Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Sunday, January 27, 2013

Kwenye soka huwa nashangilia wanyonge siku zote


Makala hii niliandika zaidi ya miaka mitatu iliyopita kwenye blogu yangu ya lugha ya Kiingereza. Nairudia hapa kwa wale ambao hawakupata fursa kuisoma wakati huo, tarehe 30 Juni 2009. Nimekosa kuangalia mapambano ya Kombe la Mataifa ya Afrika yanayoendelea sasa hivi nchini afrika Kusini lakini ningekuwa nafuatilia mashindano hayo ningekuwa nawapigia debe wanyonge, timu ambayo hakuna shabiki anatarajia itashinda.
*********************************************
Mimi siku zote hushangilia wanyonge, hususani kwenye michezo. Kwa hiyo nilifurahishwa Jumapili iliyopita nilipowasha televisheni na kushuhudia hali isiyo ya kawaida ambapo timu ya taifa ya Marekani ikiwa inaongoza kwa goli moja bila majibu na, kabla ya kipenga cha nusu ya kwanza kusikika, ikiongoza kwa magoli mawili dhidi ya miamba ya soka Brazil kwenye pambano la fainali za mabara la FIFA nchini Afrika ya Kusini.

Katika ulimwengu wa soka Brazil inatisha, ni taifa kubwa wakati Marekani ni bwana wadogo. Katika lugha ya vita na silaha Brazil ni mzinga wa upana wa milimita 130 wakati Marekani ni kama bastola ndogo isiyojaza hata mfuko wa shati. Kwa hiyo si ajabu kumsikia kocha wa Marekani Bob Bradely akisema baada ya timu yake kushindwa: "Ni matarajio yangu kuwa watu katika sehemu mbalimbali duniani wataona kuwa tunayo timu na wachezaji wazuri. Ni hatua kubwa kwetu."
Timu ya Taifa ya Brazil iliyoshinda Kombe la Dunia mwaka 1970 nchini Mexico.
Timu nilizozishabikia kwenye mashindano zilikuwa mlolongo wa timu zilizoorodheshwa na FIFA kwa ubora lakini orodha ile ikiwa imewekwa kichwa chini miguu juu, yaani zile za mwisho ndiyo nilipendelea zaidi zishinde.

Katika kipindi cha pili Brazil walisawazisha mabao yote mawili na kuongeza bao la tatu la ushindi ambalo lilikuwa uthibitisho kuwa Brazil itabaki inatawala ulimwengu wa soka, angalau kwa sasa.

Habari njema kwa timu nyingine ambazo zitapambana na Brazil kwenye Kombe la Dunia la FIFA mwakani nchini Afrika ya Kusini ni kuwa bingwa wa FIFA wa mabara - ambapo mabingwa wa mabara wanapambana dhidi yao - hajawahi kutwaa ubingwa wa dunia mwaka unaofuata.

Taarifa zinazohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/mada-yangu-ya-leo-ni-nani-ataibuka.html
http://muhunda.blogspot.com/2010/06/hii-kali.html

No comments: