Nilimsindikiza mwekezaji mmoja
kwenye ofisi ya kanda ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania kuwasilisha maombi ya
kusamehewa malipo ya kodi ya nyongeza ya thamani kwa mujibu wa sheria ya
uwekezaji. Taratibu zinataka muombaji afuate hatua hizi:
1. Achukue
ankara kwa muuzaji wa bidhaa ambazo zinaombewa msamaha
2. Ajaze
fomu maalumu ya maombi ya kusamehewa kodi ya nyongeza ya thamani
3. Awasilishe
katika ofisi ya Mamlaya ya Mapato Tanzania fomu (kwenye mkoa ambako mradi
unaendelezwa) ili idhini ya kusamehewa kodi itolewe; na
4. Arudi
kwa muuzaji na kulipia bidhaa bila kodi na kuchukuwa hivyo vifaa
Tatizo liko katika ngazi nyingi.
Kwanza, taratibu zote za kuomba misamaha ya kodi au zinafanyika Dar es Salaam
au kwenye makao makuu ya Kituo cha Uwekezaji na Mamlaka ya Mapato Tanzania, au
kwenye ofisi za kanda za kituo cha uwekezaji. Ofisi hizi za kanda siyo nyingi
kwa hiyo, kwa mwekezaji ambaye hayuko Dar es salaam au jirani na ofisi za kanda,
inamlazimu aingie gharama kubwa ya
kusafiri mara kwa mara kati ya eneo la mradi kwenda kwenye maeneo hayo ambapo
maamuzi ya kusamehewa kodi yanachukuliwa.
Si hivyo tu, lakini kwa mwekezaji
ambaye hayuko Dar es salaam au jirani na mji mkubwa hulazimika mara kwa mara
kupata mahitaji ya vifaa vya ujenzi kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania.
Mathalani, kwa mwekezaji aliyeko Butiama, anahitaji kusafiri mara kwa mara
kwenda nje ya mkoa wa Mara kununua vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mwanza
na Dar es Salaam.
Tatizo la ukiritimba, ambalo
wapanga taratibu wa Dar es Salaam (na watunga sheria wa Dodoma) huwa hawalioni,
ni hili na linaonekana vizuri kwa mfano halisi wa namna ambavyo mwekezaji wa
Butiama anapaswa kupata msamaha wake wa VAT:
1. Anasafiri
kwenda Mwanza au Dar es Salaam kupata ankara ya vifaa ambavyo anataka kununua.
Nasisitiza kuwa analazimika kusafiri kwa kuwa tunafahamu kuwa, tofauti na nchi
zilizoendelea, kwetu ni muhimu kuona vifaa kabla ya kuvinunua.
2. Anajaza
fomu ya kuomba msamaha wa kodi na kuiwasilisha kwenye ofisi ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania ya Mkoa wa Mara, na kupewa idhini. Ofisi ya mkoa pia ina jukumu
la kukagua mradi na kuhakikisha kuwa unaendelezwa.
3. Anarudi
Dar es Salaam au Mwanza kulipia vifaa bila malipo ya kodi, na kuchukuwa vifaa.
Jambo ambalo nimejifunza ni kuwa hali
ya kutoaminiana kati ya ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania katika ngazi
mbalimbali (makao makuu na mikoani) ndiyo inayosababisha hizi taratibu za ajabu
za kufanya muombaji alazimike kwenda Dar es Salaam au Mwanza mara mbili ili
kukamlisha mzunguko wa manunuzi na kupata msamaha wa kodi.
Nilimuuliza Meneja wa Mkoa wa TRA Mwanza:
“Hivi usingeweza kumpigia simu meneja mwenzako Musoma na kupata uthibitisho
kuwa mradi huu ni halali na unaendelezwa Butiama?”
Alinijubu kuwa, kwanza, sheria na kanuni
haziruhusu. Mwekezaji anatakiwa apate barua ya Mkuu wa Wilaya alipo (kutihibitisha
uwepo wa mradi katika wilaya yake) ambayo inapaswa kuwasilishwa kwenye ofisi za
Mamlaka ya Mapato ya Mkoa, na jalada la mwekezaji kufunguliwa likiwa na orodha
ya vifaa vilivyoruhusiwa msamaha wa kodi. Halafu, kila mwekezaji anapofanya
manunuzi ofisi ya TRA Mkoa itapunguza vile vilivyonunuliwa. Aidha, ofisi hiyo tu
ndiyo yenye mamlaka ya kufanya ukaguzi wa mradi kuhakiki vifaa visitumike
tofauti na ilivyoombwa na mwekezaji.
Meneja huyo wa Mwanza alinitolea
mifano kadhaa ya wawekezaji wasiyo waaminifu ambao walipewa misamaha ya kodi
lakini hawakuwa na miradi yoyote ya uwekezaji waliyoendeleza, na badala yake
wakatumia vifaa vilivyosamehewa kodi kwa matumizi mengine. Alimalizia kwa
kusema: “Unajua watu wamekuwa wadanganyigu sana siku hizi kwa hiyo lazima
kuchukuwa tahadhari.”
Nilimuuliza iwapo taratibu zote
zimekamilishwa, kwanini ofisi yoyote ya TRA katika mkoa wowote wa Tanzania
isiweze kuwasiliana na ofisi ya TRA iliyopo kwenye mkoa wenye mradi ili kutihibitisha uwepo wa mradi ili kumpunguzia mwekezaji
ambaye ni mwaminifu safari ya nenda rudi ili kukamilisha mzunguko. Bado hakuona
kuwa ni tatizo ambalo mamlaka inapaswa kusumbuliwa nalo na kwake yeye tatizo la
msingi lilikuwa kudhibiti wasiyo waaminifu bila kujali athari kwa wale waliyo
waaminifu.
Kwa maoni yangu tatizo la kudhibiti
uhalifu linagubikwa pia na uvivu wa kufikiri mbinu za kudhibiti wahalifu. Kwa
hiyo linapoonekana tatizo, uamuzi unakuwa kudhibiti utendaji badala ya
kurahisisha utendaji. Sasa hivi Tanzania ina Mkongo wa Taifa ambao ungeweza
kutumika vizuri kufanya mawasiliano kati ya ofisi za TRA za mikoa ili taarifa
muhimu za wawekezaji ziweze kupatikana kwenye ofisi yoyote ya TRA nchini.
Si hivyo tu, kompyuta zimejaa
kwenye maofisi ya Tanzania. Zinatumia kwa ajili ya nini? Nimeshuhudia kwenye
maofisi kadhaa hutumika kisikilizia nyimbo za kwenye CD na kuangalia
televisheni. Nina hakika pia hutumika kwa ajili ya Facebook, Twitter, na
shughuli nyingine za mtandao ambazo kamwe haziwezi kumpunguzi bugdha mwekezaji
anayejaribu kuomba msamaha wa kodi ya nyongeza ya thamani.
Nilimwambia yule meneja wa Mwanza
kuwa iwapo polisi wa Tanzania wangekuwa wanafanya kazi kama TRA, basi hali ya
uhalifu ingekuwa mbaya kuliko ambavyo ilivyo sasa. Kwa sababu Mtanzania angetenda
uhalifu Butiama akahamia Kibondo akiwa na uhakika kuwa polisi wa Kigoma
wakimwona watasema kuwa siyo kazi yao kumkamata kwa sababu kosa limefanyika
kwenye Mkoa wa Mara. Kwangu mimi TRA ni
chombo cha kitaifa na huduma yao haiwezi kuishia ndani ya mipaka ya mikoa. Ama sivyo
tuambiwe sasa kuwa Chama cha Mapinduzi kinaanza kutekeleza sera za CHADEMA kwa
kupitia njia za panya.
Nilijaribu kueleza kwa meneja wa
Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwenye ofisi yao ya kanda iliyopo Mwanza adha hii
ya ukiritimba, na hasa kufanyika Dar es Salaam kwa maamuzi ya masuala mbali
mbali. Kwa maoni yake (na baadhi ya sheria zinaelekeza hivyo) kuna maamuzi
mengi ambayo yanaweza kuidhinishwa na maafisa mahususi tu ambao wako Dar es
Salaam.
Nilimkumbusha kuwa kuna maelfu wa
maafisa hapa nchini wanaotekeleza majukumu kwa niaba ya rais kwa hiyo labda
umefika wakati kupitia upya sheria na kuangalia uwezekano wa kukaimishwa kwa
baadhi ya maamuzi yanayokwamisha utendaji.
Kuacha Mamlaka ya Mapato, ipo
mifano mingine mingi kwenye taasisi nyingine ambayo nayo inaathiri utendaji
katika sehemu mbalimbali za nchi. Mfano mmojawapo ni huduma za kampuni za simu.
Ni mara kadhaa nimepiga simu kwenye kitengo cha huduma kwa wateja katika
mojawapo ya kampuni za simu kulalamikia huduma fulani nikaambiwa: “njoo
ofisini.” Hawa waliyoniambia “njoo ofisini” hawakuwa na ofisi Musoma, kwa hiyo “njoo
ofisi” kwangu inamaanisha “njoo/nenda Mwanza”, safari ya kilomita 190.
Tatizo la vitengo vya huduma kwa
wateja kwenye kampuni hizi za simu ni kuwa wanapaswa kuwa na watu wenye uwezo
wa kutoa maelekezo kutatua tatizo kwa njia ya simu, lakini labda kwa kutokuwa na
watu ambao wamepewa mafunzo ya kutosha, wanaposhindwa kumaliza tatizo lako
wanasema: “njoo ofisini.”
Tanzania ina watu wengi kuliko wanaoishi
Dar es Salaam. Hili likizingatiwa, matatizo mengi ya ukiritimba yatapungua.
Taarifa nyingine zinazofanana na hii:
No comments:
Post a Comment