Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, December 20, 2012

Bondia Fadhili Majia kupambana kwenye mchujo wa kuwania ubingwa wa mkanda wa Jumuiya ya Madola


Taarifa kutoka kwa Onesmo Ngowi, Mkurugenzi wa Bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC), inaarifu kuwa bondia Fadhili Majia amepewa nafasi ya kupambana na bondia wa Ghana Isaac Quaye katika mpambano utakaoamua bondia atakayepata fursa ya kugombea mkanda wa Jumuiya ya Madola kwenye uzito wa Flyweight.

Taarifa kamili hii hapa:

Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC) imepiga kura kumruhusu bondia wa Tanzania Fadhili Majia apambane na bondia Isaac Quaye wa Ghana katika mchujo (Elimination) wa kutafuta mpinzani atakayekutana na bingwa wa mkanda wa Jumuiya ya Madola katika uzito wa Flyweight Kevin Satchell wa Uingereza. Mpambano wa Fadhili Majia na Isaac Quaye utafanyika jijini Accra, Ghana tarehe 22, Februari 2013.

Rais wa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Onesmo Ngowi ni mmoja wa wakurugenzi wa bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola na alikuwa wa kwanza kumpigia bondia Fadhili Majia kura ili acheze na Quaye.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa bondia Fadhili Majia kugombea mkanda wa Jumuiya ya Madola ambayo inaziunganisha nchi zote zilizokuwa zinatawaliwa na himaya ya Uingereza.

Wakati huo huo Bodi ya Wakurugenzi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola imepitisha azimio la kuruhusu ubingwa wa baraza hilo katika bara la Afrika. Ubingwa huo utakuwa unajulikana kama “CBC Africa Zone” na tayari wapo mabondia kadhaa wa nchi za Afrika ya Magharibi ambao wameshandaa mapambano mwakani.

Napenda kuwahamasisha mapromota wa Kitanzania kuchangamkia fursa hizi adimu na kuandaa mapambano ya ubingwa wa "CBC Africa Zone" kwa manufaa ya mabondia wetu.

TPBC imejiandaa kuwatafutia mabondia wa Kitanzania mapambano mengi ya nje ili waweze kujijenga kimchezo na pia kuweza kupata kipato kizuri.

Imetumwa na mimi:

Onesmo Ngowi
Rais, Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Nchini (TPBC)
Mkurugenzi wa Bodi ya Baraza la Ngumi la Jumuiya ya Madola (CBC)

No comments: