Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Saturday, December 22, 2012

Dk. Antipas Massawe anasema Muungano umepitwa na wakati (sehemu ya pili kati ya sehemu mbili)

Katika awamu hii ya pili ya makala yake, Dk. Antipas Massawe anaendeleza na kuhitimisha hoja kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umepitwa na wakati. Ni mawazo yake, si yangu.
*************************************
Muungano wa Tanzania umepitwa na wakati demokrasia ya vyama vingi ilipozaliwa (sehemu ya pili kati ya sehemu mbili).

Na Dk. Antipas Massawe

(inaendelea)

Kwa sehemu ya kwanza ya makala hii soma hapa:Athari ya tatu kubwa itarajiwe kujitokeza pia pale ambapo muundo wa muungano unaojumuisha serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika) utakapokataliwa kama mfano wa kuigwa na hivyo kuwa hata kikwazo kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa  Bara la Afrika unaoshirikisha Zanzibar na Tanganyika. Muundo wa muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika ilibidi uwe ni ule unaotarajiwa utakubalika kama mfano wa kuigwa na wengine wote kama msingi kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na hatimaye muungano wa Bara la Afrika tarajiwa. 

Vinginevyo huu muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulioundwa kwa mfumo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika) utaishia kuwa kikwazo kwa ushiriki wake kamilifu na wenye manufaa makubwa ndani ya Shirikisho la Afrika ya Mashariki  na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa.

Mfumo wa serikali moja ya Muungano ni mzuri kwani ndio wenye gharama ndogo lakini kwa Wazanzibari ambao karibu wote ni Waisilamu na Wabara ambao karibu wote ni mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu mfumo huu bado sio mzuri kwani utatujengea agenda za udini ndani ya demokrasia yetu ya vyama vingi na matokeo yake ni pande zote za Muungano zikijikuta kulazimishiwa serikali dhaifu na kunyimwa ile imara na kuandamwa na chuki na migogoro ya kidini kama illivyoshuhudiwa huko Zanzibar hivi karibuni. 

Mfumo huu pia sio mzuri kwani kila pande ndani ya Muungano utashindwa kubuni na kuendeleza fursa zake nyingi muhimu kwa maendeleo yake binafsi ambazo hazitaonekana muhimu katika ngazi ya Muungano. Nadhani hili ni mojawapo ya yaliyopelekea muungano wa nchi za Kisovieti kusambaratika. Ni sababu hii inaoufanya mfumo huu wa serikali moja ya Muungano kutoweza kuwa msingi mzuri wa kuigwa kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa.

Mifumo ya serikali mbili kwenye muungano (ya Zanzibar na ya Muungano) na mbili (ya Tanganyika na ya Muungano) sio mizuri kwa Wazanzibari ambao karibu wote ni Waisilamu na Wabara ambao karibu wote ni mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu kwani katika mazingira kama hayo utakuwa ukitujengea agenda za udini ndani ya demokrasia yetu ya vyama vingi na kutuletea athari zake mbaya. Mfumo huu pia sio mzuri kwani hakuna sababu zozote za msingi na zinazokubalika na pande zote mbili husika ndani ya Muungano pale ambapo upande mmoja ukiruhusiwa kuendelea kuwa na serikali yake binafsi na upande mwingine ukinyimwa fursa kama hiyo. Ni sababu hii inaoyoifanya mifumo hii ya serikali mbili za muungano kutoweza kuwa misingi mizuri ya kuigwa kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa.

Mfumo wa serikali tatu kwenye muungano (ya Zanzibar, ya Tanganyika na ya Muungano) sio nzuri kwani haitakuwa rahisi kujenga hoja za msingi kudhihirisha manufaa  ya kuwa na serikali ya tatu ya Muungano yenye gharama kubwa kati ya Zanzibar ambayo ni kisiwa kidogo sana ndani ya bahari ya Hindi na Tanganyika ambayo ni nchi kubwa sana ndani ya Bara la Afrika. Hata hivyo mfumo huu wa kila mhusika ndani ya Muunngano kuendelea kuwa na serikali yake ndani ya serikali ya muungano unaonekana ndio mfumo mzuri wa kuigwa kwenye ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa kwani kutokana na wingi wa mataifa shiriki ndani ya muungano, ajenda za udini zitakosa fursa ya kujijenga na kukua ndani yake na kila taifa shiriki na serikali yake litaendelea kuwa na fursa ya kubuni na kuendeleza zile ajenda na sera zake binafsi za maendeleo ambazo hazionekani muhimu katika ngazi ya serikali ya muungano.

Mfumo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya Tanganyika bila ya muungano) inaonekana ndiyo  unaofaa kuzijengea Zanzibar na Tanganyika uhusiano na ushirikiano mzuri na endelevu na uliojengeka kwenye misingi imara, urafiki na ushirikiano wa kibiashara baina ya mataifa mawili huru na jirani. Mfumo huu wa serikali mbili bila ya muungano utazipa pande zote mbili husika fursa nzuri kwa kila moja kushiriki kikamilifu kwenye mchakato mzima wa ujenzi wa Shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika tarajiwa ikizingatia maslahi yake binafsi na ya wote kwa ujumla.

Muungano wa Zanzibar na Tanganyika unaohusisha mfumo wa serikali mbili (ya Zanzibar na ya muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika) umepitwa na wakati pale ilipozaliwa demokrasia ya vyama vingi na ni budi ujadiliwe upya kwa kina na mapana kuendana na nyakati tulizo nazo na mazingara ya demokrasia ya vyama vingi tuliyo nayo hivi sasa ili athari na faida zake ziweze kuonekana bayana na kuwawezesha Wazanzibari  na Wabara wengi kuweza kuamua ni mfumo upi wa ushirikiano unaowafaa kuendelea nao badala ya huu uliopitwa na wakati.

Makala inayohusiana na hii hapa:
Sehemu ya kwanza ya makala hii:
http://muhunda.blogspot.com/2012/12/dk-antipas-massawe-anasema-muungano.html
Makala nyingine juu ya Muungano:
http://muhunda.blogspot.com/2012/08/mada-yangu-ya-leo-muungano-una-manufaa_24.html

No comments: