Leo Mwaka Mpya. Heri ya Mwaka Mpya kwa wote, na matarajio yangu ni kuwa huu utakuwa mwaka wa mafanikio makubwa kwako.
Mwaka mpya 2010 ningeulizwa ningependa kuwa wapi itakapotimia sekunde ya kwanza ya 2010 nadhani ningetaja chumbani kwangu kwa sababu hiyo ndiyo sehemu ambayo nimeadhimisha Mwaka Mpya kwa miaka mingi iliyotangulia. Kama ningeshinikizwa kutaja sehemu yoyote mahususi labda ningetaja Kilele cha Uhuru, juu ya Mlima Kilimanjaro.
Lakini kilichotokea Mwaka Mpya 2010 nisingeweza kutabiri hata kidogo. Nilikuwa na safari ya kutoka Butiama hadi Mwanza nikiwa njiani kuwahi ndege ambayo ingeanza safari saa 2:00 usiku, siku ya Alhamisi tarehe 31 Desemba, kuelekea Dar es Salaam. Kwa kawaida ya safari hiyo ndege huwasili Dar es Salaam kabla ya saa 6:00 usiku. Hata hivyo kabla ya kuondoka Butiama nilipata taarifa kuwa safari ile ya Air Tanzania ingechelewa kuondoka Mwanza na kuwa safari ingeanza saa 5:00 usiku. Na ndivyo ilivyotokea.
Saa moja baada ya kupaa na kama nusu dakika kabla haijatimia saa 6:00 usiku, rubani Kapteni Karim alitutangazia abiria kuwa tulianza safari toka Mwanza mwaka 2009 na tutawasili Dar mwaka 2010.
Natambua kuwepo mamia ya abiria ambao hutumia saa kadhaa na mwaka mmoja hadi mwingine kuanza na kumalizia safari zao lakini nadiriki kusema kuwa ilikuwa hisia ambayo siyo ya kawaida.
Juma moja kabla ya hapo mtu angeniambia kuwa itakapofika Mwaka Mpya nitakuwa usawa wa futi 20,000 juu ya bahari ningemwambia kuwa hizo ni njozi tu.
Tuesday, January 1, 2013
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment