Na Amani Millanga
Vijana hawa wanazijua haki zao na mahitaji yao ya msingi ya kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao, ya chakula, malazi na mavazi. Kama ilivyo kwa binadamu yeyote awaye, vijana hawa hawataki kuishi katika maisha duni ya kimaskini. Wanataka ustawi na maisha bora kwao na vizazi vyao.
Pia tufahamu kwamba vijana hawa, kwa jitihada zao binafsi, ni wajuzi katika fani mbalimbali kuanzia ufundi mekanika hadi ujenzi wa nyumba. Wana maarifa ya kuendesha biashara tena kwa faida. Wanajua fika wafanye nini ili wastawi. Ni wafanyakazi hodari ndio maana wanaweza kujilisha na si wezi. Lakini ni bahati mbaya sana katika safari yao ya maisha, njia yao imejaa vikwazo vya kila namna - dhuluma na uonevu; rushwa na ufisadi. Kutokana na hali hii vijana hawa wamekata tamaa. Wengi wao hawana tena tumaini la maisha bora. Ndoto zao zimekufa.
Sasa wanazivuta hisia na wameanza kuandamana wakiungwa mkono na wazee, wafanyakazi maofisini na jamii inayowazunguka wanawake kwa wanaume. Nilifuatilia maandamano ya Mwanza na taarifa nilizozipata zinasema kwamba wanawake katika maeneo ya jiji hilo walikuwa na ndoo za maji tayari kuwapatia vijana wanawe nyuso zao pindi mabomu ya machozi yakipigwa.
Mapambano ya Mbeya nasikia yalikuwa ni makali kweli. Katika maandamano ya vijana kudai haki zao tumeiona ‘NGUVU YA VIJANA’ ikitembea. NGUVU hii ya vijana ikiachwa bila kupewa majibu na suluhisho la matatizo yao ITAUMA NA TAIFA LITAUMIA. Tumeiona mifano kila pembe duniani na hivi karibuni katika nchi za Kiarabu. Tusifike huko.
Kuwauwa
Waandamanaji ni Kuitia Amani Kitanzi
Kuwauwa
waandamanaji ni sawa na kuiwekea kitanzi amani. Hali hii inaweza kusababisha maandamano
yenye ghasia kuibuka nchi nzima. Nayo serikali ikajikuta inatumia mabavu zaidi
kuyazima maandamano haya. Katika kuyazima maandamano ipo nafsi kubwa sana ya
watu wengi kupoteza maisha. Watu wakipoteza maisha chuki itaongezeka na damu
nyingi zaidi itazidi kumwagika kutokana na mapambano kati ya raia na vyombo vya
dola. Huo ndio wakati ambao unasubiriwa kwa hamu kwa wasioitakia mema Tanzania. Hapo litatolewa tamko katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu umwagaji damu huo na ukiukwaji wa haki za binadamu. Serikali itaingia katika mgogoro mkubwa ndani na nje katika jumuiya ya kimataifa. Matamko yatatolewa na wananchi ndani ya nchi na pia mataifa makubwa ya nje kwamba serikali ijiuzulu na Chama cha Mapinduzi (CCM) kama chama tawala kiachie ngazi.
Hatujui nini itakuwa ni hatima ya hali hii. Lakini ukweli ni kwamba amani haitakuwepo tena. Watu wengi wasio na hatia watauwawa na wengine watakuwa wakimbizi. Uchumi na ustawi utavurugika. Kwa hiyo basi Polisi ijitahidi sana kuepuka kuuwa raia wasio na hatia. Itumike busara zaidi na nguvu za kadri na kadri za “piga lakini chunga usiuwe” na si risasi za moto. Tukumbuke kuwa Tanzania ni katika nchi chache sana Afrika ambayo haijaingia katika machafuko. Na yapo mataifa yanataka siku moja Tanzania itikiswe ili waone nini kitatokea. Mungu atuepushe balaa hili.
No comments:
Post a Comment