Katika makala hii ambayo nitaitoa hapa kwa awamu mbili, Dk. Antipas Massawe anatoa hoja kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umepitwa na wakati. Ni mawazo yake, si yangu.
*************************************
Muungano wa Tanzania umepitwa
na wakati demokrasia ya vyama vingi ilipozaliwa (Sehemu ya Kwanza kati ya sehemu mbili).
Na Dk. Antipas Massawe
Muungano wa kisiasa kati
ya Tanganyika na Zanzibar ulizaliwa tarehe 26 April, 1964. Sababu kubwa iliyopelekea
kuzaliwa kwake ni moyo waliokuwa nao waasisi wake (Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume) wa kuunda muungano wa kisiasa baina ya
nchi huru za Bara la Afrika wakianzia na shirikisho la Afrika ya Mashariki. Lengo
lilikuwa kulinda na kudumisha mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 dhidi
ya utawala wa wachache wa kisultani ulioondolewa madarakani na kuanzisha ujenzi
wa shirikisho la Afrika ya Mashariki na muungano wa Bara la Afrika kisiasa.
Kuzaliwa kwa muungano wa
Tanganyika na Zanzibar kulitokana na matakwa binafsi ya waasisi wake na wananchi
wa kawaida kutoka pande mbili husika hawakushirikishwa kikamilifu katika zoezi zima
la kufanya maamuzi kuhusu kuundwa kwake na haionekani mahali popote upembuzi
yakinifu ulifanyika kubaini faida na athari za muungano wenyewe kwa wahusika (ukijumuisha
mifumo ya serikali zake zote mbadala: moja (ya Muungano), mbili (ya Zanzibar na
ya Muungano), tatu (ya Tanganyika na ya Muungano), nne (ya Zanzibar, ya
Tanganyika na ya Muungano) na tano (ya Zanzibar na ya Tanganyika bila ya
Muunngano). Kwa kifupi muungano wa Zanzibar na Tanganyika ulizaliwa wakati wa
kipindi cha udikteta wa chama kimoja tawala ndani ya pande zote mbili husika
kwenye Muungano.
Muungano wa Zanzibar na
Tanganyika ni wa pekee na haujawahi kuigwa na wengine mahali popote duniani na
umedumu chini ya utwala wa mfumo wa udikteta wa chama kimoja na sasa uko chini
ya utawala wa demokrasia ya mfumo wa vyama vingi.
Athari kubwa kutokana na Muungano hazikuweza
kuonekana kwenye kipindi chake cha awamu
ya kwanza chini ya mfumo wa udikteta wa chama kimoja kwani kwenye kipindi hiki chama
tawala ndicho kimekuwa kikiamua yote kuhusu maswala ya Muungano kitaifa na jukumu
la wengine wote kutoka bara na visiwani lilikuwa ni kubariki maamuzi hayo ya chama
kimoja tawala. Kwa mfano, chama kimoja tawala kikishaamua huyu ndiye
atakaeyekuwa rais wa Muungano, basi jukumu la wengine wote kutoka pande mbili
za Muungano limekuwa ni kupiga kura moja ya ndio kuashiria kubariki kwao chaguo
la chama hicho kimoja tawala.
Kwa hiyo kutokuwepo
upinzani kutoka vyama vingine vya siasa dhidi ya udikteta wa chama kimoja tawala
kuhusu maswala ya Muungano na rais mteule wa chama tawala kutokuwa na ushindani
wa wagombea kutoka vyama vya upinzani imekuwa ndiyo sababu ya athari kubwa
tarajiwa kushindwa kujitokeza kutokana na utekelezaji wa Muungano huu baina ya
Wazanzibari (ambao karibu wote ni Waisilamu) na Wabara (ambao karibu wote ni
mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu) na fursa iliyopewa Zanzibar ya kuendelea
kuwa na serkali yake ya Zanzibar wakati Tanganyika ikinyimwa fursa kama hiyo ya
kuendelea kuwa na serikali yake ya Tanganyika bila sababu zozote za msingi.
Athari ya kwanza kubwa kutokana na huu Muungano wa kisiasa baina ya Wazanzibari na Wabara inatarajiwa kujitokeza kwa nguvu kwenye kipindi chake cha
awamu ya pili chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Kwa mfano itakapojitokeza
kwamba miongoni mwa wagombea wa kiti cha urais mmoja ni Mkristu na mwingine ni Mwisilamu basi itarajiwe kwamba karibu Wazanzibari wote ambao ni Waisilamu watajitokeza
na kumpigia mgombea Muislamu kura ya ndio bila kuzingatia vigezo vingine vya
ubora. Athari ni kwamba Muungano huu utakuwa unatujengea ubinafsi unaoambatana
na agenda zenye lengo la kutujengea na kutuimarishia udini ndani ya demokrasia
ya vyama vingi na matokeo yake ni Muungano kunyimwa utawala bora pale matakwa
ya udini yatakapotawala chaguzi kuu za uongozi ndani ya Muungano na chuki za
kidini na migogoro yake na athari zake kuanza kujitokeza kama ilivyoshuhudiwa huko Zanzibar hivi
karibuni.
Athari ya pili kubwa kutokana na huu Muungano uliowapa Wanzanzibari
fursa ya kuendelea kuwa na serikali yao ya Zanzibar wakati Wabara wakinyimwa
fursa kama hiyo ya kuendelea kuwa na serikali yao ya Tanganyika itarajiwe pia
kujitokeza kwenye awamu yake ya pili chini ya mfumo wa demokrasia ya vyama
vingi kwani sio haki Wazanzibari kufaidi kushiriki ndani ya serikali ya
Tanganyika na bunge lake kupitia serikali ya Muungano na bunge lake wakati Wabara hawana fursa kama hiyo kutokana na kutoshirikishwa ndani ya serikali ya
Zanzibar na bunge lake na uwezekano mkubwa wa mgongano wa maamuzi na utekelezaji
wa sera za serikali ile ya Zanzibar na za ile ya Muungano.
(itaendelea...)
No comments:
Post a Comment