Hii ni tafsiri ya makala ya lugha ya Kiingereza niliyoandika na
ikachapishwa kwenye gazeti la Daily News kwenye safu yangu iliyoitwa Letter from Butiama, makala nilizoandika kati ya mwaka 2005 na 2011. Makala hiyo ilichapishwa tarehe 26 Juni 2005.
*****************************************************
Inasemekana kuwa biashara zote zinazohusu nyama ndani ya mkoa wa Mara
zinadhibitiwa na Wazanaki. Utawakuta kwenye kila ngazi ya biashara hiyo kama
wamiliki, kama wafanyabiashara wa kununua na kuuza ng'ombe, na muhimu zaidi,
kama wamiliki wa bucha. Aidha wamepata mafanikio wakubwa kwenye biashara hiyo
kwenye jiji la Mwanza.
Somo kubwa linalojitokeza katika kuchunguza masuala yanayobainisha kampuni
zenye mafanikio makubwa na zile zenye mafanikio duni ni ukweli kuwa mameneja wa
kampuni zenye mafanikio wamejikita kwenye shughuli za bidhaa na huduma ambazo
wanazielewa vyema. Inaelekea kuwa mmoja wa wafanyabiashara wa ng'ombe
niliyeonana naye anaelewa vyema ukweli huu. Alinipa somo kuhusu hali mbali
mbali za nyama kutoka sehemu tofauti za mwili wa ng'ombe na kuhitimisha kuwa
nyama ya ng'ombe yenye ladha bora kuliko zote ni inayopatikana sehemu ya ndani
ya paja la ng'ombe. Uelewa usiyo wa kawaida kama huu pengine ndiyo chanzo cha
Wazanaki kutawala biashara ya ng'ombe na nyama ndani ya mkoa wa Mara. Napata
picha ya matajiri wa Kizanaki wakimiliki biashara ya nyama ya bara la Afrika
kama ambavyo Wajapani wamedhibiti biashara ya magari.
Pamoja na hii hamasa ya Wazanaki juu ya ng'ombe na nyama, ukweli unabaki
kuwa hisia kali ya mtu mmoja inaweza kuwa mwiko kwa mtu mwingine. Migongano
mikubwa ya kitamaduni inaweza kupatikana kwenye chaguzi ambazo watu toka
tamaduni mbalimbali wanafanya kuhusu chakula wanachokula na kile wasichokula.
Kwa baadhi ya dini kula nyama ni mwiko. Mboga na nafaka ndiyo hutumika kama
vyakula vya msingi kwa jamii hizi.
Suala la chakula lilizua taharuki kwenye ziara mojawapo ya Rais Nyerere
katika miaka ya sabini kwenye nchi mojawapo ya Ulaya. Kama ilivyo desturi
kwenye misafara ya viongozi wa nchi, kiongozi mwenyeji wa nchi ile aliandaa
dhifa ya taifa kwa mgeni wake, na baada ya juma moja Rais Nyerere akaandaa
dhifa kwa mwenyeji wake. Wakati wa dhifa ya pili, mmoja wa Watanzania waliokuwa
kwenye msafara ule alimdanganya Mtanzania mwenzake kuwa miongoni mwa vyakula
vilivyoandaliwa kwenye dhifa ya kwanza ilikuwa ni pamoja na vyura na kuwa yule
mwenzake alikula hao vyura bila kufahamu.
Aliyetoa taarifa hiyo alikusudia yawe mazungumzo kati yao tu, lakini
aliyepewa taarifa ya kula miguu ya vyura alianza kujisikia vibaya hapo hapo na
akaanza kutapika wakati dhifa ikiendelea.
Nilipokuwa mwanafunzi nchini Italia mimi na rafiki yangu George kutoka
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo tulialikwa chakula cha jioni na mwenyeji wetu
Mtaliani. Baada ya kutuagizia chakula alisema kuwa alikuwa ametuchagulia
chakula mahususi kwa ajili yetu ambacho huandaliwa marafiki wa karibu kabisa au
wageni mashuhuri. Ukweli ni kuwa alikuwa ametuagizia miguu ya vyura. Ilikuwa
mara yangu ya kwanza kula miguu ya vyura na nakumbuka ladha ilikuwa kama ya
samaki. Mara tulipowekewa sahani zetu mezani na mhudumu, George alishituka na
alitaka kuhama kabisa ile meza tuliyokaa. Mimi na mwenyeji wetu tulipoanza
kushambulia ile miguu nakumbuka George alipata shida kubwa kubaki kwenye meza
moja na sisi na kuangalia kitendo ambacho ni dhahiri kilimfadhaisha sana.
Mwenyeji wetu, ambaye aliwahi kutembelea nchi kadhaa za Afrika, alishangaa
sana George. Alimuuliza anawezaje kuona kinyaa kula miguu ya vyura wakati yeye
ameshuhudia Waafrika wakila wale wadudu ambao hutokeza baada ya mvua kunyesha.
Alikuwa anazungumzia senene. George naye alishindwa kumuelewa Giuseppe. Mtu
anawezaje kulinganisha kula senene na miguu ya vyura? Alisema Giuseppe alikuwa
analinganisha vitu ambavyo havipaswi kulinganishwa kabisa.
Kuacha mimi, hamna kati yao ambaye alikuwa ameshakula miguu ya vyura pamoja
na senene. Kimya kimya niliwashangaa hao wawili ambao walikuwa wanabishana
ubishi ambao hawakuwa na mamlaka hata kidogo ya kuuendeleza. Jambo ambalo
sikuweza kulibainisha wakati ule ni chakula kipi, kati ya chura na senene,
kilikuwa na ladha nzuri zaidi.
Ukweli ni kuwa yawezekana kufikia usemi kuwa ladha ya chakula ni uamuzi
ambao uko kichwani mwa mtu mmoja mmoja. Nimewahi kujitwika ujasiri usiyo na
mfano na nikala chakula ambacho machoni kilikuwa kinatisha kuangalia lakini
nikajikuta nimeweka mdomoni chakula chenye ladha nzuri kuliko maelezo. Tofauti
na mwananchi mwenzangu ambaye alikuwa kwenye ziara ya Rais Nyerere, mimi
nilifahamu chakula nilichokula siku ile kwenye ule mgahawa nchini Italia, kwa
hiyo jambo la kushangaza ambalo naweza kulizungumzia ni ladha nzuri tu ya miguu
ya vyura.
No comments:
Post a Comment