Hii taarifa ni tasfiri ya makala ya lugha ya Kiingereza niliyoiandika mwaka 2005 kwenye gazeti la Sunday News.
Amini au usiamini kuhusu uchawi lakini ukweli unabaki kuwa uchawi ni suala lisiloepukika kwenye jamii za Kiafrika. Butiama nayo haiwezi kukwepa ukweli huu.
Mwezi Mei mtuhumiwa wa uchawi ambaye nitamuita Pepe alitimuliwa Butiama na wanakijiji waliyomtuhumu kufuga na kufanya biashara ya mazuu. Inaaminikia mazuu ni binadamu ambao huzikwa wakiaminika wamekufa lakni hufufuliwa kwa njia za kichawi na hufanyishwa kazi kwenye mashamba na pia kutoa huduma kadhaa za weledi.
Mfanyakazi wa hospitali ambaye mfanyakazi mwenzake aliyekuwa daktari alifariki hivi karibuni amesema kuwa yule mfanyakazi mwenzake, ambaye wote tunajua kuwa ni marehemu, sasa hivi anaendesha hospitali kwenye ulimwengu wa siri wa mazuu. Hospitali hiyo ina upungufu wa wafanyakazi na "mchawi" aliyetimuliwa ndiyo anasadikiwa kupeleka watu wa kuziba nafasi zilizo wazi.
Pepe alijijengea desturi ya kufanya shughuli za kawaida katika mida ambayo siyo ya kawaida. Wanakijiji wenzake wakijiandaa kulala yeye ndiyo kwanza aliwaelekeza mafundi kuendelea na ujenzi wa nyumba yake katika mida ambayo pia inajulikana ndiyo mida wale ambapo wale wanaominika kuwa wasaidizi mahiri wa wachawi, yaani fisi na bundi, wanakuwa na pirika pirika nyingi na mizunguko ya huku na kule.
Jambo moja la kushangaza ni kuwa fundi mmojawapo ambaye alishiriki kwa kipindi kifupi nyakati za usiku kujenga nyumba ya Pepe alikiri kuwa hajaona muda mzuri wa kujenga nyumba kuliko usiku kwa sababu usiku hakuna wale wapiga porojo wa mchana ambao hupunguza kasi ya kazi. Huyo fundi aliacha ujenzi wa nyumba ya Pepe baada ya kupata onyo kali kutoka kwa wazee wa kimila, wanyikura.
Baada ya hapo wanyikura walituma wito kwa Pepe kumtaka aeleze sababu ya kujenga nyumba usiku. Alielekezwa kuendeleza ujenzi wake mchana kama wengine na akafuata kwa muda lakini baadaye akarudia tena ujenzi wa usiku. Alipata wito mwingine kuonana na wanyikura lakini safari hii badala ya kuitika wito, siyo tu hakuhudhuria kikao kilichoitishwa kwa ajili yake, lakini akatuma onyo kwa wazee kuwa wakiendelea kumfuata fuata atawafungulia mashitaka mahakamani na wangeweza kujikuta jela. Kama hii ni kweli basi alikuwa amefanya kosa kubwa sana. Wazee wa jadi ni taasisi muhimu sana ya kimila. Ni dhahiri kuwatishia huku kuliibua tafrani kubwa zaidi.
Wanyikura ni kama serikali. Pepe alikuwa anachochea moto. Kwa kulipiza kisasi wanyikura wakaanza kuweka vikwazo. Hakuna aliyeruhusiwa kuongea naye. Yoyote ambaye angekiuka hiyo amri angeweza kutozwa faini, aghalabu ng'ombe mzima, kutegemea na mazingira ya ukiukwaji uliyofanyika. Athari za ukiukwaji wa aina hii kwenye mazingira ya mjini yanaweza kuwa ni madogo sana, lakini kwenye kijiji, ambapo ushrikiano na wengine ni muhimu sana katika kila nyanja, vikwazo vinaweza kuwa na athari kubwa sana. Nilipata taarifa kuwa mmiliki mmoja wa duka alipewa onyo kali na wazee wa kimila baada ya kumuuzia Pepe vocha za simu.
"Angekubali tu amri ya wazee, akakubali kulipa faini, na kuendela kujenga mchana, angekuwa bado yupo," alisema fundi. Kusingezuka kisingizio cha kumfukuza. Aliwadharau wazee akawapa mwanya wale waliyokuwa wanamshuku kwa uchawi kufanya njama za kumtimua kijijini.
Ukichukulia kuwa mtu yoyote anayeaminiwa kuwa ni mchawi anachukuliwa kuwa hawezi kuwa na woga wa aina yoyote na kuwa ni mkatili mmmoja ambaye hurandaranda usiku akitafuta binadamu wa kuwadhuru akitumia fisi kama usafiri wake, mimi nilifikia uamuzi kuwa Pepe hakufanana asilani na taswira hii. Jioni moja, nilikuwa naendesha gari nikitokea Musoma na nilisimamishwa na kundi la watu waliyokuwa wamesimama pembeni ya gari nyingine ndogo. Miongoni mwao alikuwa Pepe. Alinijulisha kuwa walikuwa wakielekea Musoma lakini baada ya kukuta mawe makubwa yameegeshwa katikati ya barabara niliyopita mimi muda ule ule kabla ya kuwafikia, waligeuza gari haraka wakihofu kushambuliwa na majambazi wenye silaha.
Niliwaambia sikuona mawe yoyote barabarani na kuongeza kuwa yawezekana kuwa baada ya wao kugeuza gari na "majambazi" nao wakatawanyika wakihofia nia yao mbaya imegundulika.
Kutokana na maelezo yangu baadhi ya abiria wa ile gari walifarijika na wakaanza jitihada za kumshawishi dereva apite palepale na kuendelea na safari kwenda Musoma. Mtu pekee aliyeamua kuwa kuendelea na safari ya Musoma ni hatari alikuwa mtuhumiwa wa uchawi, Pepe. Aliniomba lifti tukarudi naye Butiama.
Saturday, September 8, 2012
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment