Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Monday, March 26, 2012

Amani Millanga azungumzia maandamano ya Songea (sehemu ya tatu kati ya sehemu tatu)

Vijana na Maandamano, Polisi na Mauwaji: Tunaelekea Wapi? (Sehemu ya tatu kati ya sehemu tatu)

Na Amani Millanga

Wengi watakubaliana nami kuwa kiini hasa cha watu kuandamana ni kukithiri kwa umaskini nchini, ukosefu wa ajira kwa vijana, uonevu, kutokuthaminiwa kwa UTU wa watu na kuheshimiwa HAKI zao, maisha kuwa ghali, unyonyaji na dhuluma.

Katika hotuba yake ya “Wasia wa Mwalimu Nyerere kwa CCM” Hayati Baba wa Taifa aliyachambua vema mambo haya aliposema hivi:

“Tanzania isikosee ikaacha msimamo wake wa kuhakikisha kwamba uko usawa wa binadamu, kuna usawa wa msingi katika hali ya maisha ya kila mtu, na kwamba kuna heshima ya binadamu kwa kila raia wa Tanzania. Tukifanya kosa kama hilo tutavuruga msingi wote wa utulivu na amani katika nchi yetu. Maana yake ni kwamba tutaruhusu na kuimarisha tabaka na fikira za ‘Sisi’na ‘Wao’. Tutaacha watu wachache wawe na mali nguvu, na fidhuli ya kuwa na mali na nguvu; watu wengi wawe ni maskini na wanyonge; na wana maning’uniko na ghadhabu za umaskini na unyonge. Mgawanyiko wa namna hiyo ni hatari sana. Utaratibu wa vyama vingi katika mazingira na hali fulani unaweza usiathiri utulivu. Lakini tofauiti kubwa sana za mapato na hali ya maisha au hata matumaini tu ya maisha mema ya baadaye haziwezi kuzaa utulivu. Mimi siamini hata kidogo kwamba mnaweza kujenga amani na utulivu wa kudumu katika nchi masikini bila kuheshimu misingi ya haki na usawa. Na ‘unyang’au’ kwa hulka yake hauheshimu misingi ya haki na usawa.”

Suluhisho
Hatima ya maisha ya vijana si suala dogo la kuacha lijimalize lenyewe. Linataka kutafutiwa ufumbuzi wa haraka na wa kudumu. Suluhisho la kweli ni kurudi katika miongozo ya Mwalimu Nyerere ya kuthamini UTU na USAWA wa watu na kuheshimu HAKI zao. Tuonyeshe kwa vitendo kwamba kweli tunazijua, tunazitambua na kuguswa na shida za watu. Na kwamba kwa uhakika kabisa kabisa tunazifanyia kazi. Na matunda au matokeo ya kazi hiyo yanaonekana. Shaaban Robert aliandika, “Matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno.”

Vijana wanataka matendo. Wanataka ajira. Wanataka huduma bora ya afya. Wanataka elimu bora kwao na vizazi vyao. Wanataka kunufaika na utajiri wa raslimali za nchi. Wanataka rushwa idhibitiwe. Dhuluma, uonevu na unyonyaji vikomeshwe. Kazi hizi zinafanywa na serikali. Lakini serikali ina wajibu wa kuyafanyia kazi mambo haya na kuleta majibu ya kuwaridhisha vijana na wananchi. Matokeo yake imani ya vijana na wananchi kwa CCM na serikali yake itarudi.

Nayasema haya kwa upendo na moyo mweupe kabisa kama mfuasi wa siasa na mafunzo ya Mwalimu Nyerere na kada wa CCM (nje ya chama ndani ya umma) – chama kilichoijengea Tanzania heshima katika Afrika na kote duniani. Chama kilichosimamia na kutetea haki za wanyonge ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Wakati umefika sasa wa kuirejesha hadhi ya CCM. Kinyume chake basi kauli aliyoitoa Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ya “Bila CCM Madhubuti Nchi Itayumba” itatimia siku si nyingi. Pia nitumie fursa kuwasihi vijana na wananchi kwa ujumla kuepuka matumizi ya nguvu, jazba na hasira pale wanapoandamana kwani hasira haimalizi hasira. Amani ikishapotea ni vigumu sana kuirejesha.

Hitimisho
Nimalizie kwa kusema kwamba kuiuwa nafsi isiyo na hatia ni dhambi kubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi. Katika Quran Mwenyezi Mungu anasema katika SURAT AL MAIDA (Sura ya 5: Aya 32) kwamba:

“Kwa sababu ya hayo tuliwaandikia Wana wa Israili ya kwamba aliye muuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi (ufisadi) katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote. Na hakika waliwajia Mitume wetu na hoja zilizo wazi. Kisha wengi katika wao baada ya haya wakawa waharibifu katika nchi.”

Pia katika Biblia Mwenyezi Mungu katika Amri ya sita anasema “USIUWE”. Iweje leo tunaanza kuuwana? Tutaiua Tanzania.

Namuomba Mungu azidi kuibariki Tanzania. Adumishe Uhuru na Umoja kati ya wanawake, wanaume na watoto wa Tanzania kwani Uhuru na Umoja wetu ndizo ngao zetu za kuilinda na kuikinga amani yetu isitoweke.

No comments: