubora wa kimataifa ya kuliteka soko? Kama jibu ni ndiyo, kwa nini tunaendelea kukodisha ardhi tena kwa bei ya chee kwa wageni? Kama jibu ni hapana, kwa nini wenye jukumu la kumuwezesha Mtanzania kuzalisha kwa kiwango kikubwa chenye ubora wa kimataifa hawawajibishwi? Wanapaswa kuwajibishwa kwa sababu wanahujumu uchumi na ustawi wa nchi kwa kuwatelekeza wakulima.    

Hivi kweli tunashindwa kuufufua ushirika? Je tunashindwa kumwezesha mkulima mdogo akawa mkulima mkubwa? Haya yote yanawezekana kikwazo kikubwa kilichopo ni kwamba nia ya dhati ya kuinua maisha mkulima haipo. Hili linatokana na kuendelea kukumbatia sera za Benki ya Dunia na IMF ambazo zinaukomaza zaidi mfumo wa kinyonyaji wa kibeberu na kuwaharibia maisha Watanzania. Ni wakati muafaka sasa kwa serikali kuacha kukodisha ardhi yetu kwa walowezi. Kuendelea kwa zoezi hili kutaiangamiza Tanzania. Hatupaswi kuufumbia macho ukweli huu.

No comments: