Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Friday, December 27, 2013

Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Tatu na ya Mwisho)

Kwenye makala hii ambayo imegawanywa kwenye awamu tatu, Notburga Maskini anaandika kuhusu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba na alizikwa  tarehe 15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunu nchini Afrika ya Kusini.

Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Tatu na ya Mwisho)
Na Notburga Maskini*

Heshima katika historia ya nchi na dunia
Kilio kinachoendelea hivi sasa na heshima kubwa waliyopewa mashujaa wetu waliolala ni changamoto kubwa kwa kizazi kinachofuata. Walijitoa thamani kupigania heshima ya binadamu. Kinachoendelea sasa ni heshima kubwa kwao hata wakiwa wamelala na kama alivyowahi kusema Mzee Mandela katika nukuu zake: “Ukijiheshimu hata simba atakuogopa na kukuheshimu”. Taarifa zilizotangazwa na gazeti moja nchini kuwa Alqaida na al Shaabab hawatafanya mashambulizi katika kipindi hiki cha maombolezo ni kielelezo cha ukweli wa nukuu hiyo ya shujaa wetu, Baba wa Taifa la Afrika ya Kusini.
 
Waombolezaji wakitoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Nelson Mandela tarehe 11 Desemba 2013, wakati mwili wake ulipohamishiwa kwenye majengo ya Union jijini Johannesburg. (Picha ya GCIS).
Hii ni heshima japo yeye hafungamani na itikadi wala vitendo vya makundi hayo bali anafungamana na upendo, msamaha na kutokulipa visasi. Naamini iwapo dunia itajifunza haraka kutoka kwa shujaa huyu pengine vitendo hivi vinaweza kuisha na wahusika kuendelea kuwa watu wa amani.

Je tuko tayari kujifunza?
Sisi tuliobaki nyuma pamoja na kuomboleza tuna maswali ya kujiuliza na kutoa majibu sasa, iwapo:
1)      Tuko tayari kurejesha na kuendeleza mfumo wa kidhalimu unaodhalilisha na kunyonya binadamu wengine hasa wafanyakazi na wakulima;
2)      kuwafanyisha kazi ngumu wafanyakazi na wakulima bila kuwalipa ujira stahiki au kuratibu bei za mazao yao kwa kisingizio cha utandawazi huku kukiwa na lengo la kushirikiana na wanyonyaji kujilimbikizia mali binafsi kupitia jasho lao;
3)      kuendeleza wizi wa mali za umma, matumizi mabaya ya madaraka dhidi ya wanyonge na kupuuza ustawi na maendeleo yao.

Ama:
1)      Tunadhamiria kujifunza kwa mashujaa wetu Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere, kuenzi maisha yao, na kuendeleza mema yao, kwa kuwa wafanyakazi bora, watumishi waadilifu, wabunifu, na waaminifu wa wananchi wetu;
2)      Haki na nafasi za raia kumiliki rasilimali za mataifa yetu kwa usawa zinalindwa na kuwezeshwa hata kama maisha na maslahi binafsi yatatishiwa;
3)      Tutawalinda na kutetea haki za kiraia, na kuishi bila kuwatisha, kuwauwa katika kulipiza visasi au mapigano ya wenyewe kwa wenyewe,  kwa lengo la kustawisha jamii, kuondoa umaskini, na kudumisha heshima ya binadamu iliyoasisiwa na mashujaa hawa.

Kupokea mauti kwa ujasiri na fedheha za kiuongozi
Inaleta maana kuchagua kulinda na kutanguliza maslahi ya umma na Taifa, ili historia isije tuhukumu kwa kutotimiza wajibu tunaopaswa kufanya kwa jamii na nchi zetu wakati wa uhai wetu. Hali hii itatuwezesha kupokea mauti kwa ujasiri na imani kubwa. Kitendo cha fedheha kilichomkuta kiongozi mkuu wa sasa wa Afrika Kusini kuzomewa mbele ya uso wa dunia  na wananchi wake waliomchagua kidemokrasia si cha kupuuzwa hata kidogo. 

Ni muhimu kujifunza na kujitahidi kubadilika ili kuepusha shari na matokeo mengine mabaya ambayo huletwa na tabia za viongozi kuonekana wanajijali binafsi. Kuwaumbua viongozi hasa wale wasiojitambua husababisha hasira na kulipiza kisasi kwa wanaothubutu kufanya hivyo. Hali hii husababisha mitafaruku; huweza kugawa taifa na kuondoa amani. Naamini yote mazuri yaliyopiganiwa wakati wa uhai wa Mzee Mandela na Mwalimu Nyerere yamewekwa katika msingi imara ya kuwezesha kuyaendeleza. Kazi kubwa ni kwa tuliobaki nyuma kuamua na kuanzia walipoachia.

Kwaheri Mzee Nelson Rolihlalha Mandela. Mungu akupumzishe kwa amani na raha ya milele akujalie kama ulivyonuwia katika matendo na maisha yako.


*Notburga A Maskini ni Kaimu Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).

No comments: