Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, April 22, 2013

Safari hii Bunge limepata wabunge

Yaliyotokea bungeni hivi karibuni yanashangaza kidogo. Hapana, yanashangaza sana.

Baadhi ya wabunge wameamua kuvua majoho ya staha na heshima kati yao na kujitwika majoho ya kejeli, na lugha ambazo hazina ustaarabu hata kidogo. Inaelekea kuwa wanasahau kuwa mamilioni ya Watanzania wanawasikia na kuyaona wanayotenda.

Aliyetoa wazo kuwa majadiliano ya bungeni yasionyeshwe moja kwa moja kwenye televisheni anaweza kuwa ana hoja nzuri. Kwa kuona malumbano na mabishano yanayoendelea bungeni wapiga kura tunaona kama vile baadhi ya kura zetu zilikwenda kusikostahili.

Wakati mwingine ukisikiliza majadiliano yanayoendelea ndani ya bunge unaweza kufikiri siyo bunge bali ni mkutano ambao hauna kanuni wala taratibu. Huyu anabishana na mbunge mwenzake, wakati mwingine anabishana na Naibu wa Spika.

Nikiwa ndani ya gari nilisikia mbunge mmoja akiongea bungeni na kushauri serikali iidhinishe ulimaji wa bangi. Mwingine tena katika majadiliano akaporomosha tusi la nguoni kwa lugha ya Kiingereza ambalo sidhani kama limewahi kutamkwa kwenye mabunge yanayotumia lugha ya Kiingereza. Mwingine (lakini huyu aliomba radhi) akamwambia mheshimiwa mwenzake kuwa yeye haongei na mbwa, bali anaongea na mwenye mbwa.

Siyo wabunge wote wanaojihusisha na hii sura mpya ya bunge lakini mtiririko huu wa matukio na matamshi yanayotoka bungeni unatishia kushusha hadhi ya bunge kama chombo kimoja muhimu katika jamii.

Baadhi ya wabunge wanapaswa kukumbushwa kuwa wanao wajibu wa kuonekana kuwa na tabia ambazo jamii inatarajia kiongozi kuwa nayo. Nayo ni pamoja na kuonyesha ustahamilivu kwa wale wanaoweza kuwa na mawazo tofauti, na hata pale ambapo mawazo yanatofautiana basi kupingana bila ya kuonyesha dharau na kejeli. Kama tutaendelea na lugha hizi bungeni basi bado kidogo tutashuhudia bunge letu linakuwa ulingo wa ngumi.

No comments: