Miaka kadhaa iliyopita nilihudhuria mafunzo ya muda mfupi katika chuo kilichopo Tengeru karibu na Arusha, sehemu ambayo ilikuwa inatembelewa na tumbili mara kwa mara.
Jioni moja baada ya kutoka darasani nilishuhudia baadhi ya wanafunzi wenzangu, wakiwa wamevutiwa na hawa wanyama, na walijaribu kuwasogelea pole pole lakini kila walipowakaribia wale tumbili walisogea mbali.
Cha ajabu ni kuwa mmoja wa wakufunzi wetu alipopita kwenye njia ya mguu karibu kabisa na sehemu ambapo tumbili walikuwa wamekaa, wale tumbili hawakuondoka na walibaki pale pale. Raia wa Zambia ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi alitabiri mapema kuwa wale tumbili wasingemkimbia yule mkufunzi. Yule mkufunzi alikuwa mzungu. Na ndivyo ilivyotokea na akapita pale karibu yao kabisa bila kumkimbia.
Mimi ninao uzoefu wa kuishi karibu na tumbili. Huyo aliye kwenye picha ni mmoja kati wengi wa makundi makubwa ya tumbili yaliyopo hapa Butiama. Niliwaambia wenzangu kuwa inaelekea kuwa tumbili wanatambua sura za watu na hukumbuka na kuzigawanya sura hizo katika makundi mawili – wale ambao wanaweza kuwa hawatishii usalama wao na wale ambao wanatishia usalama wao. Nikiwa Butiama, wakati nafanya mazoezi ya kutembea kujiandaa kupanda Mlima Kilimanjaro hukutana na tumbili mara kwa mara na huwa hawanikimbii ingawa nimeshuhudia wanawakimbia baadhi ya watu wengine, hasa watoto.
Hawa tumbili wa Butiama wanayo sababu nzuri ya kukaa mbali na binadamu. Tumbili wana tabia ya kuiba mazao ya kilimo na wakazi wengi wa Butiama wanalazimika kuwafukuza tumbili wanaojaribu kuiba hayo mazao. Sijawahi kufukuza tumbili, kuacha mara chache wakati mlango uliachwa wazi na nikamkurupusha tumbili aliyekuwa ananyemelea maandazi yangu asubuhi.
No comments:
Post a Comment