Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Tuesday, July 5, 2011

Machinga wa Dar es Salaam


Kabla ya mwaka 1999 niliishi na kufanya kazi jijini Dar es Salaam, halafu baada ya hapo nikahamia kijijini Butiama.

Kuna mabadiliko makubwa yanaonekana jijini Dar es Salaam kwa mtu ambaye anakuwa nje ya jiji hilo kwa muda. Siyo rahisi kwa wakazi wa Dar kuona hayo mabadiliko kulinganisha na anayetokea nje ya Dar. Nakiri huwa “nashangaa” kwa mabadiliko makubwa ninayoyaona Dar kila ninapotembelea huko. Mfano, hivi karibuni nilienda sehemu ambapo ilikuwepo Sno Cream, jirani na Shule ya Forodhani, nikakuta jengo lile ilipokuwa Sno Cream limebomolewa na kuna jengo jipya linajengwa. Niliambiwa Sno Cream walishahama pale siku nyingi.

Kundi la watu wenye uzoefu wa kuwasoma watu “wanaoshangaa” ni machinga wanaorandaranda jijni Dar es Salaam wakiuza bidhaa mbalimbali. Miaka kadhaa iliyopita nilitembelea Dar es Salaam na nilikuwa nimekaa na rafiki zangu wa siku nyingi sehemu ya vinywaji na chakula inayoitwa George’s Grill. Machinga aliingia pale akiuza vitu na alikuja moja kwa moja kwangu akijaribu kuniuzia bidhaa. Nilimuuliza: ‘”Mimi fala? Katika watu wote waliokaa hapa umeona mimi ndiyo nafaa kuwa mteja wako?”

Yule machinga alijibu: “Hapana, siyo hivyo mzee”, akionekana kujizuwia kucheka.

Baada ya kuondoka Dar na kuisha kijijini kwa muda mrefu ni dhahiri kuwa nina mueleko ambao ni tofauti na wa wakazi wa Dar es Salaam, hasa  wale niliokaa nao meza moja. Yule machinga aliiona hiyo tofauti (labda kwa mavazi yangu) na akanilenga mimi moja kwa moja. Hainisumbuwi, lakini ndiyo hali halisi.

Mwanzoni mwa mwaka huu nilionana na mwanafunzi mwenzangu wa siku nyingi tuliyesoma naye Chuo cha Elimu ya Biashara (Shycom) miaka iliyopita. Anasema enzi hizo, miaka 33 iliyopita, sisi wanafunzi wa Shycom kutoka Dar tulionekana wajanja sana kuliko wanafunzi wengine ambao walitokea maeneo mengine ya Tanzania. Leo nimegeuka mawindo ya machinga.

No comments: