Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, June 20, 2011

Mlima Meru, wa pili kwa urefu Tanzania, wa 72 ulimwenguni

Mlima Meru ni Mlima wa pili kwa urefu Tanzania baada ya Mlima Kilimajaro. Una urefu wa mita 4,565 juu ya usawa wa bahari na unaorodheshwa kushika nafasi ya 72 kwa milima mirefu kuliko yote duniani. Mlima Meru uko mkoa wa Arusha, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha.
Mlima Meru ukionekana kutoka Arusha.
Watu wengi wanaoparamia milima kama mimi huanza kupanda milima rahisi kwanza kabla ya kwenda kwenye ile yenye kutoa changamoto kubwa zaidi. Wengi hupanda Mlima Meru kabla ya Kilimanjaro, ingawa mimi nimeanza kupanda Mlima Kilimanjaro nikikusudia baadaye kuukabili Mlima Meru. Waliopanda milima yote miwili wanasema kuwa, pamoja na kuwa Meru siyo mrefu kuliko Kilimanjaro (Kilimanjaro una urefu wa mita 5,895 juu ya usawa wa bahari), untoa changamoto kali kwa sababu kupanda kwake ni mpando wa siku 2 mfululizo wakati Mlima Kilimanjaro unahusisha njia zinazovuka mabonde kadhaa na hiyo ina maana kuwa wanaoelekea kileleni hujikuta wakipanda na kushuka na hata wakati mwingine kupita sehemu zenye tambarare.

Tafiti zinathibitisha kuwa miaka bilioni kadhaa iliyopita Mlima Meru ulilipuka kutokana na msukumo wa gesi za volkano na kusababisha sehemu yake ya pembeni kumeguka na kutapakaa kwenye eneo la umbali unaofikia upande wa magharibi ya Mlima Kilimanjaro. Hizo tafiti zimethibitisha kuwepo tabaka ya udongo wa Mlima Meru juu ya sehemu hiyo ya Mlima Kilimanjaro.

Picha hii ya chini ambayo imepigwa na vyombo vinavyoruka juu vya shirika la Marekani NASA inaonyesha vizuri sehemu ya Mlima Meru iliyomeguka kutokana na mlipuko wa volkano. Tofauti ya rangi iliyopo kwenye picha inaakisi tofauti ya umbali kutoka usawa wa bahari wa eneo hilo la Mlima Meru.
Hii picha ya Mlima Meru inatumika kwa hisani ya NASA/JPL-Caltech. [Photo: Courtesy NASA/JPL-Caltech]

Saturday, June 18, 2011

Tarehe za kupanda Mlima Kilimanjaro mwaka huu ni Septemba 20 hadi 27

Kila mwaka tangu mwaka 2008 nimekuwa napanda Mlima Kilimanjaro kuchangisha pesa za hisani. Mwaka 2008 nilipanda Mlima huo na raia wa Vietnam, Le Hu Dyuong. Mwaka 2009 nilipanda Kilimanjaro na Notburga Maskini, ambaye tulisoma pamoja Shinyanga Commercial Institute (Shycom) miaka iliyopita. Yeye alikuwa pamoja na mtangazaji maarufu wa Clouds FM, Gerald Hando.
Le akiwa kwenye bwawa lenye mamba, baada ya msafara wa kupanda Mlima Kilmanjaro mwaka 2008.
Mwaka jana nilipanda mlima na Jaffar Amin, mtoto wa kiongozi wa zamani wa Uganda, Idi Amin.
Jaffar Amin, akiwa amekaa mbele ya mahema yetu kwenye kambi ya Karanga iliyopo mita 3,963 juu ya usawa wa bahari wakati wa msafar wa mwaka jana wa kupanda Mlima Kilimanjaro.
Mwaka huu natarajia kupanda Mlima Kilimanjaro kuanzia tarehe 20 hadi 27 Septemba. Natarajia kupanda mlima pamoja na wafuatao. Ambao wamesema watajiunga na mimi mwaka huu ni pamoja na mwanablogu mwashuhuri Muhidini Issa Michuzi, mdau wa Utalii Aysha Boma, raia wa Uswisi Andrea Wobmann, mtengeneza filamu wa Marekani Jim Becket (amewahi kuongoza picha ya Mark Dacascos) pamoja na mpigapicha wake, na raia wa Uganda Barbara Allimadi. Kuna wengine ambao bado hawajathibitisha.

Thursday, June 16, 2011

Tabia ya Tumbili

Kumradhi endapo nitakuwa nimemuudhi yoyote kwa kutumia hii picha hapa chini ya huyu jamaa akiwa kwenye mkao wa kula, pamoja na kwamba nilishwahi kuitumia hapa.
Miaka kadhaa iliyopita nilihudhuria mafunzo ya muda mfupi katika chuo kilichopo Tengeru karibu na Arusha, sehemu ambayo ilikuwa inatembelewa na tumbili mara kwa mara.

Jioni moja baada ya kutoka darasani nilishuhudia baadhi ya wanafunzi wenzangu, wakiwa wamevutiwa na hawa wanyama, na walijaribu kuwasogelea pole pole lakini kila walipowakaribia wale tumbili walisogea mbali.

Cha ajabu ni kuwa mmoja wa wakufunzi wetu alipopita kwenye njia ya mguu karibu kabisa na sehemu ambapo tumbili walikuwa wamekaa, wale tumbili hawakuondoka na walibaki pale pale. Raia wa Zambia ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi alitabiri mapema kuwa wale tumbili wasingemkimbia yule mkufunzi. Yule mkufunzi alikuwa mzungu. Na ndivyo ilivyotokea na akapita pale karibu yao kabisa bila kumkimbia.

Mimi ninao uzoefu wa kuishi karibu na tumbili. Huyo aliye kwenye picha ni mmoja kati wengi wa makundi makubwa ya tumbili yaliyopo hapa Butiama. Niliwaambia wenzangu kuwa inaelekea kuwa tumbili wanatambua sura za watu na hukumbuka na kuzigawanya sura hizo katika makundi mawili – wale ambao wanaweza kuwa hawatishii usalama wao na wale ambao wanatishia usalama wao. Nikiwa Butiama, wakati nafanya mazoezi ya kutembea kujiandaa kupanda Mlima Kilimanjaro hukutana na tumbili mara kwa mara na huwa hawanikimbii ingawa nimeshuhudia wanawakimbia baadhi ya watu wengine, hasa watoto.
Hawa tumbili wa Butiama wanayo sababu nzuri ya kukaa mbali na binadamu. Tumbili wana tabia ya kuiba mazao ya kilimo na wakazi wengi wa Butiama wanalazimika kuwafukuza tumbili wanaojaribu kuiba hayo mazao. Sijawahi kufukuza tumbili, kuacha mara chache wakati mlango uliachwa wazi na nikamkurupusha tumbili aliyekuwa ananyemelea maandazi yangu asubuhi.yemelea ,aribu kuw

Wednesday, June 15, 2011

Leo katika historia ya Kombe la Dunia 2006: Poland, Trinidad & Tobago, na Paraguay zaaga mashindano


Poland, Trinidad & Tobago, na Paraguay ziliaga mashindano ya Kombe la Dunia.

Poland ilipoteza michezo yake yote miwili ya Kundi A, kwanza kwa Ecudaor (0-2), halafu kwa Ujerumani (0-1). Ingawa ilishinda mechi yake dhidi ya Costa Rica (2-1), haikutosha kuivusha na kuingia raundi ya pili. Ni ushindi wa Ecuador wa 3-0 dhidi ya Costa Rica uliyoivusha Ecuador, na kuiondoa Poland kwenye mashindano.

Trinidad & Tobago, katika ilipangwa na England, Sweden, na Paraguay katika Kundi B. Yenyewe ilitoka sare mechi moja tu na Sweden (0-0), na kupoteza mechi mbili. Tarehe ya leo, mwaka 2006, Trinidad & Tobago ililazwa 2-0 na England na kuyaaga mashindano, ikiwa ya mwisho kweye kundi lake.

Paraguay, ilishika nafasi ya pili toka mwisho kwenye kundi lake baada ya kufungwa 1-0 na Sweden, tarehe 15 Machi 2006, na timu ikapanda ndege kurudi Ascuncion.

Kwenye Kundi A Ujerumani na Ecuador ziliingia randi ya pili, wakati ni England na Sweden zilizoingia raundi ya pili toka Kundi B.

Monday, June 13, 2011

Omukama wa Missenyi

Mapema mwaka huu, nikiwa kwenye ziara ya Mkoani Kagera, nilipata fursa ya kutembelea Bunazi, katika Wilaya ya Missenyi na kuzuru makazi ya mtemi wa eneo hilo. Mtemi wa sasa wa Missenyi, tangu mwaka 2001, ni Omukama Paulo Lwamujongo II, aliyemrithi baba yake, Omukama Serapion N.L. Kyamukuma II (1932 – 2001) aliyetawala kati ya mwaka 1955 hadi 2011 alipofariki.

Orodha ya watawala waliyomtangulia Omukama Paulo Lwamujongo II
Na.
Jina
Maelezo
Kipindi cha Utawala (kama ni wazi, miaka haijulikani)
1
Wakara
Bunyoro

2
Kagoro I
Alitoka Bunyoro na akahamia Kyango (Buganda)

3
Nyamutura
Alifia Kyango (Buganda)

4
Lwekika I
Alifia Mayanja (Buganda)

5
Kagoro II
Alliingia Missenyi na kuwa Mwami wa kwanza wa Missenyi

6
Nyamutura II


7
Kagoro III
Hakuwa na mtoto wa kiume; kaka yake mdogo alirithi

8
Kyamukuma I
Kaka yake Kagoro III

9
Lwekika II
Mukama wa kwanza wa Missenyi
1870 – 1903
10
Suleimani Kakoko Wakara II

1913 – 1919
11
Paulo Nyamutura Lwamujongo I

1919 – 1955
12
Serapion N.L. Kyamukuma II

8 Feb 1955 – 22 Machi 2001

Kwa mujibu wa historia iliyotolewa, chimbuko lao ni Unyankole, Uganda. Maelezo zaidi:
Watawala wa Bunyoro walikuwa Wahima. Jamaa zao walikuwa wa ukoo wa Balebeki. Rumonge, mtawala mdogo wa Kihima huko Ankole alipoasi Bunyoro alifukuzwa. Nafasi yake ilichukuliwa na mtu wa ukoo wa Balabeki. Sehemu ya kusini ya Ankole mpakani mwa Mto Kagera ilikuwa Kibumbilo ambako mtawala mdogo wa Kihima, Kakoko, alitawala. Naye pia alikuwa wa ukoo wa Balebeki

Mwisho Kibumbilo ilikuwa sehemu ya Himaya ya Baganda mpaka ilipowekwa mipaka ya Wajerumani na Waingereza. Kwa hiyo historia ya utawala huu kwa Missenyi kabla ya matokeo haya haimo katika kitabu cha historia ya Buhaya.

Mwana ukoo wa Omukama wa Missenyi (kulia) akitoa maelezo ya historia mbele ya sehemu ambapo Omukama Serapion Kyamukuma alipokelea wageni wake.
Kabla ya kutawazwa mwaka 2011 Omukama Lwamujongo II alikuwa Dar es Salaam, ambako alikuwa anafanya kazi.