Kwenye Azimio la Arusha, Mwalimu Nyerere alisema haya kuhusu wanawake:
Ingefaa kuwauliza wakulima wetu, hasa wanaume, ni saa ngapi za juma na majuma mangapi kwa mwaka wanafanya kazi. Wengi hawafanyi kazi hata kwa nusu ya saa ambazo mpokea mshahara anafanya. Ukweli ni kuwa kwenye vijiji wanawake wanafanya kazi ngumu sana. Nyakati nyingine wanafanya kazi kwa saa 12 au 14 kwa siku. Wanafanya kazi hata siku za Jumapili na za sikukuu. Wanawake wanaoishi vijijini wanafanya kazi ngumu kuliko mtu mwingine yeyote Tanzania. Lakini wanaume wanaoishi vijijini (na baadhi ya wanawake mijini) wako likizo kwa nusu ya maisha yao. Nguvu ya mamilioni ya wanaume kwenye vijiji na maelfu ya wanawake mijini ambazo kwa sasa zinapotezwa kwenye udaku, dansi na kunywa, ni hazina kubwa ya nchi ambayo inaweza kuchangia maendeleo ya nchi yetu zaidi ya ambavyo tunaweza kupata kutoka mataifa tajiri.Haya ndiyo maneno yaliyomvutia Selma na wenzake kutembelea Butiama.
Selma James ni mwanaharakati wa masuala ya wanawake, ni mwandishi mwenza wa kitabu The Power of Women and the Subversion of the Community, ni mmoja wa waasisi wa International Wages for Housework Campaign, na ni mratibu wa Global Women's Strike.
Selma ni mke wa mwanaharakati mashuhuri kutoka Trinidad, C.L.R. James, ambaye aliandika vitabu kadhaa, ikiwa ni pamoja na The Black Jacobins.
Baada ya ziara yao ya Butiama, mwaka 2007, nilipata mualiko kutoka kwao kuhudhuria hafla jijini London ya uzinduzi wa Azimio la Arusha, tukio lililohusisha pia kuchapishwa kijitabu kidogo kuhusu Azimio la Arusha kikiwa na makala yangu na ya Selma James, pamoja na Azimio la Arusha lenyewe.
Selma James, kushoto, na mimi jijini London, Uingereza, mwaka 2007. |
Na kwa machache niliyoyasikia kutoka kwenye Tamasha la Tano la Kigoda cha Taalum cha Mwalimu Nyerere mapema mwezi huu, yaelekea kuwa kuna wengi ambao wanaamini kuwa Azimio linayo misingi muhimu ambayo yapaswa kuzingatiwa leo hii.
No comments:
Post a Comment