Katika makala yake hii ambayo nitaitoa katika
sehemu tatu, Amani Millanga anahoji ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa
wawekezaji na, kwa maoni yake, utaratibu huu unaturejesha kwenye ukoloni.
Kwa mujibu wa takwimu za serikali, Tanzania
inazo hekta 44 milioni za ardhi nzuri ya kilimo. Kwa sasa ni asilimia 23 tu ya
ardhi hiyo inatumika kwa kilimo, ambayo ni sawa na hekta 10,120,000. Hii
ina maana kwamba tuna ziada ya hekta 33,880,000 (yaani hekta 44,000,000 kutoa
hekta 10,120,000). Ziada hii ya ardhi ambayo haitumiki kwa lolote inaonekana ni
kubwa sana. Hoja iliyoko mezani ni kuikodisha ardhi kwa wakulima wakubwa wa
kigeni kwa ajili kilimo cha mashamba makubwa ili serikali na wananchi wanufaike
na ardhi hii ambayo “haizalishi”.
Zinatolewa hoja kwamba wakulima wa kigeni
wataleta teknolojia ya kisasa na mitaji mikubwa itakayohuisha kilimo na kutoa
ajira kwa Watanzania. Kwamba “kupitia ukodishaji wa ardhi kwa wageni Tanzania
itafanya mapinduzi makubwa ya kijani na hatimaye kupunguza umaskini”.
Ni hoja tamu, na zimeongeza kasi zaidi katika
ukodishaji ardhi ili “tunufaike na kilimo cha kibiashara” ambacho kimsingi kipo
tokea tupate uhuru. Zinatolewa hoja kwamba “Watanzania wasiwe na wasiwasi kwani
ardhi ni mali ya taifa kwa mujibu wa Katiba na sheria.” Kwamba “mwekezaji
atakodishwa ardhi kwa muda wa miaka 33, 66 au 99 na baada ya hapo ardhi
itarejeshwa serikalini.” Hivyo basi “tuwapokee wakodishaji ardhi kwa mikono
miwili kwani wanaleta neema.”
Hoja hizi hazina mashiko kwani
zinahalalisha kurejeshwa kwa ukoloni kwa mgongo laini wa ukodishaji ardhi
jambo ambalo ni hatari sana kwa Tanzania ya leo na kesho na nitaeleza kwa nini.
Ukoloni unazo sura
nyingi sana na mbinu kila aina za kuliteka taifa. Ukodishaji ardhi ni njia
mojawapo ya kuukaribisha ukoloni mpya wa kutawaliwa na makampuni ya kibeberu.
Ukisema hili wanajibu kwamba “hizo ni fikira za kale -Tanzania ni nchi huru.”
Lakini ukweli unabaki
pale pale kwamba taifa-nchi (nation-state)
ni ardhi. Hivi taifa-nchi linakaa wapi? Unapoikodisha ardhi kwa miaka 99 ina
maana umeifanya ardhi hiyo kuwa ni koloni kwa miaka 99. Wajerumani na Waingereza
walitutawala jumla ya miaka 77. Katika miaka 99 na nguvu ya pesa, mlowezi
atafanya atakavyo. Na kwa kufanya hivi atakavyo Watanzania watageuzwa watumwa
ndani ya nchi yao. Watanyanyaswa na kupigwa viboko. Tunayashuhudia haya
yakifayika katika migodi ya dhahabu hadi Watanzania kuuwawa. Na katika Tanzania
inayokumbatia rushwa na ufisadi mwekezaji anakingiwa kifua.
Je Mtanzania kibarua
katika shamba la mlowezi atapata haki yake? Zipo taarifa nyingi kwamba kwa
kutumia rushwa wageni wanapewa ardhi bwerere. Na kwa mchakato uliopo wa uraia
wa nchi mbili (kama utapitishwa) katika siku si nyingi walowezi watapewa uraia
na Tanzania ya kesho itageuka kuwa Zimbabwe ya sasa. Watanzania wataidai ardhi
yao na walowezi wataiweka Tanzania katika msukosuko mkubwa.
Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/kaburi-la-mbaguzi-nambari-wani-cecil.html
Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/kaburi-la-mbaguzi-nambari-wani-cecil.html
No comments:
Post a Comment