Katika sehemu ya pili ya makala yake hii ambayo nitaitoa katika sehemu tatu, Amani Millanga anahoji ukodishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji na, kwa maoni yake, utaratibu huu unaturejesha kwenye ukoloni.
**********************************************************
Mali ya Taifa (sehemu ya pili)
Na Amani Millanga
Hoja ya pili kwamba “ardhi
bado ipo” ni hoja ambayo inatolewa bila kuangalia kwa mapana na kina athari za
ukodishaji ardhi kwa wageni. Mwaka 1961 idadi ya watu ilikuwa ni milioni
kumi. Miaka 50 baadaye Tanzania ilikuwa na watu milioni 45. Hii ina maana
kwamba idadi ya watu imeongezeka mara 4.5 toka milioni kumi hadi milioni 45
mwaka 2011.
Kwa msingi wa hesabu hii
ina maana kwamba katika miaka 50 ijayo (mwaka 2061) Tanzania itakuwa na
watu milioni 45 x 4.5 = watu milioni 202.5. Je watu hawa wataishi wapi?
Watajimudu vipi? Watapata wapi ardhi ilhali sehemu kubwa ya ardhi yetu itakuwa
imekodishwa kwa wageni kwa miaka 99?
Hapo ina maana kwamba
utakuwa na miaka 49 ya wawekezaji kumaliza muda wao. Katika hii miaka 49 (yaani
mwaka 2110) idadi ya Watanzania itakuwa imeongezeka tena mara 4.5 (tukitumia
msingi wa hesabu yetu wa ongezeko la watu wa mara 4.5) kwa maana kwamba watu
milioni 202.5 x 4.5 = Tanzania itakuwa watu milioni 911.25 Hadi idadi ya watu
inafikia kiwango hiki cha milioni 202.5 katika miaka 50 ijayo (mwaka 2061) au
milioni 911.25 katika miaka 99 ijayo (mwaka 2110) tufahamu kwamba itakuwepo
vita kali sana ya wananchi kuidai ardhi yao. Wengi watakufa bure kwa sababu ya
maamuzi yasiyo ya kizalendo yanayotolewa hivi sasa ya kukodisha ardhi.
Mtu anaweza kusema ni
jambo ambalo haliingii akilini kwamba Tanzania katika miaka 99 ijayo itakuwa na
watu milioni 911.25. Lakini hili ni jambo ambalo linawezekana tukidurusu
historia ya ongezeko la watu duniani. Ukiziangalia takwimu za
ongezeko la idadi ya watu duniani katika miaka 2000 iliyopita utaona kwamba
ongezeko kubwa la watu limekuwepo katika miaka 200 tu iliyopita. Mwaka 1800
dunia ilikadiriwa kuwa na idadi ya watu bilioni moja na mwaka 1900 idadi ya
watu iliongezeka na kufikia bilioni moja na nusu. Tokea mwaka 1800 hadi mwaka
2000 idadi ya watu iliongezeka mara sita kufikia watu bilioni 6.1.
Katika kipindi cha miaka
12 tu yaani mwaka 2000 hadi mwaka 2012, idadi ya watu duniani imeongezeka kwa
kasi kubwa sana na imefikia watu zaidi ya bilioni 7.1 kwa mujibu wa tovuti http://www.worldometers.info/world-population/. Umoja wa Mataifa unakadiria idadi ya watu itakuwa
bilioni 9 ifikapo mwaka 2050 na ongezeko kubwa la watu liko Afrika, kusini mwa
Jangwa la Sahara, ambayo itakuwa na watu bilioni 2.756 mwaka 2050, likiwa ni
ongezeko la watu bilioni 1.9 kutoka watu milioni 856 mwaka 2010 (ongezeko la
watu zaidi ya mara mbili katika miaka 40) na 39% ya watu wenye umri kati ya miaka
15 hadi 24 duniani watakuwa Waafrika ifikapo mwaka 2100 kutoka 14% mwaka 2010.
Kwa hiyo upo ushahidi wa
kutosha kwamba katika miaka 50 ijayo Tanzania itakuwa na watu milioni 202.5.
Ardhi haiongezeki. Sasa katika hizo hekta milioni 44 tulizonazo ambazo kwa
idadi ya watu ya milioni 45 ya mwaka 2011 ni sawa na hekta 0.977 kwa kila Mtanzania
(kwa maana ya hekta milioni 44 gawa kwa watu milioni 45). Je hamuoni kwamba
wastani huo wa ardhi kwa kila mtanzania utakuwa umeshuka sana katika miaka 50
ijayo?
Hesabu hii itatupa
mwanga: hekta milioni 44 gawa kwa watu milioni 202.5 utapata hekta 0.217 kwa
kila mtanzania. Je katika kasi hii ya kukodisha ardhi kwa wageni wastani huu wa
hekta 0.217 utakuwepo kwa kila mtanzania? Ardhi itapatikana wapi? Bila shaka
vijana watasimama kuidai ardhi tena kwa mabavu.
Ni ukweli usio na shaka
kwamba idadi ya watu wanaohama vijijini kwenda mijini inaongezeka lakini hii
haina maana kwamba katika miaka 50 ijayo 80% ya Watanzania itakuwa inaishi
mijini na 20% itakuwa inaishi vijijini. Katika miaka 50 iliyopita yamekuwepo
mabadiliko madogo sana ya watu kuhamia mijini ingawa kasi ya kuhamia mijini
inaongezeka lakini bado 80% na huenda hata zaidi wanaishi vijijini hivi sasa.
Kama hali itaendelea kuwa hivi, basi katika kujenga taswira ya hali ya mambo
itavyokuwa tunaweza kukadiria kwamba 50% ya Watanzania watakuwa wanaishi mijini
mwaka 2061. Hii ina maana kwamba watu milioni 202.5 gawa kwa mbili utapata
idadi ya watu 101.25 watakuwa bado wanaishi vijijini wakitegemea kilimo kama
ajira yao kuu.
Je tutakuwa na ardhi ya
kukidhi mahitaji ya watu hawa kwa mnasaba wa kasi ya ukodishaji ardhi iliyopo?
Hapa ndipo unahitajika umakini wa hali ya juu sana katika kuangalia hatima ya
Tanzania na watu wake. Kwa mtizamo uliopo sasa Tanzania ya 2061 itakuwa na
mgogoro mkubwa sana wa ardhi zaidi ya ule wa Zimbabwe.
Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/kaburi-la-mbaguzi-nambari-wani-cecil.html
Taarifa zinazohusiana na hizi:
http://muhunda.blogspot.com/2010/07/kaburi-la-mbaguzi-nambari-wani-cecil.html
No comments:
Post a Comment