Kwenye
makala hii ambayo imegawanywa kwenye awamu tatu, Notburga Maskini anaandika
kuhusu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba na kuzikwa leo, tarehe
15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunnu nchini Afrika ya Kusini.
Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Pili)
Na Notburga Maskini*
Migongano ya Kitabaka
Matabaka ya mabwana na watwana yalijitokeza kutokana na
unyonyaji, udhalilishaji, na ubaguzi uliofanywa na makundi dhalimu ambayo
yalijitokeza na kuonekana katika mifumo ya kijamii kwa maana ya Ukomunisti na
Ubepari ambapo mabwana au wenye nguvu, waliwadhalilisha wanyonge; ilitengeneza
tabaka la watu wachache matajiri wa kupindukia ambao wameshikilia na kuwekeza
asilimia 80 ya utajiri wa dunia katika mtaa wa tano (the 5th Avenue New York).
Tabaka la pili ni la umma wa wakulima na wafanyakazi maskini
na wanyonge katika nchi zetu na duniani ambao bidii na jasho lao haviwawezeshi
kujikwamua kutokana na mirija ya dhuluma iliyopangwa na tabaka hili la watu wachache lakini lenye nguvu kubwa
kiuchumi na kiutawala. Tabaka la tatu ni tabaka la maskini wa kutupwa miongoni
mwao wakiwemo wazee, wastaafu, vijana wasio na ardhi wala ajira, wanawake na
watoto.
Hali hii ya
kuhuzunisha na tishio kwa amani ya nchi zetu na dunia ilionekana mapema machoni
na kwenye mioyo ya viongozi hawa mashujaa Nelson Rolihlahla Mandela na Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere. Waliichukia na kufanya bidii kubwa kuchukua hatua
sawia kupambana ili kuona mfumo wa haki usawa na heshima kwa binadamu
unasimikwa dhidi ya mifumo ya unyonyaji, ubaguzi na udhalilishaji.
Kazi iliyobaki ya kugawa rasilimali hizi za dunia ziweze
kuwafikia watu wengi na kuondoa umaskini duniani ndio njia pekee ya kumuenzi
Mzee Mandela bila unafiki. Tunahitaji mashujaa kama Mzee Nelson Mandela na
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambao wataweka ushawishi na kupambana hasa
wakati huu zinapoonekana dalili kuwa jambo hili linawezekana. Kifo cha shujaa
huyu tumeshuhudia viapo na dhamira
zikiwekwa kanisani na hadharani kuashiria kuwa tayari hata kufa ili kutetea ustawi
wa binadamu na amani duniani.
Picha: Maafisa wa jeshi la Afrika ya Kusini wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa Marehemu Nelson Mandela kwenye mazishi ya taifa yaliyofanyika tarehe 15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunu, jimbo la Eastern Cape.
Kusaliti na kuvunja tabaka
Mzee Nelson Mandela na Mwalimu Julius Nyerere ni miongoni
mwa watu waliojaaliwa na Mwenyezi Mungu kuumwa na kuchukizwa na hali mbaya ya
binadamu wote. Waliona ubaya na adha inayotokana na binadamu kumdhalilisha
binadamu mwingine na hatari yake kwa amani ya dunia hivyo hawakuivumilia hata
kwa sekunde chache. Walipinga hali hii pamoja na uwezo waliokuwa nao kutokana
elimu na nafasi zao za kuzaliwa wakiwa watoto wa machifu, ambapo wangaliweza
kuungana na wadhalilishaji na kuwa wanufaikaji wa mifumo dhalimu iliyojaa
uroho, uchoyo, dharau, na tamaa.
Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere walizungumza kwa sauti kubwa
na hivyo kuweka ushawishi mkubwa ndani ya jamii na nchi zao na kuanzisha
vuguvugu la mapambano yaliyokusudia kuleta heshima kwa binadamu. Ni dhahiri
kuwa walitumia maisha yao hapa duniani kujitoa mhanga kwa ujasiri wa kupindukia
hata kuuwa matabaka yao (class suicide) kupigania usawa haki
na heshima kwa binadamu. Ndiyo maana kuondoka kwao duniani
Mzee Nelson Mandela aliyetanguliwa na rafiki yake mkubwa Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere muongo mmoja na nusu uliopita kunaleta mshtuko na wasiwasi
mkubwa kwa amani ya dunia, usawa, ubinadamu, demokrasia, na utawala bora. Hii inatokana na ukweli kwamba binadamu wa
aina hii hutokea kwa nadra sana.
Itaendelea na: Heshima katika historia ya nchi na dunia
*Notburga A Maskini ni Kaimu Rais wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
No comments:
Post a Comment