Shirikisho la Ngumi la Kimataifa (IBF) limemteua Rais wa Shirikisho hilo katika bara
la Afrika, Onesmo Alfred Ngowi kusimamia pambano la ubingwa wa mabara
linalotambuliwa na IBF.
Mpambano huo utafanyika katika jiji
la Accra nchini Ghana tarehe 26 Mei kati ya bingwa wa mabara wa IBF Emmanuel
Tagoe wa Ghana na mpinzani wake Antonio De Vitis wa Italy katika uzito wa Junior
Lightweight.
Katika mpambano huo wa kutetea mkanda
wa ubingwa wa IBF ambao unashikiliwa na Tagoe Ngowi atasaidiwa
na waamuzi wengine kama ifuatavyo: Refarii: Roger Barnor (Ghana). Majaji:
Francisco de Ruvo, (Italy), Andre Pasquier (France) na Shadrack Acquaye (Ghana).
Mpambano huo uliopewa jina la “Ni Sasa au Hakuna Tena”, bondia Joseph Agbeko wa Ghana atagombea mkanda wa dunia
wa Organizesheni ya Ngumi ya Kimataifa (IBO) akichuana na bondia Michael Domingo
wa Ufilipino katika uzito wa Bantam.
Bondia Joseph Agbeko anayeishi
katika mji wa Bronx katika jiji la New York nchini Marekani atakumbukwa kwenye mpambano wake mkali wa kugombea ubingwa wa
IBF katika uzito wa Bantam kati yake na bondia Abner Mares wa Mexico tarehe
3 mwezi Agosti 2011 katika jiji la Las Vegas, Nevada, nchini Marekani ambako
ilibidi warudiane mara ya pili baada ya kutokea malalamiko ya kuonewa kwa Agbeko.
Hata hivyo bondia Abner Mares
alimshinda tena Joseph Agbeko waliporudiana tarehe 18 Novemba 2011 katika jiji
la California, nchini Marekani.
Naye bondia Joshua Okine wa Ghana
ambaye alikuwa bingwa wa mabara wa IBF katika uzito wa Middle kabla ya kupoteza
ubingwa wake kwa kupandisha uzito atapambana na bondia Theofiilus Teteh pia wa
Ghana kugombea mkanda wa WBO Africa.
Bondia Sammuel Amaoko, anayejulikana pia kama Bruno wa
Ghana, atapambana na bondia Sidney Siqueira wa
Brazil kugombea mkanda wa WBO Africa katika uzito wa Heavyweight.
Mapambano haya yaliyoandaliwa na
Golden Mike Boxing Promotions ya Ghana yatafanyika katika uwanja wa kimataifa wa
El-Wak, jijini Accra nchini Ghana chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Ngumi
za Kulipwa ya Ghana (Ghana Boxing Authority, GBA).
Usimamizi wa Ngowi katika mpambano
huu unakuja kipindi kifupi baada ya Francis Cheka wa Tanzania kuunyakua mkanda
wa IBF Continental Africa Title katika uzito wa Super Middle
tarehe 28 April mwaka huu.
|
No comments:
Post a Comment