Kuna mambo mawili muhimu yanajitokeza baada ya kuuwawa kwa mwandishi wa habari wa Channel Ten wa Iringa, Daudi Mwangosi, tarehe 2 Septemba 2012. Kwanza, Jeshi la Polisi, ambalo mmoja wa askari wake ameshafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo, linahitaji kutoa mafunzo maalum ya namna polisi waliyopo kwenye eneo la maandamano wanavyopaswa kusimamia suala la amani katika maandamano.
Siyo kila tukio la mkusanyiko wa watu linahatarisha mali au maisha ya raia, kwa hiyo ni dhahiri pia kuwa siyo lazima kila mara kutumia nguvu zisizokuwa za lazima dhidi ya raia. Polisi wanafunzi wanapaswa kupewa elimu inayojenga taswira kuwa anaepinga serikali iliyoko madarakani siyo lazima pia awe ni adui wa Taifa au anaetishia usalama wa Taifa.
Picha inayojitokeza baada ya baadhi ya matukio ambapo polisi wameua raia ni kama vile kazi kuu ya polisi ni kuhakikisha kuwa upinzani halali wa kisiasa unaminywa kiasi cha kutosha na kuondoa kabisa uwezekano wa serikali iliyopo madarakani kuondolewa madarakani kwa njia za kidemokrasia.
Polisi wapate mafunzo kuwaelimisha kuwa kazi yao siyo kulinda maslahi ya kisiasa ya serikali iliyopo madarakani, na wafunzwe kukubali uwezekano kuwa chama chochote kilichopo upande wa upinzani kinaweza hatimaye kushinda uchaguzi na kuongoza serikali.
Jambo la pili na ambalo ni muhimu sana ni kuwa sasa waandishi wa habari wapate mafunzo ya namna ya kukusanya habari kwenye maeneo yenye usalama mdogo ili kupunguza tishio kwa usalama na maisha yao. Polisi anafanya kazi kwa amri, na kuna mazingira mengi ya kisheria yanayomruhusu polisi kutumia silaha kwa jinsi ambavyo anaona ni sawa kutokana na mazingira yanayomkabili. Polisi anayefukuzwa na kundi la waandamanaji ambao anaamini wanakusudia kumuua hatasita kutumia silaha yake dhidi ya kundi hilo. Huu ni mfano tu; haya sidhani kama ni mazingira yaliyotokea kwenye tukio lilisobabisha kifo cha Daudi Mwangosi.
Jambo la msingi ni kuwa, hata pale ambapo tunajua tunayo haki, si busara hata kidogo kubishana na mtu ambaye ameshika silaha na anaamini kuwa anatekeleza amri halali aliyopewa na mkubwa wake. Na hili haliwezi kubadilika mpaka itolewe elimu ambayo itambadilisha polisi Mtanzania ili atumie mbinu tofauti kukabiliana na waandamanaji.
Sunday, September 16, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment