Tembelea Butiama

Tembelea Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Karibu Butiama / Welcome to Butiama

Kurasa Muhimu

Thursday, September 30, 2010

Tuma taarifa za uchaguzi kwa njia ya mtandao na simu

Taarifa hizi nimepata toka kwa Steven Nyabero wa Vijana FM na inaelezwa kuwa ni njia ya kutumua taarifa mbalimbali ambazo zinahusiana na uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Kwa mujibu wa maelezo yake:

"Vijana FM inatumia Crowdmap, chombo kilichotengenezwa na Ushahidi, kukusanya taarifa, mawazo na uzoefu wakati wa Uchaguzi Mkuu Tanzania. Ni matarajio yetu kwamba chombo hiki kitawapa jukwaa watu kutoa taarifa, maoni, kuanzisha mijadala na kueneza ujuzi wa mchakato wa uchaguzi na matukio mbalimbali."
Anaendela:

Taarifa zinaweza kuwasilishwa kwa njia tatu:

  1. Kwa kutuma barua pepe: TZelect (at) gmail (dot) com
  2. Kwa Twitter hashtags #TZelect au #uchaguzitz (Shukrani Jamii Forums)
  3. Kwa kujaza fomu kwenye tovuti

Wednesday, September 29, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya saba kati ya kumi)


Jumamosi 23 Agosti 2008
Tuliamka kukiwa na hali nzuri ya jua na tukaanza mpando mmoja mkali kuelekea Kambi ya Barafu. Nagundua mabadiliko kidogo; najihisi kama nina nishati ya ziada kidogo. Hii itakuwa ni Red Bull. Nilijadiliana kwa kirefu na Yahoo uwezekano wa kuleta watu wengine kupanda Mlima Kilimanjaro mwakani iwapo nitafanikiwa kufika kileleni. Hii itakuwa Red Bull iliyonipa ujasiri wa kufikiri kuwa upo uwezekano kwangu wa kufika kileleni.

Tulifika Kambi ya Barafu (iliyopo mita 4,600 juu ya usawa wa bahari) ikikaribia wakati wa mlo wa mchana na tukala saa 8 mchana. Najihisi kama, kadiri siku zinavyopita, mwili wangu unaanza kuzowea hali ya kuwa kwenye nyanda za juu. Yahoo, pamoja na kuwa kila wakati anazungumzia mikakati ya kujitoa iwapo nitashnidwa kuukabili Mlima, amesema kuwa naonekana mwenye hali nafuu leo.

Kwenye kambi ya wahifadhi kuna mtu alikuwa anauza makopo ya bia ya Kilimanjaro kwa Sh.3,000 kila moja, na bei hiyo hiyo kwa Coca Cola. Ukilinganisha ni jinsi gani tulivyo juu kutoka usawa wa bahari, unaweza kusema kuwa bei hizo ja juu ni muafaka kabisa.

Tulikutana tena na kundi la wale vijana wa Kijerumani, waliyotupita karibu na Lava Tower jana, wakiteremka kutoka kileleni. Niliambiwa kuwa walipitiliza Kambi ya Karanga [kambi ambayo sisi tulilala] na yawezekana kuwa walilala kwa saa chache tu kwenye Kambi ya Barafu kabla ya kuanza kuelekea kileleni.

Leo hii nina uzoefu wa kutosha wa kupanda milima kiasi cha kuweza kutoa ushauri kwa wanafunzi wasiyo wazoefu. Siwezi kupendekeza kupanda Mlima huu kwa mtu ambaye:
  • hafanyi mazoezi mara kwa mara
  • hawezi kustahimili hali ya baridi
  • hukaa ofisini kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa na kuhamia kwenye kaunta ya baa kati ya Ijumaa na Jumapili
  • saa chache baada ya kuanza kutembea atafikiri, "Hivi huku nimefuata nini? Naweza kuwa kwenye chumba chenye joto, napata laga yangu moja baridi, na nikiangalia kwenye luninga ligi ambayo hupendelea sana kuangalia."

Ukikusudia kupanda huu mlima lazima uwe unasukumwa na jambo moja zito sana. Mimi nimechagua kuchangisha pesa kwa ajili ya elimu. Nimekuwa najaribu kufikiria kwa nini mtu yoyote awe tayari kulipa pesa na ajiingize kwenye fatiki kubwa kiasi hiki na bado nakosa jawabu. Naweza kuandika orodha ndefu ya marafiki zangu, wanafamilia, na washirika wangu ambao hawatakuwa tayari hata kulipwa pesa kuja kupanda mlima huu.

Kesho, nitafahamu iwapo ninazo sifa za kuweza kufika kwenye kilele kirefu kuliko vyote vya bara la Afrika. Leo, tunauona mlima vizuri kabisa na naanza kuhisi kuwa kesho nitapambana na kasheshe isiyo ya kawaida. 
Naanza kutafakari msemo niliyousikia kuwa "kupanda Mlima Kilimanjaro ni mtihani wa kisaikolojia zaidi kuliko wa maguvu." Ninavyautazama mpando mkali wa kesho, naanza kuelewa uzito wa usemi huo:
Nimesimama mbele ya Mlima Kilimanjaro katika safari ya kuelekea Kambi ya Barafu

 inawezekana vipi kwa mtu yoyote ambaye anapanda mlima huu kwa mara ya kwanza kushindwa kuelewa uzito huo.

Wakati najiandaa kulala joini namwambia Le kuwa mpaka sasa sehemu ngumu kabisa ya kupanda mlima huu inanikumba ninapokwenda chooni. Nikiwa nyumbani ninayo fursa, ambaye nadra kuitumia, ya kufungua gazeti na kulisoma nikiwa maliwatoni; hapa Kilimanjaro nalazimika kuchuchumaa. Mimi napata shida kubwa kuchuchumaa sehemu yoyote, wacha mlimani. Kwa hiyo kuchuchumaa mita 4,600 juu ya usawa wa bahari ni mtihani mkubwa sana kwangu.

Kwenye nyanda za juu hata kufunga kamba za viatu inahitaji kuhenyeka kwa hali ya juu. Asubuhi nafunga kamba ya kiatu kimoja halafu inabidi nipumzike na kuvuta pumzi kwa kama dakika tano hivi kabla ya kufunga kamba ya kiatu cha pili. Kwenda chooni inahitaji mara mbili ya nguvu inayotumika kufunga kamba za viatu.

Leo nilishuhudia wakweaji watatu wakiwasili Kambi ya Barafu na nikaona nyusa zao zilizogubikwa uchovu mkubwa na nikawaza: kama hivi ndivyo na mimi huonekana kila ninapofika kambini baada ya kutembea kwa siku nzima, basi kupanda huu mlima siyo mchezo hata kidogo.

Nimeshaamua kuwa huu mlima ni wa kupendezesha macho tu na wa kusifiwa kwa mbali, na pengine wa kusifiwa na kutazamwa kwenye picha lakini, kwa hakika, siyo mlima wa kukwea hata kidogo.

Makala ijayo: Kilele cha Uhuru na Kambi ya Crater


Makala zinazohusiana na hii:

Tuesday, September 28, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya sita kati ya kumi)

Alhamisi 21 Agosti 2008
Tulianza na mpando wa taratibu kutoka Kambi ya Shira (iliyopo mita 3,400 kutoka usawa wa bahari) na tutafika na kupita Lava Tower (iliyopo mita 4,600 juu ya usawa wa bahari). Wenye nishati ya ziada wanaweza kukwea Lava Tower ambayo nilikadiria ina urefu wa mita 500 juu ya njia ya kuelekea Kambi ya Barranco, kikomo cha safari yetu kwa siku ya leo. Tulikutana na kundi la vijana wa Kijerumani wakiteremka toka Lava Tower.
Taswira ya Mlima Kilimanjaro kutoka upande wake wa mashariki

Ilikuwa ni mteremko mmoja mrefu na wa kuchosha kutoka Lava Tower kuelekea Barranco (iliyopo mita 3,950 kutoka usawa wa bahari) ambako nilikutana na wahifadhi wawili, wote wakiwa wanamazingira, na ambao walionyesha shauku kubwa kujua kusudio la msafara wangu. Kwanini nilikuwa napanda Mlima Kilimanjaro? Nikifanikiwa kufika kileleni nitapanda milima mingine, kama Meru, au Oldoinyo Lengai? Mmojawapo aliniambia kuwa yeye ni Mmasai na aliniambia kuwa ana jina refu kama langu. Aliniambia kuwa mwenzie ni kutoka wa kabila la Wairaqi.

Jioni wakati wa tathmini ya siku nilihisi kama Yahoo alihisi kuwa ninapata shida kupanda mlima baada ya yeye kushauri kuwa mimi nitumie njia tofauti ya kuteremka badala ya ile njia ambayo Jose' alipendekeza na ambayo Le alikuwa na shauku ya kuitumia. Yahoo alisema pengine itabidi nichukue njia ya moja kwa moja kuelekea lango la Mweka badala ya kutumia njia ya Machame iliyopendekezwa na Jose'.

Nilikubali. Kiongozi wa msafara ndiyo hufanya maamuzi yote ya mwisho kwa kuzingatia tathmini yake kwa kila moja na ingawa sikujihisi kuwa nimefikia kikomo cha uwezo wangu, sikuwa na nguvu ya kutosha kuanza kubishana nae baada ya kutembea kwa siku nzima. Labda nitakuwa na maoni tofauti kesho asubuhi.

Ijumaa 22 Agisti 2008
Nimeamka nikijisikia na hali nzuri zaidi leo. Tulianza kutembea tukiwa mbele ya jabali ambalo nakisia lilikuwa na urefu wa mita 750. Hii, Pius alituambia, ndiyo inaitwa "Mpando wa Kifungua Kinywa" Kutokana na ugumu wa mpando huu alisema mara tutakapofika kule juu tutajihisi kuwa tunahitaji kupata tena kifungua kinywa. Alituambia kuwa wakweaji wengi huwa wakifika hapa hukata tamaa na kuteremka kurudi Moshi. Na cha kustaajabisha ni kuwa hii ni njia ambayo mwasisi mmoja aliamua kuwa, kama ambavyo Le anapenda sana kutamka, inawezekana kupita.

Pius alituambia kuwa alikaribia kuacha kazi yake kama muongozaji wa misafara ya kupanda Mlima Kilimanjaro alipoambiwa kwa mara ya kwanza kuwa Mpando wa Kifungua Kinywa ndiyo njia pekee ya kuelekea kileleni kutokea hapa. Katikati ya kupambana na Mpando wa Kifungua Kinywa tulifika eneo linaloitwa Busu la Mwamba ambapo unakumbatia uso wa jabali ili kujinusuru kuanguka na kuepuka mauti.

Sehemu ya mwisho tulipokaribia Kambi ya Karanga (iliyopo mita 3,963 juu ya usawa wa bahari) ilikuwa ni mpando mwingine mrefu na wa kuchosha. Kutokea Karanga tuliweza kuuona Mlima Kilimanjaro kama ambavyo wengi tumozoea kuuona. Kadiri tunavyozidi kuelekea mashariki, tunapata taswira tofauti ya mlima kila siku. Kabla ya kulala, nilikunywa mojawapo ya kopo moja ya Red Bull na nilisumbuka sana karibu usiku mzima. Asubuhi Pius alituambia kuwa yawezekana kuwa usiku nyuzi joto zilishuka chini ya kiwango cha kugandisha maji.

Makala ijayo: Athari za Red Bull


Makala zinazohusiana na hii:

Monday, September 27, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya tano kati ya kumi)

Jumanne 19 Agosti 2008
Tulipanda gari kutoka Moshi tukielekea upande wa Arusha halafu tukakatiza kuelekea Machame kwenda eneo la kuanzia safari yetu. Nilisikitika kuwa mawingu yalituzuwia kuuona vizuri Mlima Kilimanjaro. Wahifadhi 

Le, akiwa nje ya mahema yetu ya kulala
Kilimanjaro walikagua vifaa vya wasindikizaji wetu kwenye lango la Londorossi. Kundi letu lilikuwa na wabeba mizigo 9, Yahoo, na msaidizi wake.

Wabeba mizigo wa Mlima Kilimanjaro wanafanya kazi katika mazingira magumu na wanabeba mizigo mizito  ya mahema, mifuko ya kulalia, chakula, na maji ili kutuwezesha sisi kufika kilele cha Uhuru katika mazingira ya starehe. Hata hivyo, mazingira yao magumu yanasababisha athari siyo tu kwa afya zao ila na hata kwa maisha yao. Tulisimuliwa hadithi ya wabeba mizigo waliokuta mauti kutokana na kutokuwa na mavazi muafaka ya kuhimili baridi.

Mlima Kilimanjaro unaonekana kwa mara ya kwanza baada ya kutoka eneo la msitu.
Tuliteremshwa mwisho wa barabara mbaya, aina ya barabara ambayo inapitika na magari yaliyotengenezwa mahususi kukabili barabara za aina hiyo. Tulianza na mwendo wa kutembea wa kasi ndogo kabisa ambayo sijawahi kuona tangu nianze kujifunza kutembea. Yahoo, akiwa mbele yetu, ndiye aliyepanga hiyo kasi ambayo tuliendelea nayo kwa muda wa saa nne. Katika siku zilizofuata, tulivyoanza kupambana na maeneo magumu ya mpando nilielewa umuhimu wa kasi ile ndogo ambayo inasaidia sana kupiga hatua ya wastani wakati wote. Usiku wa kwanza tulilala kambi ya Big Tree, tukiwa kati ya mbega kadhaa.

Tatizo kuu la usiku wa kwanza ni kulala mapema. Kujaribu kulala saa mbili usiku ilikuwa mateso, lakini kwa usiku wa kwanza tu. Katika siku saba zilizofuata nilikuwa na uchovu mkubwa sana kutokana na kutembea kila siku kiasi ambapo ningeweza kulala hata saa 6 mchana. Mtihani mwingine ulikuwa kulala ndani ya mfuko wa kulalia. Jaribu kufikiria kulala ndani ya zulia lililoviringishwa na uweze kupata usingizi. Wakati tukikaribia kumaliza safari yetu Le alipendekeza kuwa nitafute mfuko wa kulalia toka Australia ambao unatengenezwa na nafasi kubwa zaidi kwa mtumiaji.

Niliona ajabu sana kuwa wakati nahangaika kutafuta usingizi nilisikia jamaa anakoroma kutoka hema la jirani yangu.

Jumatano 20 Agosti 2008
Leo, naamini nilifanikiwa kutembea kwa mwendo mrefu kuliko yote ambayo nimewahi kutembea. Siamini hata Neslon Mandela amewahi kutembea kwa mwendo mrefu zaidi. Kuachilia saa moja ya mlo wa mchana katika kambi ya Shira, tulitembea kuanzia saa 1 asubuhi mpaka karibia saa 2 usiku, tukiwa tumepambanishwa na mpando mmoja mkali baada ya kumaliza eneo la msitu na kuelekea kwenye Uwanda wa Shira.

Sehemu ngumu kuliko yote kwa leo ilikuwa baada ya machweo wakati Yahoo alipotuonyesha mwanga uliyokuwa mbali juu ya safu ya kilima na akasema ndiyo kikomo cha safari yetu kwa leo. Ilikuwa ni mpando mgumu ambao ulikuwa kama hauelekei kwisha. Ilifika wakati nilimpa Yahoo mfuko wangu wa mgongoni na nilimalizia safari bila mzigo. Baada ya hapa nilianza kuwa na hofu kuwa pengine sitaweza kufika kileleni.

Ingawa sikusumbuliwa na baridi nilihisi kupungukiwa pumzi, na Yahoo aliniambia kuwa hizo zilikuwa dalili za ugonjwa wa nyanda za juu unaosababishwa na upungufu wa oksijeni. Alisema baadhi ya dalili za mgonjwa mahututi ni pamoja na rangi ya ulimi kugeuka kijani.

Makala ijayo: Tunaelekea kambi ya Barranco na "mpando wa kifungua kinywa".


Makala zinazohusiana na hii:

Sunday, September 26, 2010

Kikwete ahutubia Musoma Mjini kwenye kampeni za uchaguzi

Jana, mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, alihutubia umati wa wananchi wa Musoma Mjini katika ratiba yake ya kampeni ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba mwaka huu.


Mgombea urais wa CCM akihutubia mkutano wa kampeni za uchaguzi kwenye kiwanja cha Shule ya Msingi Mukendo jana mjini Musoma 
Katika hotuba ambayo ilitanguliwa na hotuba fupi za mbunge aliyemaliza muda wake wa CCM kwa jimbo la Bunda, Stephen Wassira, na ya mbunge mwingine wa CCM aliyemaliza muda wake katika jimbo la Musoma Mjini, Vedasto Mathayo, na ya Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, Rais Kikwete alitoa ahadi mbalimbali za chama chake kwa wapiga kura iwapo atachaguliwa kuongoza tena kuanzia Oktoba.

Aidha, aliorodhesha yale aliyoyataja kama mafanikio ya serikali yake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwenye sekta za afya, maji, umeme, barabara, kilimo na ufugaji.

Ahadi nazo zilikuwa nyingi tu katika sekta zote muhimu, zikiwa ni pamoja na kumalizia ujenzi wa hospitali ya Kwangwa iliyopo Musoma; mpango wa kuongeza matumizi ya serikali kupambana na ugonjwa wa Malaria kwa matumizi ya chandarua, pamoja na kunyunyuzia dawa za kuua mbu. Alitaja pia mpango wa ushirikiano na nchi ya Cuba, nchi ambayo ilifanikiwa kufuta malaria kwa dawa zinazoshambulia mbu katika maeneo ya kuzalia.


Mgombea urais wa CCM alisema:
Nimekuja tena kuwaomba CCM iendelee kuongoza nchi yetu. Sababu ziko nyingi, nitataja mambo matatu. La Kwanza, hakuna chama kama CCM. Vyama vya siasa viko vingi, lakini kwa muundo, kwa mtandao, kwa sera, kwa mipango, mipangilio na uendelezaji hakuna hata kimoja kitaikaribia CCM.
Pili, tunaingoza vizuri nchi hii. Nchi imetulia, mafanikio yanaonekana dhahiri. Tanzania ilivyokuwa mwaka 1961 sivyo ilivyo leo, ilivyokuwa mwaka 2005 sivyo ilivyo leo. Na katika miaka mitano hii tumefanya mambo mengi ambayo huko nyuma yalionekana hayawezekani, tumeyaweza.
Tatu, sisi waaminifu.

Katika hotuba yake hawakusahau kina mama:
Wakipewa nafasi kina mama wanaweza. Kina mama niliahidi tutawapeni nafasi, mawaziri wengi katika baraza langu kuliko wakati mwingine wowote katika historia, majaji wengi. Kila mahali, tuliahidi [asilimia] hamsini kwa hamsini. Bunge lijalo wanawake watakuwa [asilimia] hamsini, na kina baba watakuwa [aslimia] hamsini.
Aliendelea:
Tuliahidi kuborehsa upatikanaji wa huduma mbalimbali: elimu, afya, maji, barabara, umeme, mitandao ya simu, na kadhalika.

Mwaka 2005, sekondari za Musoma zilikuwa na vijana 3,000. Leo sekondari zina vijana 10,777. Ameeleza mheshimiwa mbunge kuwa ziko changamoto za walimu, vitabu, maabara, na nyumba za walimu. Ni kweli. Lakini ni changamoto za maendeleo. Lakini sisi tumejiandaa kuikabili changamoto hiyo na tumepata mafanikio makubwa.

Tuliamua kupanua mafunzo ya ualimu katika vyuo vikuu, na vyuo vya ualimu kwa ngazi ya diploma. Mwaka 2005 tulikuwa tunapata kutoka vyuo vikuu walimu wasiozidi 600. Mwaka huu tutatoa walimu 12,124. Si mafanikio madogo. Ni mambo yanayofanywa na watu makini kama sisi, na yanatekelezwa na serikali makini kama serikali ya CCM.

Mwakani kila shule ya sekondari itapata walimu wasiopungua watano. Chuo Kikuu tulichojenga Dodoma kitatoa wanafunzi 40,000. Kati ya hao 15,000 ni wanafunzi waliyosomea ualimu. Tatizo la ualimu lipo?
Waliyomtangulia walisema yafuatayo:

Alianza Stephen Wassira:

Stephen Wassira, mgombea ubunge wa CCM kwa jimbo la Bunda, akihutubia wakazi wa Musoma jana
Watu wengine nao wamesema wanataka tuwachague. Lakini kilichonishangaza wakati nafuatilia maneno yao, nikagundua wanawadanganya Watanzania kwa ahadi za uongo. Mmoja anasema, 'mkinichagua mabati yatakuwa shilingi elfu tano.' Sasa mimi namuuliza: pale Ikulu kuna kiwanda cha mabati? Maana mabati ni bidhaa, inatengenezwa katika mazingira fulani ya uchumi. Kuna masuala ya gharama ya kuzalisha mabati hayo. Kuna gharama ya kusafirisha. Kuna mambo ambayo yako nje kabisa hata ya uwezo wa rais wa Watanzania. Bei ya mafuta ikipanda, huyo rais wa mabati ya shilingi elfu tano atayafanyaje? Anaongopa....Huyu anadanganya, tena anadanganya mchana.
Akafuatia Makongoro Nyerere:
Leo amekuja mgombea wetu wa urais, na kila harusi huwa haikosi wasindikizaji.Ukifika kwenye stendi ya mabasi kuna watu kadha wa kadha ambao wanashughulikia shughuli ya usafiri. Wapiga debe wapo, makonda wapo, na madereva wa magari wapo. Wewe ukifika pale stendi, hela yako unampa mpiga debe? Utafika? Usimpe hela yako mpiga debe, maana yeye ni mpiga debe tu. Mpe hela yako konda.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, akiwa jukwaani muda mfupi kabla ya kumkaribisha mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete, kwenye mkutano wa jana.
Leo mtu anataka kuwa raisi wetu aende akauweke mwenge [wa Uhuru] stoo. Halafu anakuja hapa anadanganya wana Musoma wenzangu eti yeye anamuenzi Nyerere. Wewe unamuenzi Nyerere mwenge wake unataka kwenda kuuweka stoo, ndiyo ujanja wako huo?


Akamalizia Vedasto Mathayo:

Katika kipindi cha miaka mitano...ilani ya uchaguzi tumeweza kuitekeleza barabara, tumeitekeleza kwa asilimia tisini. Mwaka 2005, tulisema kwamba lazima tuendelee kuboresha huduma za kijamii, na tukasema: kipaumbele chetu cha kwanza tutakipeleka kwenye elimu. Ilani yetu ya uchaguzi ilikuwa inatuagiza 2005 - 2010 kila kata iwe na sekondari moja. Kazi hiyo tumeifanya vizuri...tunazo sekondari 15.

Rais Kikwete, kushoto, akiwa na mgombea ubunge wa CCM kwa jimbo la Musoma Mjini, Vedasto Mathayo, kulia, kwenye mkutano wa jana 
Hakuna mtoto wa Musoma Mjini hata mmoja aliyefaulu akashindwa kwenda sekondari. Pale ambapo wazazi hawana uwezo, Serikali ya Chama cha Mapinduzi kila mwaka kwa  Musoma Mjini, inasomesha watoto zaidi ya 250 bure.

Aliendelea kutaja mafanikio kwenye ujenzi wa barabara, sekta ya afya, na maji. Alimuomba mgomea urais wa chama chake aweke nguvu katika ujenzi wa barabara.

Friday, September 24, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya nne kati ya kumi)

Jumapili 17 Agosti 2008
Baada ya kuamua kuacha kupanda milima ya Upare niliendelea kujipa moyo kutokana na mawaidha ya Jose' akisema kuwa haina haja ya kuwa mkakamavu wa kiwango cha juu kabisa kuweza kukabili safari ya siku 7 hadi 8 ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa njia aliyoipendekeza, yaani Lemosho - Southern Circuit, Barafu, hadi kilele cha Uhuru. Njia hii ndefu inauandaa mwili kuzowea polepole hali ya kuwepo kwenye nyanda za juu na ndiyo njia yenye uhakika mkubwa zaidi ya kumwezesha mkweaji kufika kileleni.

Rafiki yangu Jose' ameshapanda Mlima Kilimanjaro mara 12 na angeungana nami mwaka huu kupanda tena mlima kwa mara ya kumi na tatu. Lakini kwa bahati mbaya aliumia kifundo cha mguu na hataweza kuja. Ameshawahi pia kukwea maeneo ya milima ya Himalaya hadi kufikia Mt. Everest Base Camp.

Aliniarifu kuwa Bw. Le Hu Dyuong, mhandisi mtaalam wa programu za kompyuta na raia wa Vietnam ataungana na mimi kupanda Kiliamnjaro. Le pia ameshawahi kufika Everest Base Camp na kabla ya kupanda Mlima Kilimanjaro alitoka kupanda Mlima Kenya. Le aliniomba niahirishe kuanza safari ya kupanda Kilimanjaro ili kutoa fursa kwake apumzike kwa siku chache baada ya kupanda Mlima Kenya. [Siku chache baada ya kupanda Kilimanjaro, alienda kupanda Mlima Meru]. Halafu akapumzika kwa majuma mawili na akaanza kufanya mipango ya kupanda Mlima Oldoinyo Lengai, lakini mipango haikukaa vizuri na hivyo hakuweza kupanda hiyo volkano.

Jumatatu 18 Agosti 2008
Asubuhi nilikutana na Le kwenye kituo cha basi cha mjini Moshi, akitokea Arusha. Tulifikia hoteli ya Springlands na wakati wa mlo wa mchana tulikaa meza moja na wanandoa raia wa Afrika ya Kusini waliohamia Manchester, Uingereza. Walituambia kuwa kupanda Kilimanjaro siyo mchezo, lakini ni jambo la manufaa. Walitushauri tujaribu kupitia Lava Tower tunapoelekea kileleni.

Jioni tulijumuika kwa ajili ya mkutano wa maandalizi na tukatambulishwa kwa jamaa mmoja mrefu mwembamba mwenye rasta ambaye ndiye kiongozi wetu wa msafara, anaitwa Pius. Alituarifu kuwa anajulikana pia kama "Yahoo" kwa wenzake.

Tulibishana naye kidogo alipotaka kushauri tupunguze siku za safari zilipendekezwa na Jose' na badala yake ziwe chache zaidi. Tulisisitiza kutumia muda ule ule tuliyopanga na hasa kulala kambi ya Barafu (kambi ya mwisho kabla ya safari ya kuelekea kileleni) ili kuiwezesha miili yetu kuzowea hali ya kuwa kwenye nyanda za juu na kuepuka athari ya upungufu wa oksijeni.

Nilimwambia Yahoo kuwa anaweza kuwa ana haraka ya kurudi Moshi ili aondoke na wageni wengine kueleka kileleni na kuweza kujiongezea kipato lakini, kwa bahati mbaya, alikuwa amepewa kazi ya kuongoza wakweaji wawili, mmoja asiye na uzoefu wa kutosha na mwingine ambaye alikuwa na uzoefu wa kutosha kuhusu ugonjwa wa nyanda za juu unaosababishwa na upungufu wa oksijeni na ambaye hakuwa tayari kuacha kuchukuwa tahadhari. Yahoo alikubali kwa shingo upande.

Baada ya kununua ramani ya Mlima Kilimanjaro kutoka dukani muuza duka alijaribu kuniuzia dawa ya mbu, lakini Le akamstukia na kupinga kuwepo kwa mbu kwenye Mlima Kilimanjaro. Watanzania tunatambua umahiri wa wakazi wa mkoa wa Kilimanjaro katika masuala ya kutafuta pesa. Kwa hakika, kama bado sikuwa natambua hilo, basi nilitambua leo kuwa ndugu zetu Wachaga walikuwa watu wenye ujuzi wa uuzaji usiyo wa kawaida.

Makala ijayo: Napiga hatua ya kwanza kuelekea kileleni

Bonyeza hapa kuisoma makala hii kwa Kiingereza

Makala zinazohusiana na hii:

Tuesday, September 21, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya tatu kati ya kumi)

Ijumaa 15 Agosti 2008
Niliondoka Butiama alfajiri, nikikusudia kuendesha gari hadi Mwanza kabla askari wa usalama barabarani hawajafika barabarani kukagua bima ya gari ambayo muda wake ulikuwa umeisha siku chache zilizopita. Tatizo langu ni kuwa niligundua wakati muda umeshapita kuhusu gharama kubwa za kupanda Mlima Kilimanjaro, na sikuwa na uhakika iwapo ningeweza kumudu kwa pamoja gharama za kupanda mlima na kulipia bima ya gari.

Nilipofika Mwanza nilipita ofisi ya Air Tanzania kuchukuwa tiketi yangu ya bei nafuu niliyopewa na Air Tanzania Corporation Limited (ATCL) ikiwa ni mchango wao kwa The Mwalimu Nyerere Charity Climb 2008 kwa kunisafirisha toka Mwanza hadi Kilimanjaro, na kurudi Mwanza. Nahisi kama mzaha kuwa masikioni tukio lenyewe linasikika kama tukio moja kubwa sana la kuchangisha pesa, lakini ukweli ni kuwa ni mimi peke yangu tu, mtu mmoja ambaye nimejiingiza kwenye utata wa kukwea Mlima Kilimanjaro. Mimi ndiyo nilkuwa kampeni nzima. Nilipanda ndege kuelekea Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro jioni.

Jumamosi 16 Agosti 2008
Niliamka mapema kutuma makala yangu kwenye gazeti la Sunday News nikiwa nimechelwa tena, kama kawaida. Ninalo tatizo kubwa la kupata mada mpya ya kuandika kila juma kwa ajili ya makala yangu. Natumia sehemu kubwa ya juma kufikiria jambo ambalo naweza kuandika kwenye makala yangu na inapofikia wakati wa kukaa chini na kuandika makala yenyewe, nakuwa nimeshavuka muda uliyowekwa wa kuwasilisha makala. Faida mojawapo ya kupanda Mlima itakuwa nitafanikiwa kukamua mada zaidi ya moja kwa ajili ya kuandikia kwenye makala yangu.

Niliongea na Zainab Ansell, mmiliki wa Zara Tanzania Adventures na kaniambia kuwa kamuni yake imeamua kunilipia gharama zote za siku nane za kupanda Mlima Kilimanjaro zinazofikia dola za Marekani 1,500. Nilifurahi sana.

Jioni, rafiki yangu toka Mwanga alinitumia gari kunichukuwa Moshi na nikalala kwenye chumba ambacho kilikuwa na takriban mbu mia moja. Nilitumia zaidi ya saa nzima kuwapunguza wale mbu kwa kutumia mbinu inayojulikana kama kombora la nguo. Mbinu hiyo inahusisha kusubiri mbu atue kwenye ukuta halafu kufurumisha dhidi ya ukuta nguo na kumbamiza ukutani na kumuua. Kwa kadiri ninayofahamu, ndiyo njia iliyo rafiki zaidi kwa mazingira ya kumaliza mbu.

Taarifa ijayo: Nakutana na Le, mtu aliyebobea kupanda milima, na Yahoo, muongozaji wetu wa mlimani.
Makala zinazohusiana na hii:

Sunday, September 19, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya pili kati ya kumi)

Mwaka 2007 ilivyoonekana kuwa nilikuwa nimepoteza fursa nyingine ya kupanda Mlima Kilimanjaro niliamua kuweka nguvu ya ziada, ama sivyo ningeendelea kuota tu kufika kilele cha Uhuru. Nilipaswa kujiweka katika hatua ya kutorudi nyuma. Niliamua kuwaambia watu wachache kuwa nitapanda Mlima Kilimanjaro mwaka huu kuchangisha pesa kwa ajili ya elimu. Wa kwanza kumueleza hayo alikuwa mwalimu mkuu wa Sekondari ya Wasichana ya Chief Edward Wanzagi iliyo jirani na Butiama na akaniambia, "Kwa nini usichange pesa kwa ajili yetu? Tunahitaji mabweni ya wanafunzi."

Aidha, niliandika barua pepe kwa Howard Chinner, mkazi wa Sevenoaks, England, ambaye nimekuwa nawasiliana nae baada ya yeye kusoma moja ya makala zangu. Alipendekeza naweza pia kuchangisha pesa kwa ajili ya Village Education Project Kilimanjaro (VEPK) iliyopo Mshiri, Marangu, kwenye miteremko ya Mlima Kiliamnajro.

Ilikuwa ni kutokana pia na pendekezo lake kuwa tukio ambalo lingekuwa halina hata jina, likihusisha kupanda mlima mrefu kuliko yote duniani inayosimama pekee (milima mirefu zaidi ya Kilimanjaro, kwa mfano Mlima Everest, ni mkusanyiko wa milima zaidi ya mmoja), lilipata jina la The Mwalimu Nyerere Charity Climb. Baada ya kuanza safari ya kuelekea kileleni, na kadiri nilivyoendelea kujenga matumaini yangu kuwa nitafika kileleni, niliamua kupachika "2008" kwenye jina hilo, nikiashiria kuwa litakuwa ni tukio la kila mwaka.

Kwa ahadi hizo mbili (moja kwa Skondari ya Chief Edward na nyingine kwa VEPK) haikuwezekana tena kutafuta sababu  ya kutopanda mlima. Baada ya hapo nilituma barua pepe kwa wote niliyofikiri wangekuwa na utashi wa kuchangia mojawapo wa walengwa wa mchango huo wa hisani. Nilipokea majibu ya kutumainia, na hiyo ikanizuwia zaidi kupanga mipango yoyote isiyojumuisha kipengele cha kupanda Mlima Kilimanjaro.

Kabla ya kupanda, nilitumia muda kidogo kuongeza uwezo wangu wa kuhimili kwata kwa kufanya mazoezi ya kutembelea baadhi ya vilima vya Butiama. Nilibadilisha mpango wangu wa awali wa kutembea kilomita tano nikizunguka msitu wa Muhunda, msitu wa nasaba wa Butiama, na kuanza kufanya safari ndefu zaidi za kwenda Mlima Mtuzu, nikiongeza kiasi cha kilomita tatu za ziada. Wakati nilipoanza kuzoea mazoezi yangu haya ya ziada, niliaanza kujenga imani kuwa mwili wangu ulianza kubadilika kuwa kifaa cha kutisha cha kupanda mlima.

Rafiki yangu mmoja anayeishi jirani na Mlima Kilimanjaro aliniambia kuwa imani yangu hiyo ilikuwa haina msingi, kwamba Butiama haina milima ila ina vichuguu tu, na kuwa ningetaka kupata picha halisi ya kupanda Mlima Kilimanjaro ningeipata kwa kumtembelea Mwanga na kukaa pale kwa muda nikikwea milima ya Upare.

Nilienda Mwanga na kukaa siku mbili, lakini sikupanda mlima wowote. Badala yake nilipumzika na kuomba kuwa nilikuwa imara kiasi cha kutosha kupanda Mlima Kilimanjaro.

Makala ijayo: Naondoka kijijini, na kuelekea mlimani.


Makala inayohusiana na makala hii:

Saturday, September 18, 2010

Mwenge umepita Butiama leo

Mbio za Mwenge wa Uhuru leo zimefika Butiama. Kama desturi ya mbio za mwenge katika miaka tangu kufariki Mwalimu Nyerere mwaka 1999, ratiba ya mwenge kila mwaka inahusisha kupitisha mwenge kwenye makazi ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Mwitongo, Butiama.

Kukaribisha mwenge leo Mwitongo alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, akiongoza baadhi ya wakazi wa kijiji cha Butiama.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Makongoro Nyerere, (mwenye shati la kijani) akimkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Geoffrey Ngatuni, kwenye tukio la mwenge kupita Mwitongo, Butiama.

Mwenge ukiingia Mwitongo, Butiama.

Makongoro Nyerere akipokea mwenge toka kwa mkimbizaji mwenge, Flatei Massay

Ulinzi wa mwenge siyo wa kawaida.

Ulinzi wa mwenge siyo wa kawaida.

Kiongozi wa mwenge, Dk. Nassoro Matuzya, akipandisha mwenge eneo la mwenge wa Mwitongo.
Kabla ya risala iliyotolewa na kiongozi wa mbio za mwenge, Dk. Nassoro Matuzya, Mwenge wa Uhuru ulipandishwa kwenye eneo ulipo mwenge wa Mwitongo ili kuwasha mwenge wa Mwitongo kwa kutumia Mwenge wa Uhuru.

Wakimbizaji mwenge baadaye walizuru kaburi la Mwalimu Nyerere lililopo Mwitongo.

Friday, September 17, 2010

Kisa cha kuacha kuvuta sigara: safari yangu ya kupanda Mlima Kilimanjaro (makala ya kwanza kati ya kumi)

Sikumbuki ni lini nilianza kupata wazo la kupanda Mlima Kilimanjaro, lakini inaweza kuwa ni miaka minane iliyopita.* Bila sababu yoyote ya msingi, niliamua nataka kupanda Mlima Kilimanjaro.

Kufikia uamuzi huo ilikuwa ni jambo rahisi kuliko yote, lakini kuetekeleza azma hiyo ilikuwa jambo tofauti kabisa. Miaka kadhaa ikapita na nikatambua kuwa bila kuchukuwa hatua madhubuti, kamwe nisingepanda huu mlima.

Miaka ilivyopita, niliibua sababu zaidi za kunisukuma kupanda huu mlima. Niliendelea kukutana na watu kutoka pembe zote za dunia ambao walikuwa wameshapanda Mlima Kilimanjaro na nikajihisi kunyimwa kufaidi hazina kubwa ya Watanzania ambayo watu toka nje wameweza kuivumbua wakati Watanzania wachache mno wanapanda Mlima Kilmanjaro. Nilifikia hatua nikaamua sitaweza kuvumilia tena hali ya kukutana na mgeni toka nje ambaye ameshapanda Kilimanjaro na nishindwe kumwambia kuwa hata mimi nimeshaupanda huo mlima.

Katika muongo uliyopita mengi yamesemwa na kuandikwa kuhusu ongezeko la joto duniani na athari zake kwa mazingira. Baadhi ya wataalamu wanatabiri kuwa kwa sababu ya ongezeko la joto duniani theluji za Kilimanjaro zitayeyuka katika muda siyo mrefu ujayo. Nilipata msukumo kupanda kilele kirefu kabisa cha Afrika kuona hiyo theluji kabla athari za maendeleo ya binadamu hayajaifuta toka kwenye uso wa dunia.

Lazime itamkwe kuwa kuna mtazamo tofauti unaoashiria kuwa barafu za Mlima Kilimanjaro zinapunguwa siyo kutokana na ongezeko la joto duniani, ila kwa sababu ya mkusanyiko wa sababu nyingine. [Bonyeza hapa kusoma makala ya Kiingereza yenye mtazamo huo tofauti].

Mwezi Agosti 2005 nilikutana na Jenerali (Mstaafu) Mirisho Sarakikya, aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na ambaye amebobea kwa kupanda Kilimanjaro. Ameshapanda Kilimajaro mara 46. Nilimuahidi kuwa ningeungana naye mwezi Septemba 2006 lakini sikuweza sikuweza kutimiza ahadi, na nikaendelea kusumbuliwa na maneno yake tulivyoona mwaka 2005: "Nitasikitika sana kama wewe ni kati ya wale Watanzania ambao hukutana nao mara moja na hatuonani tena."

Sababu moja inayoweza kuchangia Watanzania wachache kufika kwenye kilele ni gharama. Inagharimu wastani wa dola za Marekani 1,500 kulipia safari ya siku nane, gharama ambayo Watanzania wengi hawaimudu. Kuna idadi kubwa ya Watanzania wanaoweza kulipa gharama hizo, lakini swali ni iwapo wanayo azma ya kukabili kibarua cha kupanda ambacho, kwa binadamu yoyote wa kawaida, ni kibarua kigumu.

Nilishangazwa kugundua kuwa, mbali na waongozaji na wabeba mizigo, ilikuwa ni kama hamna kabisa Mtanzania kwenye Mlima Kilimanjaro. Yawezekana nilikutana na zaidi ya wageni 100 nilipopanda Mlima, lakini kati ya hao nilionana naMtanzania mmoja tu akielekea kileleni wakati nashuka. Kwa masikitiko, aliathiriwa na ugonjwa wa mwinuko unaoletwa na upungufu wa oksijeni na aliteremshwa kutoka mlimani kwa machela.

Makala ijayo: Maandalizi ya kupanda


* Hii makala ilichapishwa kwanza tarehe 18/10/2008, kwenye wavuti yangu ya lugha ya Kiingereza, From Butiama and Beyond

Wednesday, September 15, 2010

Mlima Kilimanjaro Novemba

Mwezi Novemba, mwaka huu, natarajia kupanda Mlima Kilimanjaro kwa mara ya tatu chini ya mpango wa kuchangisha pesa za hisani katika tukio ambalo linaitwa The Mwalimu Nyerere Charity Climb 2010.

Mwaka 2008 nilifanikiwa kuchangisha zaidi ya Sh.20/- milioni ambazo zilichangia ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Chief Edward Wanzagi iliyopo Buturu, Mkoa wa Mara.

Wanafunzi wa Sekondari ya Wasichana ya Chief Edward Wanzagi, mbele ya shule yao.

Mwaka 2009 nilipanda tena Kilimanjaro nikikusudia kuchangisha pesa kwa ajili ya asasi ya mjini Musoma, Community Alive, inayojishughulisha na kutoa msaada kwa watoto yatima ambao wazazi wao wamekufa kwa UKIMWI. Pamoja na kupata msaada mkubwa wa vyombo vya habari katika kuhamasisha uchangiaji, pesa zilizoahidiwa zilivuka kwa kiasii kidogo tu Sh.2/- milioni. Na sehemu yote ya hizo ahadi haikulipwa.

Mwaka huu bado haijaamuliwa mchango utakuwa kwa ajili ya madhumuni gani.

Mwaka 2008 nilipanda Kilimanjaro na raia wa Vietnam, Le Huyn. Mwaka jana nilipanda na Watanzania wawili: Notburga Maskini wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa), pamoja na Gerald Hando wa Clouds FM.

Mwaka huu Gerald Hando amesema atashiriki tena. Kundi zima litashirikisha wafuatao:

1. Jaffar Amin 
Jaffar Amin, akijaribisha miwani ya kuvaa wakati wa kupanda Mlima Kilimanjaro
2. Muhidini Issa Michuzi wa Blogu ya Jamii & 3. Fred Fredwaa wa Radio Free Africa
Muhidini Michuzi, na Fred Fredwaa Fidelis

4. Philipp Kissanga, raia wa Austria

Phillipp Kissanga, kulia
5. Matare Nyerere
Matare (wa tano kutoka kushoto) akiwa na timu yake ya mpira ambayo kiwanja cha nyumbani ni kwenye klabu ya Tazara, Dar es Salaam 
6. Amrani Batenga (Mfanyabiashara wa Mwanza)
7. Cutlat Mazengo (National Insurance Corporation)
8. Gerald Hando (Clouds FM)
9. Prof. Khoti Kamanga (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam)
10. Mustafa Othim (kutoka Nakuru, Kenya)
11. Salum Mwaimu (wa Channel10)
12. Mary Kalikawe (Mkurugenzi wa Kiroyera Tours)
13. Stefan Joham (raia wa Austria)
14. Makongoro Nyerere (Mwenyekiti wa CCM, Mkoa wa Mara)
15. William Rutta (Meneja, Kiroyera Tours) 

William Rutta
Katika taarifa zijazo, nitatoa maelezo na picha ya safari yangu ya mwaka 2008 kupanda Mlima Kilimanjaro.

Makala inayohusiana na hii:
http://muhunda.blogspot.com/2010/09/kisa-cha-kuacha-kuvuta-sigara-ari-yangu.html

Monday, September 13, 2010

John Mnyika wa CHADEMA anajibu hoja dhidi ya sera ya majimbo (sehemu ya pili na ya mwisho)

Hii ni sehemu na pili na ya mwisho ikijibu ya hoja ya Amani Millanga dhidi ya sera ya majimbo.

Katika makala hii, Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika, anaendelea kutetea sera ya majimbo ya CHADEMA.
-----------------------------------------------------------------------------------------------------------
Sera ya Majimbo: Afrika Kusini, Nigeria na mfumo mpya wa utawala Tanzania


na 

John Mnyika
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje (CHADEMA)

Hivi karibuni niliandika makala yenye [kichwa cha habari] "Sera ya majimbo na siri ya Maisha bora kwa kila Mtanzania'. Wengi wamenipigia jumbe mbalimbali za kunipongeza. Wengine wameniuliza maswali na baadhi wamepingana na hoja zangu. Lengo la makala yangu ya leo ni kujibu baadhi ya maswali hayo na kufafanua dhana na muktadha wa baadhi ya hoja nilizozitoa.

Nafurahi kwamba kuna waliopingana na hoja zangu si kwa sababu tu ya kubisha, ila wameingia katika viatu vya Watanzania wenye hofu kuhusu majimbo ama wanapotoshwa kuhusu majimbo. Na ni kweli kabisa. Na hasa baada ya kuzindua sera 'nzito' (heavy) kwenye uchaguzi na tena kuanzia kuitambulisha Kilimanjaro! Washindani wetu wakaitumia hii fursa kupotosha sera hii na kuwatia hofu wananchi. Uzuri ni kwamba hakukuwa na hoja zilizotolewa, zaidi ya kauli tu ni 'ukabila', italeta vita kama Nigeria, ni Ubaguzi, wengine watakosa rasilimali n.k. 

Sasa tuna miaka mitano ya kubishana kwa hoja. Na niliwahi kusema huko nyuma ukweli ukitamalaki aliyesema uwongo hutamani kujifunika kwa kiganja kama Adili na nduguze. Na hii ndiyo itawakumba viongozi wa juu wa CCM miaka kadhaa toka sasa. Changamoto kwetu sasa ni kuuhamisha mjadala huu kwa wananchi ili wafahamu undani wa mambo haya. Na nonavyoona sasa kuna masuala ambayo tumeanza kuelewana.

Wapo waliotoa hoja kwamba tusifanye kitu kwa kuiga! Ukweli ni kwamba hii haikuwa sera ya kuiga. Ilizuka kama wazo (idea) tu, kwamba kwa kuwa falsafa yetu ni nguvu ya umma, kwa nini tusipeleke mamlaka kwa umma. Tukajiuliza ni kwa njia gani, likaja wazo la kuwa na mfumo mpya wa utawala - ikiwemo suala la muundo mpya wa utawala (majimbo). 

Na kwa kweli ilikuwa ni eneo jipya kabisa kiasi kwamba kulikuwa na mitazamo tofauti kuhusu mfumo uweje. Katika harakati hizo ndio tulipoanza kuangalia pia je nchi nyingine zinafanyaje? (hii inakaribia na kuiga). Lakini hatukuingia kiundani sana kuchota mifano ya nchi nyingine kwa kuwa hata muda huo hatukuwa nao. Kwa hiyo tukafikiria kwa kadiri ya mazingira yetu. Tukaingia kwenye uchaguzi, CCM wakaanza kupotosha kwa kutumia mifano ya nchi mbalimbali. Hapo sasa ikabidi kuingia kiundani hiyo mifano wanayotoa kwa nia ya kuwajibu, hapo ndipo mjadala sasa kwa pande zote ukaanza kutawaliwa na mifano ya nje (hapo ndipo hisia za kwamba tunaiga kujengeka). Lakini nilisema na narudia - sisi tulikuja na dhana ya uliberali/umajimbo wa kiutendaji (functional federalism).

Wapo waliojenga hoja kinzani kwamba nchi nyingi wanachukua ufiderali kwa sababu ya kutafuta UMOJA. Nakubaliana nao. Lakini UMOJA ni sababu moja tu. Hata sisi ni moja ya sababu kama msingi mmojawapo (rejea makala yangu ya awali). Lakini kila nchi ni zaidi ya hapo, pitia misingi ya ufiderali ya nchi mbalimbali utakubaliana na mimi.

Mchambuzi mmoja amechukua muda mrefu kupinga hoja zangu kwa kuzungumzia mfano wa Afrika Kusini na ubaguzi wa rangi (Apartheid). Kwa kufanya hivyo, nami hapa chini nitatota uchambuzi wangu kuhusu Afrika Kusini. Hoja kubwa iliyotolewa ni kwamba Afrika Kusini (SA) wamechukua muundo wa majimbo ili kukabiliana na ubaguzi wa rangi (Apartheid), na kwamba palikuwa na majimbo manne katika nchi hiyo ambayo yamegawanyika. 

Nakubali kuwa palikuwa na majimbo manne (kwa hiyo kama ingekuwa ni kwa lengo la kuunganisha majimbo kuleta umoja na kuondoa unbaguzi pekee kwa nini Afrika Kusini imeamua kuwa na majimbo tisa badala ya hayo manne?). Haya majimbo mengine matano yametoka wapi? Yameundwa kwa vigezo gani? Nitajadili suala hili kiasi hapo chini.

Wengine wamenijia huu [juu?] na kusema hawakubaliani nami katika mipaka yetu, imewekwa kiubaguzi. Kwanza niseme kwamba sijatamka bayana kwamba mipaka yetu imewekwa kiubaguzi. Nilichosema ni kwamba imetokea mara kadhaa watawala wetu kuweka mipaka ya kiwilaya bila kutoa sababu za kina na kuonekana kuwa ni misingi ya ukabila ama makabila. Niliwauliza maswali mawili ambayo kwa kuwa sikupewa majibu ya kina nimeona leo niyaulize rasmi kupitia makala yangu: "Unaweza ukaniambia ni kwanini Rais ameigawa wilaya ya Tarime kuwa wilaya mbili za Tarime na Rorya? Au unaweza kuniambia kwa nini wilaya ya Hai ambayo ni ndogo iligawanywa kuwa wilaya mbili za Hai na Siha (wilaya ambayo kwa idadi wa watu ni ndogo kuliko kata moja yenye watu wengi zaidi katika jimbo la Ubungo)?"

Mchambuzi mmoja ametoa hoja kwamba hatuna sababu ya kuweka mistari ya uwanja wa mpira wa kikapu (basketball) ilihali tunacheza mpira wa miguu (football). Na mchambuzi amehitimisha hoja yake kwa kuuliza kwa lugha ya Kiingereza sera ya majimbo 'for what' ambayo naweza kutafsiri "kwa ajili gani ama kwa nini?" Hii ni njia nzuri ya kujenga hoja kwa kutumia mifano, nami nitautumia mfano huu kufafanua hoja za awali.

Hapa kuna mambo mawili - Mosi, ni kwamba hii mistari tunayoita mistari hivi sasa ilichorwa na watu kama sisi (ila wao tunawaita watawala). Mistari ya nchi ilichorwa na wakoloni. Baadhi ya mistari ya mikoa na wilaya tukairithi toka kwao. Na mistari mingine watawala wakaanza kuichora. Na mingine wanaendelea kuichora. Mwaka juzi wakachora mstari kukatokea mkoa unaitwa Manyara. Na sasa nasikia wanataka kuchora zaidi.

Wasiwasi wetu ni kwamba wanaichora vibaya, bila shabaha (hawajibu swali FOR WHAT). Sisi tunataka ichorwe na wananchi kupitia mchakato wa kuunda katiba mpya. Iwe mistari ya wananchi kwa ujumla wao na kwa matakwa yao. Tunaweka wazi misingi ya ufiderali. Halafu kwa pamoja tuamue uweje na mipaka yake iweje.

Tunapotaja mipaka ya maeneo hivi sasa, mathalani ya Jimbo la Ziwa ama Jimbo la Kaskazini n.k., tunataja kama mawazo yetu tu na ili kurahisisha uelewa. Mipaka itakuwa ipi hili ni suala la wananchi kuamua. Tofauti na sasa ambapo Rais anaweza akalala akaamka akatangaza kugawa mkoa...na akateua anayemtaka kuwa mkuu wa mkoa ama akafanya hivyo kwa wilaya. Hakuna udhibiti, hakuna urari, hakuna ushiriki (No checks, No balance, No participation)....FOR WHAT, anaweza tu kuwajibu kwamba URAIS HAUNA UBIA, AMA NIMEFANYA HIVYO KWA MASLAHI YA UMMA, AMA NIMEFANYA HIVYO KWA MAMLAKA MLIYONIPA!

Mmoja ameandika kulalamika kwamba sera ya majimbo itaibagua "Singida". Nadhani Singida imetumika kama ishara (symbol) ikimaanisha maeneo ambayo hayana rasilimali. Mambo kadhaa yanajitokeza. Mosi, hakuna haja ya kufikiria sana kuhusu Singida - hakutakuwa na Jimbo linaitwa Singida. Singida ni mkoa wa hivi sasa ambao utavunjwa na kuunganishwa na maeneo mengine kuwa JIMBO LA KATI (Central Province). Itajumuisha maeneo gani itategemea idadi ya majimbo nchi nzima kwa mujibu wa uamuzi wa wananci. Lakini kama tukiwa na majimbo 8 au 9 basi Jimbo la Kati linaweza kuwa maeneo ya DODOMA, SINGIDA, MTERA, KILOSA n.k. Sasa wakazi wa maeneo haya watuambie je, kanda hii haitakuwa na rasilimali? Huku kuna Zabibu, mabwawa ya maji, mito, mbuga za wanyama, ardhi ya kilimo n.k.

Lakini nirudie ambacho niliwahi kukisema, na nakirudia tena - duniani kote RASILIMALI ni zaidi ya MALIASILI. Kuna majimbo (states) hazina MALIASILI lakini zinatumia RASLIMALI watu na upekee wake kufanya kwenda mbele. Kadiri Singida inavyoendelea kuwa tegemezi kwa Dar es Salaam (soma - serikali kuu) msitegemee maajabu ya Mussa. Hivi mpaka sasa DODOMA imetumiaje fursa ya kuwa Mji Mkuu wa Bunge kuleta maendeleo? (Hapa namaanisha, Dodoma sio mji mkuu wa Tanzania - huu ni mjadala mwingine tofauti). Ni wapi kwenye katiba pameandikwa kwamba mji mkuu ni Dodoma ama ni lini sheria ya bunge ilipitishwa kubadili makao makuu ya nchi kuwa Dodoma zaidi ya sheria njiti iliyoibuka baadae ya Mamlaka ya Maendeleo ya Mji Mkuu (CDA)?

Nimelalamikiwa kwa kutumia mifano ya nchi zilizofanikiwa. Nadhani ni kitu kizuri kutumia mifano mizuri na kujifunza kutoka katika mifano mibaya. Wachambuzi watupe nchi ambazo zimeshindwa kutokana na kutumia Mfumo wa Ufiderali. Nami nitatoa mifano ya nchi nyingi zaidi zilizofanikiwa kutokana na ufiderali na nchi zilizoshindwa kutokana na serikali kuu kuhodhi kila kitu (unitary).

Yupo aliyesema kwamba Nigeria haiendelei kutokana na majimbo. Wanaojua historia na mwelekeo wa nchi watakubaliana nami kwamba yanayotokea Nigeria si kwa sababu ya majimbo, tena ukweli ni kwamba kuna majimbo ambayo yamepitisha sheria za maendeleo (progressive laws) zinazowapa wananchi wake manufaa ya rasilimali. Kuna majimbo ambayo hayana msalie mtume na rushwa. Harakati (struggle) za Niger Delta si kati ya wananchi kwa wananchi, ni kati ya wananchi na watawala waliofunga ndoa na makampuni ya kinyonyaji. Ni struggle ambayo hata Tanzania inakuja, tuwe na mfumo wa ufiderali, tusiwe nao hatuwezi kuwazuia wananchi kudai raslimali zao.

Njia pekee ni kutambua hili kama tatizo la kiuongozi na kulishughulikia. Na kwa kweli muundo wa sera ya majimbo (in herent) unatambua suala la wananchi kumiliki ama kunufaika na rasilimali kama nilivyodokeza katika makala yangu iliyopita.

Sasa nirudi kwenye mfano wa Afrika Kusini. Nchi hii imepitia mchakato wa kuwashirikisha wananchi katika kuunda katiba yao tofauti na katiba ya Tanzania hivyo uamuzi wa majimbo ni wa wananchi. Nao ndio waliamua kuwa na majimbo tisa badala ya manne. Na ni kwa kuangalia sababu za ukubwa wa kimaeneo, rasilimali, historia, mamlaka n.k. Na hili si suala geni, Canada kwa mfano ilibuni mfumo wake wa majimbo mwaka 1867 (kwa sababu za umoja zaidi), lakini majimbo ya Canada yamekuwa yakibadilika, ama kuongezeka au wajibu wake kubadilika kutokana na mageuzi ya kijamii, ukubwa, dhima ya serikali, na maamuzi ya kimahakama.

Hii inathibitisha kwamba majimbo ya kiutendaji (functional federalism) sio ndoto. Ni kitu kinawezekana kwa lengo la kukidhi matakwa fulani (the FOR WHAT). Matakwa ambayo kwa mimi nimeyaainisha kwenye misingi tisa niliyotoa katika makala yangu iliyopita.

Chama ambacho kilikuwa kinapambana na ubaguzi wa rangi Afrika Kusini ni African National Congress (ANC). Kwa hiyo kama nia ya kuunda majimbo ingekuwa ni kupambana na ubaguzi wa rangi, ANC ingekuwa ya kwanza kutaka mfumo wa MAJIMBO/UFIDERALI. Lakini ANC ilikuwa inapinga majimbo (kama walivyo rafiki zao CCM wa Tanzania). Na walikuwa wanasema wanataka Mamlaka ya Serikali Kuu (unitary government) ili serikali kuu ya chama tawala ANC iweze kutoa huduma kwa wananchi kila mahali mathalani hospitali, shule na kuondoa tofauti za kiuchumi (hii ni hoja ambayo kwa kutamkwa ni tamu!).

Na ANC (kama ambavyo CCM inafanya sasa) ilikuwa ikisambaza propaganda kwamba neno FEDERALISM (MAJIMBO) ni la kibaguzi na la kimbari na kwamba linafanana na HOMELANDS, neno ililokuwa linayagawa maeneo kwa mujibu wa ubaguzi wa rangi (Ndio maana haishangazi kwamba kwenye katiba ya Afrika Kusnini hakuna neno FEDERALISM ingawa nchi imeundwa, inatambua na kufuata mfumo wa UFIDERALI).

Lakini nakubaliana na uchambuzi kwamba katika yale majimbo manne ya asili yapo ambayo yalikuwa yakitaka kujitenga mathalani KwaZULU Natal. Lakini mwisho wa siku wananchi waliupenda zaidi mfumo wa ufiderali.

Mwalimu [Nyerere] alitaka Serikali ya Mamlaka (unitary government) - hoja zake zilikuwa hizo hizo za serikali kuu kupeleka huduma kila mahali. Ametimiza wajibu wake katika wakati wake. Kuna mahali amefanikiwa, kuna mahali ameshindwa. Sasa, zimepita nyakati za dola kuhodhi uchumi (state centralized economy).

Sasa ni wakati wa watu (namaanisha wazawa na si wageni) kumiliki uchumi (people centred economy). Na huu ndio msingi wa falsafa ya nguvu ya umma na itikadi ya mrengo wa kati. Na hili nimelichambua katika misingi ya ufiderali ambao CHADEMA inapendekeza Tanzania tuufute [tuufuate?] Ndio maana naendelea kusisitiza kuwa pamoja na kuwa kipaumbele ni UONGOZI kuna uhusiano mkubwa baina ya MFUMO/MUUNDO WA UONGOZI na UONGZI wenyewe.

Na hili ndilo nashauri serikali inayoongozwa na CCM ilizingatie. Kama haitalizingatia basi wananchi wanapaswa kujulishwa mapema kwamba wakichagua CHADEMA wanachagua falsafa ya NGUVU YA UMMA kutumika katika utawala na UFIDERALI kuwa muundo - labda kama wananchi (ambao sio wote wanaunga mkono sera CHADEMA) au bunge (ambalo halitakuwa la CHADEMA peke yake) - WAKATAE wakati wa mjadala wa KATIBA MPYA! Wakati huo tutaamua kama tufuate Ufiderali uliogawanika (divided federalism) kama ilivyo Canada ama tufuate Ufiderali uliounganika (integrated federalism) kama ilivyo Ujerumai.

Naamini maoni yangu haya yataibua mjadala zaidi tuendelee kujadili, wananchi wengi zaidi wafahamu ukweli ili tukubaliane ama tukubaliane kutokukubaliana.

Taarifa zinazohusiana na hii:

Sunday, September 12, 2010

Jagwa Music waendeleza rirandi nchini Denmark

Jagwa Music ni kikundi ambacho kinapiga muziki wa Mchiriku, au Mnanda, kama vijana wengi wanavyopenda kuuita. Wasanii hawa sasa hivi wako katika ziara ya maonyesho mawili nchini Denmark.

Jana usiku walianza makamuzi ya kasi kubwa. Leo hii, kuanzia saa mbili usiku watakuwa katika mji wa Roskilde kwa ajli ya makamuzi mengine.

Ziara hii, itayakayohitimishwa tarehe 13 Septemba, ni kwa ajli ya kujitangaza kwa ajili ya maandalizi ya ziara nyingine ndefu hapo mapema mwaka 2011.


Waratibu wa safari hii ni kampuni ya Jahazi Music, na kwa maandalizi yote nchini Tanzania wanashirikiana na kampuni ya Maisha Music.


Mwenyeji wa ziara hii nchini Denmark ni kampuni ya GlobalCPH. Kikundi hiki kinamilikiwa na George Sultani Jolijo, na kusimamiwa na kampuni ya Maisha Music Tanzania Limited.