Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, July 14, 2011

'Muhunda' aonekana Butiama


Hivi karibuni, siku chache baada ya mazishi ya mwanafamilia, alionekana nyani mkubwa akikatisha kwenye baadhi ya maeneo ya kijiji cha Butiama.

Nilipata taarifa za kuonekana kwa nyani huyo baada ya kuulizwa: “Umemuona Muhunda?”

“Muhunda?”

“Ndiyo, ametutembelea.”

Wakati napokea taarifa hiyo, mbwa walikuwa wakibweka ovyo, mithili ya mbwa mwitu.

Kuna Muhunda wawili tu ninaowafahamu. Mmoja ni baba yangu mdogo, Joseph Muhunda. Na mwingine ni mzimu wa kabila la Wazanaki, kiumbe asiye wa kawaida anayeaminika kuishi ndani ya msitu wa nasaba wa Muhunda uliyopo jirani na Mwitongo, sehemu yalipokuwa makazi ya babu yangu. Ni marufuku kuingia ndani ya msitu huo ila kwa watu maalumu tu, kwa mfano rika la wazee, au wanyikura ambao ndiyo wasimamizi wa msitu. Aidha kukata miti ya huo msitu pia ni marufuku ingawa kuokota matawi makavu yalioanguka inaruhusiwa.

Mwalimu mstaafu, Jack Nyamwaga, anakumbuka kuwa wakati wa utoto wake kuna nyani mkubwa alifika kwenye makazi ya babu yangu, Mtemi Nyerere Burito. Yule nyani alisogelea na kuanza kula mihogo iliyokuwa imeanikwa nje, na watoto walipojaribu kumfukuza Mtemi Nyerere aliwazuwia na kusema wamwache yule nyani aendelee kula ile mihogo.

Inaaminika kuwa mzimu huu hujibadilisha katika maumbile mbalimbali ikiwa ni pamoja na chui, nyoka, mbuzi, au nyani. Ni nadra kuona nyani Butiama na ingawa nimewahi kuwaona kwenye milima ya jirani na Butiama huwa hawafiki eneo la Butiama. Hii ni mara ya pili katika kipindi cha miaka 11 kwa nyani kuonekana hapa Butiama.

Wanaoamini kuwepo kwa mzimu huu wanaamini kuwa umefika kufuatia msiba tuliyopata hivi karibuni. Mashuhuda wanasema kuwa huyu nyani aliyeonekana hivi karibuni alitokea upande wa kaskazini, akavuka eneo lenye makazi, akipuuzia watoto waliokuwa wanamrushia mawe, na alifika kwenye kaburi la ndugu tuliyemzika hivi karibuni na akabaki pale kwa dakika chache halafu akaelekea Mwitongo.
Wakati wa msiba wa ndugu yangu, Mazembe Joseph Nyerere.
Siyo mbwa tu walikuwa wamekosa amani, inasemekana kuwa hata tumbili ‘waliingia mitini’ na hawakuonekana kabisa, ingawa kwa kawaida eneo la Mwitongo lina makundi mengi ya tumbili.
Tumbili 'waliingia mitini.'
Katika miaka iliyopita kila nyani mkubwa alipojitokeza eneo la Butiama wanyikura walikutana na kutuma wawakilishi kwa mpiga ramli mashuhuri aliye eneo la Mto Kirumi kupata ufafanuzi juu ya ujumbe au tafsiri ya kuonekana ‘Muhunda’. Iwapo ‘Muhunda’ alikuwa amekasirishwa na tukio fulani ndani ya jamii, basi ujumbe uliwasilishwa kwa jamii na tambiko lilifanyika.

2 comments:

Anonymous said...

Hii habari ya kusisimua. Sasa mpiga ramli anasemaje kuhusu ujio huo wa Muhunda? Je ulifanikiwa kupata picha yake tumuone?

Madaraka said...

Sikufanikiwa kupiga picha, na bado sijapata taarifa kama wazee walienda kwa mpiga ramli.