Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, November 24, 2012

Jimmy ChangChuu, msanii toka Bagamoyo atembelea Butiama

Jimmy ChangChuu, ni msanii anayeishi na kufanya kazi Bagamoyo. Baadhi ya kazi anazofanya ni pamoja na kuchonga vinyago, kufinyanga, kuandaa michoro ya grafiti (michoro ya ukutani) na ni mwanamitindo.

Aidha hushiriki kwenye matangazo ya televisheni na anafahamisha kuwa ameshiriki kwenye kipindi televisheni cha cha Dume Challenge. Hivi karibuni alitembelea Butiama na yafuatayo ni maoni yake kuhusu Butiama.
***************************************************

"Naishi hizi sehemu mbili, Dar es Salaam na Bagamoyo, kwa sababu Bagamoyo ni sehemu yangu ambayo napata msukumo, ni sehemu iliyotulia. Mizunguko ya Dar es Salaam kidogo inakuwa inanishinda lakini ninapohitajika Dar es Salaam nakuwepo na familia.

Hii ni mara yangu ya kwanza kufika Butiama. Mara ya kwanza nilipokuja tu ile mandhari ilinifanya nijisikie kama niko na amani, nilipata amani kwenye moyo. Mazingira yametulia, yaani hakuna kitu ambacho kinaweza kikajiingiza wakati unafikiria kufanya kitu fulani au wakati uanataka kufanya kitu. Kwa hiyo ni sehemu ambayo imetulia ambayo inaweza kukupa msukumo.

Ni ngumu sana kupata msukumo kwenye sehemu ambapo kuna vitu vinapita ambavyo vinakuvuruga lakini hapa unaona hali asili ya mazingira, unaona ndege, yaani vitu ambavyo vinakufanya unaona kuwa kuna Muumba ambaye ametengeneza hivi vitu. Ni vitu ambavyo vinavutia kweli.

Kitu ambacho kinaweza kufanya niwaambie watu waje Butiama ni mazingira na hali ya utulivu halafu nikiangalia chimbuko la kabila la Wazanaki kuna vitu ambavyo nilikuwa nikiviangalia ambavyo vina nguvu kubwa ambavyo ukiviangalia kwa juu juu huwezi kuviona, lakini kuna vitu ambavyo vipo ambavyo vimemfanya Mwalimu Nyerere akawa ana nguvu kwenye maamuzi yake, vitu ambavyo vinaendana na tamaduni yetu ya Kitanzania na ambavyo Mwalimu aliviweka kwenye siasa yake na kwenye mila na hakutoka nje ya mila yake kusikiliza mila za kigeni. Alisimama yeye pale aliposimama kutoka kwenye chimbuko la tamaduni yake.

Kwa hiyo unakuta sasa hata katika utawala wake hakutoka nje sana kwa sababu hata nikiangalia nilivyokwenda makumbusho [Makumbusho ya Mwalimu J.K. Nyerere] kule kuna vitu ambavyo nimesoma na Nyerere mwenyewe alikuwa anakwambia elimu ya wakoloni ilikuwa inawaandaa wao kuwatumikia wakoloni siyo kuwaandaa kuweza kujiendeleza wao wenyewe.

Kitu kizuri kama watu wanataka kuwa kwenye siasa na kuwa viongozi wazuri wanapaswa kujifunza kutoka kwa Nyerere na aliyoyafanya. Tangu akiwa shuleni alianza kuwa kiongozi na alichaguliwa na watu. Watu waliona Mwalimu alikuwa na kitu fulani wakamchagua. Siyo kwamba yeye alipendekeza 'mimi nataka kuwa kwenye nafasi hii.' Watu walimuona kuwa ana kitu ambacho anaweza kuchangia kwa wengine na pia alikuwa na uwezo wa kushawishi wengine."

Monday, November 12, 2012

Sijiuzulu ng'o! Hata mkija na winchi ya bandari

Jenerali David Petraeus wa Marekani amejiuzulu hivi karibuni kwa sababu ya mahusiano na mwanadada ambaye jina lake haliko kwenye cheti cha ndoa cha Jenerali huyo. Kwa Kiswahili anaitwa nyumba ndogo; kwa Kizanaki anajulikana kama kitungo.

Haya yangetokea Tanzania hamna mtu yoyote angeachia ngazi, na suala hili linaibua mitazamo tofauti kati ya utumishi wa umma hapa Tanzania na utumishi wa umma katika nchi nyingine.

Ukweli ni kuwa hata katika mijadala niliyoisikia kwenye vyombo vya habari vya nje kuna wale ambao wanaona kuwa Jenerali Petraeus hakustahili kung'atuka kwa sababu haya ni mambo ambayo yanatokea kwa watumishi wa ngazi za juu kwenye nchi mbalimbali duniani. Mtakumbuka kuwa Rais mstaafu Bill Clinton naye alikutwa na masuala yanayofanana na haya, na aliwekwa kiti moto kwa muda mrefu lakini hakujitoa kwenye uongozi. Tuhuma kubwa dhidi yake ilikuwa kusema uongo baada ya kula kiapo.

Kwa mantiki hiyo, inaelekea wadhifa wa Jenerali Petraeus kama Mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani, Central Intelligence Agency, ni nyeti zaidi katika nafasi ya uongozi wa nchini Marekani kuliko hata ule wa Rais wa Marekani, na inasemekana kuwa mkuu wa kazi wa Jenerali Petraeus ndiye aliyemshauri kuachia ngazi na yeye akafuata ushauri huo.

Nimetafakari suala hili iwapo aliyehusishwa na mahusiano haya angekuwa Mkuu wa Usalama wa nchi tofauti na Marekani na iwapo mkuu huyo angekuwa ni Mzanaki.

Soma mahojiano haya ya kubuni:

Mwandishi: Ndugu Madaraka, ninayo taarifa kuwa unahusishwa na tuhuma kuwa una uhusiano wa nje ya ndoa na [jina limehifadhiwa na gazeti] na...

Madaraka: Ndugu? Nani ndugu yako? Bwana mdogo, mimi ni mheshimiwa, tena mheshimiwa sana na ukitaka nijibu maswali yako nataka unipe heshima yangu. Na inaandikwa "m-h-e-" kabla ya jina...

Mwandishi: Samahani, mheshimiwa, nilikuwa nauliza....

Mhe. Madaraka: Swali nimelisikia. Bwana mdogo, nyie wasomi wa siku hizi mnafahamu sana mila na tamaduni za Ulaya na Marekani, lakini cha ajabu mnashindwa kudumisha na kuheshimu mila na tamaduni zenu wenyewe. Na ndiyo maana siku zote mtaendelea kutawaliwa kimawazo. Na ukishatawaliwa kimawazo utapangiwa mpaka maneno ya kuongea na mkeo nyumbani.

Sasa ngoja nikupe somo la bure kuhusu mila na tamaduni za kabila langu. Huyo mama ambaye wewe unashindwa kutaja jina lake, jina lake halisi ni [jina tumelihifadhi] na wala siyo siri kuwa ni mke wangu...

Mwandishi: Atakuwaje mke wako wakati tunafahamu mke wako ni......

Mhe. Madaraka: Mura! Enye ndakuburra ni mkane, bhono ni wazo? [Kijana! Mimi nakwambia ni mke wangu, sasa ni wako?] Bwana mdogo, ukitaka nikujibu usiniingilie ninapokujibu. Ukitaka kunipangia idadi ya kina mama zangu kwa sababu ulisomea Marekani, nashauri umuulize haya maswali Petraeus. Hapa siyo Marekani. Wao wana mila zao na mimi najaribu kukueleza mila zangu, kama utanisikiliza. Hutaki, kafanye kazi Marekani kwa sababu mimi hapa hatutaelewana.

Huyo nyie mnayemwita nyumba ndogo kijijini kwangu ana heshima yake, na wala hafichwi. Tunamuita kitungo, kama umeshawahi kusikia. Na kama ulifikiri utanitoa upepo kwa kunipa hofu kuwa umekalia siri ambayo utaifichua na kuniaibisha utakuwa unapoteza muda. Kwa taarifa yako ndugu zangu wote wanamfahamu, pamoja na mke wangu. Na hii ni pamoja na mamlaka iliyoniteua.

Haya, una lingine?

Mwandishi: Sawa mheshimiwa. Sasa pamoja na kwamba hizo ndiyo mila za Kizanaki, lakini wewe ni mtumishi wa Serikali na unashika wadhifa unaohusiana na usalama na maslahi ya Taifa. Utakuwa unafahamu kuwa nchi hii haiendeshwi kwa taratibu za kabila la Kizanaki. Inafuata kanuni, taratibu, na sheria. Huoni kama kwa kuwa na mahusiano haya yasiyo rasmi unaweza kuwa unahatarisha kuvujisha siri za nchi na kuwa unastahili kujiuzulu.

Mhe. Madaraka: Hivi wewe una akili timamu? Huyo aliyeniteuwa hana akili? Mimi mwenyewe sina akili? Kwamba nitaleweshwa na mahusiano yangu binafsi halafu nianze kuzianika siri za Serikali? Mbona hamkuwa na wasiwasi kuwa nitatoa siri kwa mke wangu, iweje leo nizitoe kwa huyu bi mdogo? Kama tatizo ni mahusiano na kina mama basi hizi kazi wawe wanafanya mapadri, watu ambao hawafungi ndoa. Lakini ni jambo ambalo pia mtalipinga, mtasema hatuwezi kuchanganya dini na Serikali maana hamksoi cha kusema nyie.

Unafahamu ile winchi ya badnari inayobeba kontena la futi 40? Nakwambia hata mkiileta ile kujaribu kuniondoa hapa, sitang'oka

Uchaguzi nafasi 10 za wajumbe wa NEC - CCM Tanzania Bara, Wassira aongoza

Matokeo ya chaguzi za nafasi 10 za wajumbe wa NEC Tanzania Bara wa Chama cha Mapinduzi zinazoendela Dodoma yametoka. Matokeo haya hapa:

1.  Stephen Wassira                  - 2,135
2.  January Makamba               - 2,093
3.  Mwigulu Nchemba             - 1,967
4.  Martine Shigela                  - 1,824
5.  William Lukuvi                  - 1,805
6.  Bernard Membe                 - 1,455
7.  Mathayo David Mathayo   - 1,414
8.  Jackson Msome                  - 1,207
9.  Wilson Mukama                 - 1,174
10. Fenela Mukangara            -     984

Saturday, November 10, 2012

Konyagi watoa ala za muziki kwa Msondo Ngoma

Kampuni inayotengeneza kinywaji Konyagi imetoa zawadi ya ala za muziki kwa bendi kongwe ya muziki wa dansi nchini, Msondo Ngoma.
Msondo Ngoma jukwaani.
Akikabidhi hizo ala, Mkurugenzi Mkuu wa Tanzania Distilleries Limited ambao ndiyo watangenezaji wa Konyagi, alisema vifaa hivyo vimetolewa kwa ajili ya kuenzi utamaduni wa Mtanzania na kuiwezesha Msondo Ngoma kuwa imara katika kutoa burudani kwa Watanzania.

Alisema, "Msondo ni bendi kongwe tangu kuanzishwa kwake mwaka 1964. Imesimama imara katika kutoa burudani ya uhakika kwa Watanzania na kutumia nyimbo zake katika kuelimisha, na kufunza jamii ya Watanzania walio wengi."

Alisema kwa kuwapatia vyombo hivyo, Msondo Ngoma itakuwa moto wa kuotea mbali katika kutoa burudani ya uhakika, hali itakofanya bendi nyingine kuwa wasindikizaji katika tasnia ya muziki wa dansi nchini.

Mkurugenzi wa bendi hiyo, Maalim Gurumo, alisema kwa sasa wana deni kubwa kwa Watanzania na kampuni ya Konyagi katika kutoa burudani ya uhakika baada ya kupatiwa vifaa hivyo.
Mkurugenzi wa Tanzania Distilleries Limited David Mgwasa, wa pili kutoka kulia, akikabidhi ala kwa wanamuziki wa Msondo Ngoma.
"Tunaamini baada ya leo kupata vifaa hivi tutatoa burudani ya uhakika sanjari na kukijenga vyema kikosi chetu kwa lengo la kukiimarisha," alisema Gurumo.

Kiongozi wa bendi, Saidi Mabela, alitoa shukurani kwa kampuni ya Konyagi kwa kuwapatia vyombo na aliahidi kuendelea kutoa burudani safi kwa Watanzania na Afrka kwa ujumla.
Habari kamili ziko hapa.

Tuesday, November 6, 2012

Mlima Kilimanjaro unapendeza zaidi tokea Tanzania au Kenya?

Kuna mdau hapa anauliza swali: Mlima unaonekana vizuri tokea Tanzania au Kenya? Huyu mdau anahisi kuna hujuma inafanywa na jirani zetu kuvutia wageni wengi zaidi waende Kenya na ndiyo maana hoja hii inaibuliwa.

Hili swali halipaswi hata kuulizwa. Mlima Kilimanjaro unavyoonekana kutokea Kenya ni tofauti kidogo na unavyoonekana upande wa Tanzania. Kama kuna mtu kapendezewa na taswira ya mlima tokea Kenya huwezi kumlazimisha afurahie taswira ya mlima huo kutoka upande wa Tanzania.

Lakini huu utaratibu wa kulalamikia jirani zetu wa Kenya kunufaika na Mlima Kilimanjaro wakati sisi wenyewe tumekaa na kuongea tu pia hauna manufaa yoyote kwa maendeleo yetu.

Ninavyoamini mimi, mgeni yoyote aliyetoka nje ambaye amekuja kukwea mlima huu maarufu hajali kama uko Kenya, Tanzania, au kwenye sayari ya Zuhura. Mgeni anavutiwa na mlima wenyewe na siyo mipaka ya nchi.

Mimi nimeshakwea Mlima Kilimanjaro mara kadhaa na ukweli ni kuwa ni Watanzania wachache sana wanakwenda huko kulinganisha na wageni wa nje. Kwa kweli kule mlimani Mtanzania ndiyo mgeni na wageni ndiyo wenyeji kwa sababu idadi yao ni kubwa sana. Hivi karibuni nimekutana na Wakenya kibao kwenye njia ya Marangu wakielekea kileleni.

Mimi ningefurahi sana kuona hawa wenye uchungu na mlima huu kusemwa uko Kenya basi wawe wanajitokeza mara moja moja nao kukwea huu mlima. Hiyo itawawezesha kuzungumzia mlima wao kwa kujiamini badala ya kuuliza maswali tu na kulalamika.
Mlima Kilimanjaro unavyoonekana kutoka upande wa Tanzania.
Kitu ambacho watajifunza ni kuwa mandhari nzuri kuliko zote za mlima huu ziko huko huko mlimani. Lakini haya ni maoni yangu tu.

Sunday, November 4, 2012

Lugha yetu Kiswahili

Jana kwenye redio nimesikia marudio ya majadiliano kutoka kwenye vikao vya Bunge la Muungano vinavyoendelea sasa hivi. Alisikika mbunge mmoja, akiwa anatetea hoja kuwa lugha ya Kiswahili itumike kwenye uendeshaji wa shughuli za mahakama, akisema yafuatayo (siyo nukuu halisi kwa maana ya neno kwa neno lakini ni sahihi kwa maana ya nukuu yenyewe):

"...mienendo yote ya shughuli za mahakama iendeshwe kwa lugha ya Kiswahili tu, na kusiwe na option ya Kiswahili au Kiingereza, iwe ni Kiswahili tu."

Anayesisitiza matumizi ya Kiswahili pekee kwenye shughuli za mahakama za Tanzania anajenga hoja yake kwa kutumia neno la Kiingereza.

Ni kazi kweli kweli.

Kwenye kamusi neno option lina maana kadhaa, ikiwa ni pamoja na: uchaguzi, na hiari.

Thursday, November 1, 2012

Mada ya yangu ya leo: aliyeikashifu Kurani aadhibiwe

Kwa hali ya kawaida, mtoto aliyedhalilisha kitabu kitukufu cha dini ya Kiislamu angeweza kuadhibiwa kwa kuchapwa bakora na mzazi wake au kupewa adhabu nyingine nzito ambayo watoto wote wanaokosea hupewa.

Lakini tukio liliotokea siyo la kawaida, kama ambavyo tumeshuhudia madhara yaliyofuata na vurugu zilizotokana na kitendo kile. Makanisa yalivamiwa na mali nyingi kuporwa na kuharibiwa. Uporaji wa mali haufanani hata kidogo na Uislamu kwa hiyo ni dhahiri kuwa katika kundi la watuhumiwa wa matukio haya ambalo linasemekana kuwa ni la waumini wa dini ya Kiislamu walishiriki pia watu ambao hawakusukumwa na hasira ya kudhalilishwa kwa Kurani na dini ya Kiislamu bali ni watu waliyoona fursa ya kuharibu na kupora mali.

Tanzania inayo sheria inayosimamia watuhumiwa ambao wako chini ya umri wa miaka 18. Ni dhahiri hakuna ubishi kuwa huyo mtoto alifanya kosa hilo. Jambo moja ambalo linaweza kuepusha manung'uniko ya dhati ya waumini wa dini ya Kiislamu kulalamikia kile kitendo ni kufikisha suala la yule mtoto mahakamani bila uchelewesho. Kufanya hivyo kutaondoa kabisa kisingizio cha wale ambao wanatafuta fursa ya kufanya fujo kwa kisingizio cha kutetea hadhi na heshima ya dini ya Kiislamu.

Nina hakika yule mtoto tayari anajutia kitendo chake, lakini suala la kutafuta suluhu baina ya waumini wa dini mbalimbali, na suala la kulinda amani nchini linahitaji hatua za kisheria zichukuliwe haraka dhidi yake.