******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012
makala ya John Kitime
(Sehemu ya nne kati ya sehemu nne)
Ikiwa kulikuwa na mchango wa serikali katika muziki, basi ulikuwa mdogo au ulikuwa ni kwa shughuli maalumu lakini si kwa kutengeneza mazingira ya kuwezesha unafuu kwa wanamuziki kwa ujumla. Idara ya Utamaduni imeendelea kupata bajeti ndogo ambayo imefanya Baraza La Sanaa La Taifa kuendelea kubaki Dar es Salaam tu, likibangaiza kuweko kwa kutegemea kutoa vibali mbalimbali kwa wasanii, na nguvu zake kuonekana Dar es Salaam tu. Na kwa kuwa hakuna Maafisa Utamaduni Mkoa, na Maafisa Utamaduni Wilaya na Manispaa wako chini ya serikali za mitaa hivyo kuwa wizara tofauti na Waziri wa Utamaduni, nguvu za serikali katika utamaduni ni 0.
COSOTA,
chombo ambacho shughuli yake ilikuwa ni kulinda hakimiliki za wasanii na
ambacho kilikuwa chini ya wasanii, kwa kinyemela kabisa kimerudishwa katika
mikono ya serikali, lakini bado kinakusanya mirabaha 'kwa niaba ya wasanii'
huku kukiwa na bodi isiyo na uwakilishi wa wasanii kuanzia 2007. Swali:
utakusanyaje pesa kwa niaba yangu lakini huniruhusu kujua ni kiasi gani
umekusanya, unazitumiaje na ukiulizwa unakuwa mkali!!!!!!? Kuna wasanii
wamekuwa wakidai kurudishiwa COSOTA, ushauri wangu wasanii wakae
wajipange na kuelewa vizuri sheria ya Hakimiliki kabla ya kujitwishwa
zigo hilo la miba.
Katika
miezi sita ya mwisho ya 2012 kumejitokeza spidi kali ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa
Mapato kutengeneza mazingira ya kukusanya mapato kutokana na mauzo ya kazi za
muziki na filamu. Kimsingi kulipa kodi ni wajibu wa kila mwananchi na wasanii
ni wananchi pia, lakini taratibu zake ndiyo zinanipa utata, hasa pale ambapo kwa
muda mrefu imekuwa ikitangazwa kuwa njia hii itasaidia wasanii kwa kupunguza
kuibiwa.
Sentensi
hii inaonyesha wazi anayeiongelea au hajui mfumo wa biashara ya kazi muziki,
au kwa makusudi anapotosha ili kuficha kitu. Wasanii wengi huwa wamekwishalipwa
kwa kazi ambazo zimesambaa na ziko barabarani zinaibiwa, wanaoibiwa ni
wasambazaji. Hivyo kulinda kazi hizo unamlinda msambazaji si msanii. Pia kuanza
kukusanya kodi kwa kazi hizi kumepewa jina ‘kurasimishwa kwa kazi ya usanii’.
Kuna mabilioni wasanii
wanatakiwa walipwe na watumiaji wa kazi za sanaa, kama redio na TV, mapromota,
waajiri na kadhalika lakini hakuna anaeliongelea hilo wala hakuna anaetamka
takwimu hizo. Kuna kazi ya kurudisha mitaala ya masomo ya sanaa mashuleni,
kurudisha vyuo vya walimu wa sanaa, kurudisha maafisa utamaduni kuwa chini ya
Wizara ya Utamaduni kuwawezesha kufanya kazi zao kadiri ya Sera ya Utamaduni, na
mengine mengi ya aina hiyo ndiyo ningeona kurasimisha kazi za sanaa. Lakini
kukusanya kodi tu kwa kazi ambazo hata hivyo mikataba yake mingi inautata na
kuita urasimishaji si sahihi.
Katika
nchi nyingi critics au watu ninaoweza
kuwaita Kiswahili wakosoaji, huwa ni muhimu katika maendeleo ya sanaa. Watu
hawa hupata heshima kutokana na kuweza kuangalia mapungufu katika kazi za sanaa
na kuyasema, jambo ambalo hupelekea wasanii kujirekibisha na kutengeneza kazi
bora zaidi. Hapa kwetu kutoa ushauri ni kutafuta matusi, toka kwa wasanii wenye
kazi husika, vyombo vya habari na hata sehemu ya jamii. Umefika muda wahusika
kuchukua uchambuzi kama changamoto za kuboresha kazi.
Niliyoyataja
hapa yote yako wazi. Ninachotegemea ni kuona 2013 hatua zinaanza kupigwa
kurekebisha ili wanamuziki wa nchi hii nao wapate nafasi sawa na wengine wa
nchi nyingine.
John
Kitime
31.12.2012
Sinza,
Dar es Salaam
Taarifa zinazohusiana na hii:
No comments:
Post a Comment