Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, December 24, 2012

Kuzima simu ndani ya benki ni usumbufu tu

Ukiingia benki nyingi za Tanzania utakutana na tangazo linalozuwia kutumia simu ukiwa ndani ya benki na inawezekana kuambiwa kuzima simu yako ya kiganjani ukijaribu kuitumia.

Sijaelewa mantiki ya kanuni hii. Naamini kuwa wenye mabenki wana hofu kuwa mtu mwenye kusudio la kutenda uhalifu ndani ya benki anaweza kutumia simu kurahisisha uhalifu huo. Na hii inawezekana kuwa ni kweli lakini mtu aliyekusudia kufanya uhalifu atafanya hivyo katika mazingira yoyote yale.

Hapa inaleta maana kuwa jambazi asiye na simu hawezi kutenda uhalifu. Nimewahi kumueleza mfanyakazi wa benki aliyenizuwia nisiongee na simu kuwa kuna wahalifu wengi wapo nje ya nchi ambao wanaibia mabenki kwa njia ya mtandao. Wao wameambiwa nao wazime kompyuta zao? Na yule askari mwenye silaha ambaye yuko nje ya benki kazi yake nini? Kuelekeza wateja kuegesha magari tu na kutumia mashine za ATM?

Mimi imenitokea mara kadhaa simu yangu kuita nikiwa ndani ya benki lakini mara zote hujitahidi kumaliza mazungumzo haraka ili nimalize yaliyonipeleka benki kwanza halafu ndiyo, kwa wakati wangu, nimtafute huyo aliyenipigia kumalizia mazungumzo iwapo hayakuisha.

Ingeleta maana zaidi kwa wenye mabenki kusema kuwa mteja anapoingia benki amalize yaliyompeleka benki kwanza halafu ndiyo aanze kuongea na simu kwa sababu mshika mawili moja humponyoka, lakini hoja kuwa mtu siye na simu hawezi kufanya ujambazi haina uzito wowote.

No comments: