************************************************
Ninavyoangalia jamii ya Tanzania ilivyo sasa hivi, pamoja na
mambo yote mema tuliyonayo, tumejaliwa watu wenye kuheshimiana, wenye
kupendana, kwa kiwango kikubwa. Tunaanza
kuchukiana chukiana, lakini kwa sababu ya mipangilio mibaya na kujitawala
vibaya. Lakini kimsingi, watu wetu ni watu wema. Watawala wao ndiyo waovu.
Matokeo yake ni kuwa tumejenga jamii ya watu katika kiwango
ambacho kinatisha cha watu wa aina zifuatazo:-
-
Watu wasioaminika
-
Matapeli
-
Wababaishaji
-
Na wapuuzi
Sisi, pamoja na watawala wetu.
Watu warushaji katika mahusiano ya kibiashara kiasi kwamba
hatuaminiki katika nchi jirani. Mara mafuta yamechakachuliwa; mara ukiuza pamba
wameweka mawe. Ali mradi, tumekuwa sisi ni waNigeria wa eneo hili la Afrika.
Watu tunaoonea wanyonge. Kuwaibia masikini. Kuwapora wahanga
wa ajali, na kuwaua albino kwa imani za kijinga. Washirikina tunaoamini ujinga
wakati uthibitisho wa teknolojia tunao mikononi. Kwamba tunaweza ku-Google, search engine ya Google, kutafuta mchawi mahiri yuko wapi.
Ujuha wa kiasi hicho. Na wengine sasa wanakwenda bungeni.
Watu na jamii fasta fasta. Wenye tamaa ya kupata utajiri wa haraka bila kufanya
kazi. Tumekubali wito wa:
-
Kuwa mjanja!
-
Chizika!
-
Pandisha mzuka!
-
Full kujirusha!
Ambayo yote yametujaza upuuzi wa kibambucha.
Jamii isiyopenda kujifunza. Tumevifanya vitabu ni kama wakwe zetu, tunaogopa kuvifunua wakati tunaona jinsi majirani zetu, kwa mfano, Kenya, vijana wanavyohangaika kujisomea. Ukienda Nairobi, nenda Saritz Centre, uende bookshop ile angalia jinsi wanavyosoma halafu mnaogopa Wakenya watachukuwa nafasi zetu; Wakenya watachukuwa ardhi yetu.
Bora waje Wakenya kuliko kuwa na wajinga wakaharibu nchi hii.
Watu wakutoa majibu mepesi mepesi kwa maswali mazito. Kwa sababu hatupendi kusumbua akili zetu. Wapiga kura wanaouza kura zao kwa bakuli la kunde, na kisha kulalamika wasipopata uongozi wa kuwafanyia kazi. Watu wasiojua misingi ya haki. Wanaochoma moto mwizi wa kuku, lakini mwizi wanamchagua kumpeleka bungeni.
Kumi, kwa ufupi, watu na jamii iliyopotea.
Jamii hii haiwezi kuandika katiba. Mpaka i-address masuala haya. Mimi naamini kabisa tukienda kuandika katiba sasa hivi, nakubaliana na Issa [Prof. Issa Shivji], kwamba kama hiyo Tume ya Rais itakuwa na watu wanawakilisha makundi mbalimbali, itaanza kuzungumza na hali yenyewe tuliyo nayo ndiyo hii, yaani fanya unavyotaka, hutapata chochote cha maana kwa sababu humu ndani kutakuwa na wezi, wazandiki, matapeli, wababaishaji, wala rushwa. Kila mtu anajaribu kuweka nafasi yake mbele. Na maslahi yake mbele.
Sasa tufanye nini? Yuko Mzee Ibrahim Kaduma hapa. Natumai kuwa kitabu chake kilichozinduliwa juzi kitakuwa hapa. Ili kupambana na haya niliyoyasema, ambayo ni magonjwa makubwa, ni majanga makubwa, na ndiyo yanatawala, hebu turudi kwenye misingi.
Moja: Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja.
Nitatumikia nchi yangu na watu wake wote.
Nitajitolea nafsi yangu kuondoa umasikini, ujinga, maradhi, na dhuluma.
Ongeza na rushwa.
Nne: Rushwa ni adui wa haki sitapokea wala kutoa rushwa.
Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cheo cha mtu mwingine kwa
faida yangu. Hebu niambie ni watu gani ndani ya Serikali wanaweza kusimama hadharani wakasema maneno haya?
(Hadhira: hawapo!)
Sasa tuwafanye wayaseme haya. Katika uandikaji...katika mchakato mzima wa kujadili katiba mpya, tufike mahala tuwalazimishe watu waliomo katika utawala, wasimame mbele yetu waseme hivi: Cheo ni dhamana. Sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa manufaa yangu. Waseme! Halafu tuwapime.
Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kutumia elimu yangu kwa faida ya Nchi.
Nyie wasomi hapa chuoni mnasema hiyo? Au? Nasikia wanafunzi wengi sana mnasoma accountancy. Accountancy ni somo zuri lakini sasa sijui mnataka kwenda kufanya kazi wapi?
Nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.
Nitasema kweli daima. Fitna kwangu mwiko.
Nitakuwa raia mwema wa Tanzania, Afrika, na Dunia nzima.
Tuyatafakari hayo. Tuwe na muafaka wa kitaifa. Tuwe na maridhiano, tuwe na makubaliano. Tuwe na national charter, kutokana na hilo sasa ndiyo twende na michakato mingine aliyosema Shivji [Prof. Issa Shivji] ya kujenga misingi ya maelewano nchini na kuandika katiba mpya itakayotuongoza kwa miaka hamsini au mia ijayo. Nawashukuruni sana.
No comments:
Post a Comment