Katika makala hii yenye sehemu mbili, Dk. Amani Millanga anasisitiza umuhimu kwa Taifa wa kuendeleza mfumo wa reli.
*****************************************
KUTOTUMIA RELI KUNAUA UCHUMI (sehemu ya kwanza kati ya sehemu mbili)
Dk. Amani Millanga |
Kwa miaka zaidi ya kumi Tanzania imezungukwa na taswira iliyokomaa
ya kudhoofika kwa njia kuu za usafirishaji za reli, meli na ndege kana kwamba
hazina umuhimu wowote katika ujenzi na ukuwaji wa uchumi wa taifa letu na
ustawi watu wake. Vituo vyote vya treni vimeota magugu. Reli imegeuka kichaka.
Sababu kubwa za kudhoofika huku ni serikali kushinikizwa na wakubwa
kujitoa katika kumiliki njia kuu za usafirashaji. Mashirika yetu ya reli,
bandari na ndege yamekufa. Huu ni msiba mkubwa kwa taifa. Athari zake
zinatugusa sote na utaziona kwa macho kila pembe ya nchi. Mwaka 2010 niliandika
kuhusu Athari za Kutokutumia Reli. Makala haya ni muhtasari yake.
Tanzania inatumia magari mengi sana ambayo yanatugharimu pesa
nyingi za mafuta, vipuri na matairi. Matokeo yake ni mfumuko wa bei kwa sababu
ya gharama kubwa za usafirishaji. Kwa mfano mwaka 2010 mfuko wa sementi ulikuwa
unauzwa sh.9,000 katika maduka ya rejareja jijini Dar es Salaam lakini Mwanza
ilikuwa sh 18,000. Gharama za kusafirisha tani moja ya sementi ilikuwa ni sh.150,000 ili hali kwa treni ilikuwa sh.103,663. Hapo utaona zingebaki sh.46,337
mfukoni mwa wananchi kwa kila tani ya sementi, mchele, mahindi, sukari, chumvi
n.k. kama tungetumia treni au sh.2,316.85 kwa kila kilo 50.
Kama nchi nzima tungesafirisha kwa kiwango cha chini kabisa tani
milioni tano tu kwa treni utapata hesabu hii: sh.46,337 zidisha kwa tani
5,000,000 utapata sh 231,685,000,000 (sh bilioni 231.685) ambazo zingebaki
mfukoni mwa wananchi. Hali hii inagusa kila sehemu ya Tanzania. Huko Muleba bei
ya sementi ilikuwa ni sh.23,000 mpaka 25,000. Kumbe behewa la sementi lingekuwa
linafika Mwanza na kuwekwa kwenye meli ya mizigo hadi Kemondo bila shaka
unafuu wa maisha ungekuwa mkubwa kwa mkazi wa Muleba ambaye kipato chake kwa
mwaka ni kati ya sh.100,000 na sh.150,000 kwa mujibu wa takwimu za serikali.
Usafiri wa treni pia ni nafuu sana kwa abiria. Mfano nauli ya
kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza daraja la tatu ilikuwa ni sh.19,000 ili hali
kwa nauli ya basi ilikuwa sh.50,000. Hii ina maana sh.21,000 zingebaki mfukoni
kwake. Kama watu milioni moja wangetumia treni kwa mwaka 2010 ina maana sh.21,000,000,000 zingebaki mfukoni mwao.
Kampuni ya reli kwa sasa ilikuwa na wafanyakazi 3,220 mwaka 2010
baada ya kupunguzwa kutoka 6,500. Kama shirika la reli litasimamiwa vizuri na
serikali litatoa ajira rasmi na zisizo rasmi kwa malaki ya Watanzania. Miongoni
mwa ajira rasmi ni pamoja na wahandisi wa ujenzi na ukarabati wa treni na reli,
madereva wa treni, mafundi katika karakana, wahudumu katika treni za abiria,
wakata tiketi katika vituo, watunza takwimu za usafirshaji mizigo, wapakua mizigo
kwenye mabehewa na hata wafanyabiashara kama kina mama lishe na baba lishe
katika vituo vya treni.
(itaendelea)
sehemu ya pili ya makala hii
No comments:
Post a Comment