Kwenye
makala hii ambayo imegawanywa kwenye awamu tatu, Notburga Maskini anaandika
kuhusu Mzee Nelson Mandela, aliyefariki tarehe 5 Desemba na kuzikwa leo, tarehe
15 Desemba 2013 kwenye kijiji cha Qunnu nchini Afrika ya Kusini.
Mandela! Mandela! Mandela! (Sehemu ya Kwanza)
Na Notburga Maskini*
Hiki kimekuwa ni kilio cha dunia nzima kumwomboleza
shujaa mpigania uhuru, amani, haki, utu na utawala bora duniani, mwana wa bara
la Afrika mwenye asili ya Afrika ya Kusini Nelson Rolihlahla Mandela
mwanaharakati, kiongozi wa chama cha ANC na Rais Mstaafu wa Afrika ya Kusini;
aliyeaga dunia tarehe 5 Desemba 2013. Mimi binafsi na kwa niaba ya wafanyakazi wa Tanzania
naungana na Watanzania wenzangu, wafanyakazi wa Afrika ya Kusini na Dunia
kuomboleza msiba huu mkubwa ambao ni pigo kubwa kwa tabaka la wafanyakazi
duniani na vilevile ni pigo dhidi ya utawala bora, haki, amani na utu.
Picha: Wanachama wa
Umkhonto We Sizwe, lililokuwa jeshi la chama cha African National Congress
lilioendesha mapambano ya kivita dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika ya
Kusini, wakiwasili kwenye makazi ya jijini Johannesburg ya marehemu Nelson
Mandela tarehe 8 Desemba 2013. (Picha ya GCIS).
Niandikapo
makala hii nakumbuka mwaka 2003 nilipokuwa jijini Johannesburg kuhudhuria
mkutano wa dunia kuhusu uwekezaji wa mitaji Afrika, Kusini mwa Sahara kwenye
ukumbi mmojawapo katika jengo maarufu la Sandton. Wakati wa kutoka
ukumbini tulikutana nae ana kwa ana mlangoni akiwa na watu wengine, nafikiri
kiongozi huyu alitokea kwenye ukumbi mwingine wa mkutano katika jengo
hilo. Binafsi nilifurahi sana kumuona Mzee Mandela aliyekuwa katika hali
ya kawaida kabisa. Hata hivyo mimi na hata wenzangu hatukuweza kufanya
chochote angalau kuweza kumsalimia kutokana na kutofahamu taratibu na mipaka ya
kiitifaki. Alikuwa
ni kivutio kikubwa kwetu sote tuliokuwepo siku hiyo.
Afrika Kusini na Tanzania
Ndugu zetu wa Afrika ya Kusini kama ilivyokuwa kwetu
Watanzania tarehe 14 Oktoba 1999 alipotuaga Mwasisi wa Taifa hili,
mwanamapinduzi aliyeheshimika duniani, na kipenzi cha Watanzania, Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, nao wanapitia hali ngumu iliyojaa
majonzi, vilio, na mashaka lakini pia wakimshukuru Mungu kwa zawadi kubwa aliyoupatia
umma wa Afrika Kusini, Bara la Afrika na Dunia.
Katika kitabu chake cha dondoo Nelson Mandela By Himself, 2013 Mzee Mandela anatufariji kwa maneno yake mwenyewe
kuwa:
“kifo hakikwepeki. Wakati binadamu ameshatimiza yale aliyofikiri kuwa ni
wajibu wake kwa watu wake na nchi yake, anaweza kupumzika kwa amani. Naamini kuwa nimefanya bidii kutimiza wajibu huo na
ndio maana nitalala katika umilele”
Ni dhahiri kuwa Mzee Mandela ameondoka akiwa
anaridhishwa na bidii kubwa aliyoweka katika kazi kubwa aliyoifanya ya kuondoa
ubaguzi wa rangi na udhalilishwaji wa mtu mweusi katika nchi yake ya Afrika ya
Kusini. Pengine Watanzania na waombolezaji tuliobaki yafaa
kutafakari sasa kuhusu wajibu wetu kwa watu wetu na nchi zetu na iwapo tutaweza
kuwa jasiri na kusema maneno hayo siku yetu itakapofika.
Imani na mapenzi ya Umma dhidi ya chuki za maadui
Mzee Nelson Mandela kama alivyokuwa Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wameteka mioyo ya walimwengu na wananchi wao
kwa imani yao katika utu badala ya vitu, na kusimamia kwa vitendo bila ya
kutetereka. Wanamapinduzi hawa wa Afrika waliweka mbele maslahi ya
taifa na utu wa watu wao. Walijitoa
muhanga maisha yao yote kwa ajili ya nchi zao na watu wao jambo ambalo ni nadra
kwa viongozi wengi tuliowashuhudia katika karne ya ishirini.
Wakati Mwalimu Julius Nyerere akiongoza mapambano ya
ukombozi wa Bara la Afrika na dhidi ya udhalimu dhidi ya ubinadamu ikiwemo
Afrika Kusini yenyewe, alitengeneza maadui waliotokana na kundi la
wakandamizaji waliojijengea uhalali na kuamini kuwa wao ni bora kuliko binadamu
wengine. Hata hivyo maadui hao kama tunavyoshuhudia leo
wamejirudi na kujifunza thamani ya utu na utaifa katika kutumikia umma.
Isingewezekana wakati ule wa mapambano ya ukombozi
kuwa Afrika ya Kusini ingebadilika na kuwa kama ilivyo
sasa. Kinachodhihirika hapa ni nguvu ya upendo, msamaha, na uzalendo kwa
nchi na watu wake vinavyoweza kuleta mabadiliko chanya. Hili ni somo kubwa kwa Afrika na Dunia.
Itaendelea
na: Migongano ya Kitabaka
*Notburga A Maskini ni Kaimu Rais wa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA).
No comments:
Post a Comment