******************************************
Tathmini ya muziki wa Tanzania mwaka 2012
makala ya John Kitime
(Sehemu ya pili kati ya sehemu nne)
Muziki
asili pia umekosekana kwenye vyombo vya habari kwa kuwa si vikundi vingi vya
muziki huu vyenye uwezo wa kulipia gharama za studio ambao muziki huu
unastahili kurekodiwa. Studio nyingi zimejengwa kwa ajili ya muziki wa aina ya
Bongoflava tu. Zile studio za kuweza kuruhusu kundi la muziki wa asili kurekodi
gharama yake huwa ni kubwa sana.
Kundi
la Makirikiri lilitakiwa kuwa elimu tosha kwa wasanii wa muziki wa kiasili,
kuwa na muziki huo ukifuata taratibu nzuri ya kurekodiwa unauza vizuri sana. Bahati
mbaya kuna vikundi sasa vimeacha muziki na ngoma zao, vinaiga uchezaji wa Makirikiri.
Pengine
watu watasema nimesahau muziki wa kwaya; sijausahau. Kwa kweli muziki huu
umebaki hasa kwenye muziki wa injili.
Hapo zamani ulikuwa ukitumika sana kwenye siasa na kampeni , lakini kwa mwaka
2012 hali imekuwa mbaya kwa muziki huu.
Pamoja
na kuwa wengine wangeweza kusema tunasonga mbele katika muziki, kwangu mimi
naona tunarudi nyuma kitaaluma. Tasnia inaingiza pesa nyingi zaidi, na hata
kuna wasanii walioingiza pesa nyingi sana, lakini kwangu hilo si kipimo cha maendeleo katika
tasnia hii.
Kama
nilivyoanza kusema washika maikrofon wamekuwa ndiyo alama ya muziki wa Tanzania.
Muziki ni zaidi ya kuimba. Katika kuimba sauti nzuri ya muimbaji ni muhimu, na
ninashukuru kwa hilo tunao waimbaji wazuri wengi sana, lakini ule muziki
unaomsindikiza muimbaji ni muhimu sana kwani ule hauna mipaka wala lugha, na
ndio unaoweza kutufungulia mlango wa soko la kimataifa. Wengi tunapenda sana
muziki wa kutoka Kongo, Nigeria, Afrika Kusini; pamoja na kuwa hatujui hata moja
wanaloliongelea tunaupenda muziki huo kutokana na mpangilio wa vyombo vyao.
Kutokujali
wapigaji katika mfumo wa nchi yetu ndiyo unatupelekea kuwa watu wa ‘copy and paste’ wa upigaji wa muziki wa
nchi nyingine. Ukiorodhesha nyimbo zote zilizotikisa nchi hii kwa mwaka 2012
utagundua asilimia kubwa ya muziki uliotumika ulikuwa ni wa kunakili kutoka
muziki wa nchi nyingine, Nigeria, Congo na Afrika Kusini ndiyo wamekuwa waalimu
wetu wakuu.
Ushauri
kwa ma-producer wa Bongoflava: kuangalia pia muziki wetu wa asili humu ndani ya
nchi ili tuje tumalize 2013 na kitu chetu ambacho Wanaigeria, Wakongo nao pia
waige toka kwetu. Inawezekana sana maana wimbo wa Weekend wa Afro70 uliwahi
kuweko katika kumi bora 1972, Nigeria.
Muziki
wa injili pamoja na kuwa ndiyo unaotegemewa kutufundisha maadili, ulikuwa na
kasoro moja kubwa nayo ni kukosa maadili kwa ku-copy na ku-paste. Nyimbo
nyingi zilizokuwa maarufu na kuteka hisia za maelfu ya watu zilikuwa ni kuiga
moja kwa moja kutoka Afrika ya kusini. Najiuliza je ndiyo kilichopunguza moto wa
muziki huu 2012? Kulikuwa hakuna za kukopi? Wanamuziki wa injili kama ilivyo
kwa ushauri kuhusu Bongoflava, ni muda wa kurudi nyuma na kutumia rasilimali ya
utamaduni iliyoko kuleta mabadiliko na kukuza soko la muziki huo.
(itaendelea)
Taarifa zinazohusiana na hii:
No comments:
Post a Comment