Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, July 4, 2011

"Wagumu" wa Mlima Kilimanjaro

Mgeni yoyote anayepanda mlima Kilimanjaro anahitaji huduma ya waongoza msafara, wapishi, na wabeba mizigo. Hili kundi la mwisho wanajulikana kama “wagumu” kwa sababu ya ugumu wa kazi wanayofanya ya kumbebea mgeni vitu muhimu vinavyohitajika: mahema, chakula, maji, na vifaa vingine vya lazima.
Mgumu (kushoto) akiwa na mzigo wake baada ya kumpita Muongoza Msafara (mwenye kofia nyekundu) anayeongoza mgeni aliye nyuma yake.
Asubuhi wao huamka mapema kuandaa kifungua kinywa kwa wageni wakishirikiana na mpishi. Baada ya kifungua kinywa Muongoza Msafara (ambaye naye huanza kazi kama mbeba mizigo kwa miaka kadhaa) huongoza msafara wa wageni kuelekea kwenye kambi inayofuata. Msafara wa kukwea Mlima Kilimanjaro unaweza kuchukuwa kati ya siku 5 hadi 12, kutegemea na njia inayotumika.

Baada ya msafara kuondoka kambini, wagumu huvunja kambi na kufungasha mahema na mizigo mingine yote na kuanza safari ya kuelekea kambi inayofuata. Kwa kuwa ni wazoefu wa kubebea mzigo, huupita msafara wa wageni na Muongoza Msafara na msafara unapofika kwenye kambi wageni wanakuta wagumu wameshasimika upya mahema yote, na mpishi anakuwa tayari ameshapika chakula cha wageni. Wanafanya hivi kila siku ya msafara.
 
Wagumu wanayo sifa ya kutumia pesa inayotokana na kazi yao ya kusindikiza wageni kupanda Mlima Kilimanjaro kwa fujo. Dada mmoja mhudumu wa baa moja ya mjini Moshi aliniambia baadhi yao wanapolipwa pesa yao huhamia baa mpaka pesa iishe. Pesa inapoishia kwenye pombe, wengine hujisababishia majeraha ya mwili na kudanganywa wake zao kuwa wameporwa malipo yao na vibaka.
Wagumu wa Kilimanjaro wakifurahia siku ya mwisho ya msafara katika Kambi ya Mweka.
 Hii ndiyo baadhi ya mikasa ya wagumu wa Kilimanjaro.
Wagumu wa Kilimanjaro wakifurahia siku ya mwisho ya msafara katika Kambi ya Mweka.

No comments: